Simba Bingwa Kombe la Shirikisho 2026 Baada ya Kuifunga Azam FC

Simba Bingwa Kombe la Shirikisho 2026 Baada ya Kuifunga Azam FC

Simba imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kuifunga Azam FC bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Jumamosi, Julai 4, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.

Ushindi huo umeifanya Simba kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho 2026, huku Wekundu hao wakimaliza ukame wa miaka mitano bila kutwaa taji hilo.

Bao pekee la mchezo lilipatikana dakika ya 62 baada ya Yahya Zayd wa Azam FC kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa adhabu uliopigwa na Elie Mpanzu.

Simba ilipata mpira huo wa adhabu baada ya Pascal Msindo kumuangusha Libasse Gueye nje kidogo ya eneo la hatari la Azam FC.

Simba Bingwa Kombe la Shirikisho 2026 Baada ya Kuifunga Azam FC

Azam FC Yashindwa Kusawazisha

Baada ya Simba kupata bao, Azam FC iliongeza juhudi katika kutafuta bao la kusawazisha, lakini safu ya ulinzi ya Simba ilisimama imara na kuondoa hatari zilizoelekezwa langoni mwao.

Mambo yalizidi kuwa magumu kwa Azam FC katika dakika ya 67 baada ya kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuonyeshwa kadi nyekundu na refa Sifu Amon.

Fei Toto alitolewa nje baada ya kumpiga ngumi Libasse Gueye, ambaye alikuwa akijaribu kumdhibiti wakati kiungo huyo wa Azam FC akiwa na mpira.

Simba iliendelea kulinda bao lake hadi mwisho wa mchezo na kutwaa taji hilo kwa ushindi wa bao 1-0.

Simba Yamaliza Ukame wa Miaka Mitano

Taji hilo ni la kwanza kwa Simba katika mashindano hayo ndani ya miaka mitano.

Kabla ya ushindi wa mwaka huu, Simba ilitwaa ubingwa huo Julai 25, 2021 baada ya kuifunga Yanga bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Simba pia imeendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo wa fainali katika mashindano hayo tangu yaliporejea msimu wa 2015/2016.

Katika kipindi hicho, Simba imecheza mechi nne za fainali na kushinda zote.

Azam FC Yaendeleza Nuksi ya Fainali

Kwa upande wa Azam FC, kichapo dhidi ya Simba kimeendeleza matokeo mabaya katika mechi za fainali msimu huu.

Kabla ya fainali dhidi ya Simba, Azam FC pia ilipoteza katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu.

Simba nayo imetumia ushindi huo kulipiza kisasi cha kuondolewa na Azam FC katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2022/2023, ilipofungwa mabao 2-1.

Safari ya mwaka huu imemalizika kwa Simba kutwaa taji baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, huku bao la kujifunga la Yahya Zayd likiamua fainali hiyo ya Gombani.

Soma Pia:

  1. Orodha ya Mabingwa wa Kombe La Shirikisho Tanzania
  2. Hiki Hapa Kikosi cha Azam Dhidi ya Simba Leo 04/07/2026
  3. Matokeo ya Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB
  4. Kikosi cha Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB
  5. Rekodi Zinavyoibeba Simba Dhidi ya Azam FC Fainali ya Kombe la CRDB
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo