Championship 2025/2026: Vita ya Play-Off na Kushuka Daraja Yachukua Sura Mpya Raundi ya 29
Baada ya Geita Gold na Kagera Sugar kurejea Ligi Kuu Bara, Championship 2025/2026 inaingia raundi ya 29 kesho Jumapili ikiwa na mechi zote nane zitakazopigwa kwenye viwanja mbalimbali.
Raundi hii ina uzito mkubwa kwa sababu itatoa picha ya timu zitakazocheza ‘Play-Off’ ya kubakia Championship msimu ujao wa 2026/2027, pamoja na timu moja itakayoshuka moja kwa moja daraja na kuungana na Hausung FC ya Njombe inayoburuza mkiani.

Geita Gold, Kagera Sugar tayari Ligi Kuu
Kagera Sugar, iliyo nafasi ya pili ikiwa na pointi 68, tayari imekata tiketi ya kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga KenGold ya Mbeya mabao 3-0. Kagera itakuwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kuikaribisha Gunners ya Dodoma, ambayo ilichapwa mabao 2-0 na Bigman FC.
Kagera ilishuka daraja msimu wa 2024/2025 baada ya kudumu Ligi Kuu kwa miaka 20 tangu iliposhiriki mwaka 2005. Msimu huo, timu hiyo ilimaliza nafasi ya 15 ikiwa na pointi 23, ikishinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17.
Kikosi hicho kinachonolewa na Juma Kaseja, aliyewahi kuitumikia Simba, Yanga, Taifa Stars na pia Kagera Sugar kama mchezaji na kocha wa makipa, kimefanikisha kurejea Ligi Kuu baada ya mwenendo mzuri tangu mwanzo wa msimu.
Kwa upande wa Geita Gold, vinara hao wenye pointi 71 walirejea Ligi Kuu baada ya kuifunga Songea United mabao 3-1. Raundi hii, Geita itacheza dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
Geita Gold ilishuka daraja msimu wa 2023/2024, kisha msimu wa 2024/2025 ikamaliza nafasi ya nne kwenye Championship ikiwa na pointi 56 chini ya Kocha Mohamed Muya. Safari yao ya kurejea Ligi Kuu ilikwama baada ya kuondolewa kwenye ‘Play-Off’ na Stand United kwa jumla ya mabao 4-2.
Msimu huu, chini ya Kocha Mkuu Zubery Katwila, Geita Gold imefanikisha lengo la kurejea Ligi Kuu, huku ikiendelea kupigania kumaliza kama bingwa katika mechi mbili zilizobaki.
Polisi Tanzania na Mbeya Kwanza uso kwa uso
Moja ya mechi zinazobeba uzito mkubwa raundi hii ni kati ya Polisi Tanzania na Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.
Polisi inakutana na Mbeya Kwanza wakati timu zote zikiwa na pointi 60. Polisi ilikuwa nafasi ya nne, huku Mbeya Kwanza ikishika nafasi ya tatu, na tayari zimejihakikishia nafasi nne za juu zitakazowaweka kwenye mechi za ‘Play-Off’ kuisaka tiketi ya kurejea Ligi Kuu.
Polisi Tanzania inaingia kwenye mchezo huo baada ya kuchapwa bao 1-0 na Mbuni FC ya Arusha. Mbeya Kwanza, kwa upande wake, ina kumbukumbu nzuri baada ya kuifunga Stand United bao 1-0.
Msimu wa 2024/2025 haukuwa mzuri kwa Polisi Tanzania, iliyomaliza nafasi ya 10 kwenye Championship ikiwa na pointi 33. Timu hiyo ilishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, ikifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Polisi inaendelea kupambana kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022/2023, ilipomaliza nafasi ya 15 ikiwa na pointi 25, baada ya kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza 17.
Mbeya Kwanza nayo inaendelea na safari ya kutafuta nafasi ya kurudi Ligi Kuu. Timu hiyo ilishuka daraja msimu wa 2021/2022 baada ya kumaliza mkiani ikiwa na pointi 25, ikishinda mechi tano, sare 10 na kupoteza 15.
Hausung tayari imeshuka, Barberian ipo hatarini
Kwa upande wa mkia wa msimamo, Hausung FC ya Njombe tayari imekuwa timu ya kwanza kushuka rasmi daraja. Timu hiyo inaburuza mkiani ikiwa na pointi tisa na itakuwa ugenini kucheza na Songea United kwenye Uwanja wa Majimaji, Ruvuma.
Barberian FC nayo ipo kwenye hatari kubwa. Itacheza dhidi ya TMA FC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, ikiwa imetoka kuchapwa bao 1-0 na B19 FC. Ikiwa itapoteza tena, itashuka rasmi daraja na kuungana na Hausung FC.
TMA FC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali baada ya kuifunga African Sports ya Tanga mabao 2-0 katika mechi iliyopita.
Ratiba ya mechi za raundi ya 29 Championship 2025/2026
| Mechi | Uwanja |
| Kagera Sugar vs Gunners FC | Kaitaba, Bukoba |
| Geita Gold vs Stand United | CCM Kambarage, Shinyanga |
| Songea United vs Hausung FC | Majimaji, Ruvuma |
| Polisi Tanzania vs Mbeya Kwanza | Ushirika, Moshi |
| KenGold vs B19 FC | Halmashauri ya Chunya, Mbeya |
| African Sports vs Bigman FC | Mkwakwani, Tanga |
| TMA FC vs Barberian FC | Sheikh Amri Abeid, Arusha |
| Transit Camp vs Mbuni FC | Filbert Bayi, Pwani |
KenGold, iliyotoka kuchapwa mabao 3-0 na Kagera Sugar, itakuwa na kibarua dhidi ya B19 FC, ambayo inaingia na kumbukumbu ya kuifunga Barberian FC bao 1-0.
African Sports ya Tanga, baada ya kuchapwa mabao 2-0 na TMA FC, itacheza na Bigman FC ya Lindi. Bigman inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali baada ya kuifunga Gunners FC ya Dodoma mabao 2-0.
Mechi ya mwisho ya raundi hii itapigwa Uwanja wa Filbert Bayi, Pwani, ambapo Transit Camp, iliyotoka kuifunga Hausung FC bao 1-0, itacheza dhidi ya Mbuni FC, iliyotoka kuifunga Polisi Tanzania bao 1-0.
Raundi ya 29 ya Championship 2025/2026 inakuja wakati picha ya kupanda Ligi Kuu tayari imeanza kukamilika, lakini vita ya ‘Play-Off’ na kushuka daraja bado inaendelea kuamua hatima ya timu kadhaa kuelekea mwisho wa msimu.
Mapendekezo ya Mhariri:
- PSG Mabingwa Tena UEFA Champions League Baada ya Ushindi wa Penalti Dhidi ya Arsenal
- Liverpool Yaachana na Arne Slot, Iraola Apewa Nafasi Kubwa Kumrithi
- Ratiba Ligi Kuu Bara 2026 Yawagawa Wadau Baada ya Msimu Kusogezwa Hadi Juni 30
- Ratiba ya Kombe la Dunia 2026: Mechi Zote, Tarehe, Viwanja na Makundi
- Yanga Yaiingilia Azam Dili la Winga Mkongo Henoc Molia




```






Leave a Reply