Kikosi cha Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB

Kikosi cha Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB

Kikosi cha Mnyama Simba leo kitashuka dimbani katika mtanange wa kumsaka bingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB Federation Cup, maarufu kama Kombe la FA. Simba itachuana vikali dhidi ya Azam FC katika mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, leo Julai 4, 2026 kuanzia saa 11:00 jioni.

Ni fainali inayobeba heshima ya msimu kwa pande zote mbili. Simba na Azam zinaingia uwanjani zikitafuta taji lililosalia kwenye msimu ambao Yanga tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ikiwaacha wapinzani hao nafasi ya pili na tatu mtawalia.

KipengeleTaarifa
MechiSimba vs Azam FC
MashindanoFainali ya Kombe la Shirikisho CRDB
TareheJulai 4, 2026
MudaSaa 11:00 jioni
UwanjaUwanja wa Gombani, Pemba
Mwamuzi wa katiSifu Amoni kutoka Mbeya
Waamuzi wasaidiziHamdani Said kutoka Mtwara na Zawadi Yusuph kutoka Dar es Salaam
Mwamuzi wa akibaAhmed Arajiga kutoka Manyara

Kikosi cha Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB

Kikosi cha Simba vs Azam leo: mastaa wa kuangalia

Simba inatarajiwa kuingia kwenye fainali hii ikiwa na baadhi ya wachezaji wake muhimu waliobeba timu kwenye mechi za karibuni.

Kwenye eneo la mbele na kiungo, macho yatakuwa kwa Elie Mpanzu, ambaye amekuwa akitumika kama mshambuliaji wa mwisho, pamoja na Clatous Chama, Libasse Gueye na Anicet Oura.

Wachezaji hao wanatajwa kuwa sehemu muhimu ya nguvu ya Simba kuelekea pambano hili, hasa baada ya timu hiyo kuonyesha uimara kwenye safu ya kiungo na ushambuliaji katika msimu uliomalizika.

Kwa upande wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni moja ya majina yanayobeba uzito kwenye kikosi cha Florent Ibenge. Kiungo huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu waliopumzishwa kwenye mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji, ambao Azam ilishinda mabao 2-0.

Simba yafika fainali kwa kishindo

Simba imetinga fainali baada ya ushindi mkubwa wa mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa Juni 20, 2026 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Safari ya Wekundu wa Msimbazi kwenye michuano ya msimu huu ilianza hatua ya 64 bora, ambako waliifunga Greenland FC ya Kagera mabao 3-0. Katika hatua ya 32 bora, Simba iliiondosha B19 FC kwa ushindi wa mabao 2-0.

Hatua ya 16 bora iliikutanisha Simba na Dodoma Jiji, mchezo ambao Wekundu hao walishinda mabao 3-1. Robo fainali, Simba iliendelea na mwendo wake kwa kuifunga TRA United mabao 4-0 kabla ya ushindi mwingine wa 4-0 dhidi ya Coastal Union kwenye nusu fainali.

Azam yaivua Yanga ubingwa

Azam FC ilikata tiketi ya fainali kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Yanga kwenye nusu fainali iliyopigwa Juni 21, 2026 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Ushindi huo ulikuwa na uzito wa kipekee kwa Azam, si kwa sababu tu uliipeleka fainali, bali pia uliivua Yanga ubingwa wa michuano hiyo baada ya kutwaa taji hilo mara nne mfululizo.

Azam ilianza kampeni yake hatua ya 64 bora kwa kuifunga Endument FC ya Kilimanjaro bao 1-0. Katika raundi ya 32 bora, iliifunga Mbeya Kwanza 1-0, kisha ikaichapa Fountain Gate mabao 4-0 kwenye hatua ya 16 bora.

Kwenye robo fainali, Azam iliiondosha Mashujaa kwa ushindi wa bao 1-0 kabla ya kuifunga Yanga kwenye nusu fainali na kutinga mchezo wa mwisho wa msimu.

Presha ya taji kwa Simba

Simba inaiendea fainali hii ikiwa na lengo la kumaliza msimu kwa taji na kupunguza presha ya mashabiki wake baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC, uliosalia kwa watani wao Yanga kwa msimu wa tano mfululizo.

Kocha Steven Barker ameingia kwenye mchezo huu akiwa na rekodi nzuri tangu alipoanza kukiongoza kikosi hicho. Simba haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi wala Kombe la Shirikisho CRDB chini yake, huku kiwango cha timu hiyo kikitajwa kurejea kwenye ubora wake.

Nguvu ya Simba msimu huu pia imeonekana kwenye namba zake. Timu hiyo ilimaliza ligi ikiwa imeruhusu mabao 11 katika mechi 30, huku safu yake ya ushambuliaji ikifunga mabao 54.

Simba pia inasaka taji la pili msimu huu baada ya awali kutwaa Kombe la Muungano kwa kuifunga Yanga bao 1-0.

Azam yaitafuta heshima ya pili

Azam FC inaingia kwenye fainali hii ikiwa na nafasi ya kulifanya Kombe la Shirikisho CRDB kuwa taji la pili la michuano hiyo katika historia ya klabu.

Chini ya kocha Florent Ibenge, Azam imekuwa na msimu wenye ushindani, ikimaliza Ligi Kuu Bara nafasi ya tatu. Pia imeonyesha kuwa inaweza kuwakabili Simba, baada ya kutopoteza dhidi yao kwenye mechi za ligi msimu huu.

Azam ilishinda mchezo mmoja wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Simba, kisha ikatoka sare katika mchezo wa pili. Rekodi hiyo inaongeza uzito kwenye fainali ya leo, hasa kwa timu inayotaka kufunga msimu kwa taji.

Rekodi za Simba kwenye fainali za michuano hii

Rekodi za fainali zinaiweka Simba kwenye nafasi yenye historia nzuri. Tangu michuano hii iliporejea msimu wa 2015-2016, Simba imecheza fainali mara tatu na kushinda zote.

Msimu wa 2016-2017, Simba iliifunga Mbao FC mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mchezo huo uliamuliwa kwenye dakika za nyongeza baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 bila kufungana.

Msimu wa 2019-2020, Simba ilitwaa tena taji hilo kwa kuifunga Namungo FC mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Agosti 2, 2020 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga. Mabao ya Simba yalifungwa na Luis Miquissone dakika ya 27 na John Bocco dakika ya 39.

Fainali ya tatu kwa Simba ilikuwa msimu wa 2020-2021, ilipoifunga Yanga bao 1-0 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Bao la Simba lilifungwa na Taddeo Lwanga dakika ya 80.

Rekodi za Azam kwenye fainali

Kwa Azam FC, fainali ya leo ni ya tano tangu msimu wa 2015-2016. Katika fainali nne zilizopita, Azam imeshinda moja na kupoteza tatu.

Taji pekee la Azam kwenye michuano hii lilikuja msimu wa 2018-2019, ilipoifunga Lipuli FC ya Iringa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi. Bao hilo lilifungwa na Obrey Chirwa dakika ya 64.

Fainali tatu ambazo Azam ilipoteza zote zilikuwa dhidi ya Yanga. Msimu wa 2015-2016, ilifungwa mabao 3-1. Msimu wa 2022-2023, ilipoteza kwa bao 1-0. Msimu wa 2023-2024, ilikosa taji kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya sare ya 0-0 kwenye dakika 120 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Simba vs Azam kwenye Kombe la CRDB

Kabla ya fainali ya leo, Simba na Azam FC zimekutana mara nne kwenye michuano ya Kombe la CRDB/FA. Simba imeshinda mara tatu, huku Azam ikishinda mara moja.

Mara ya kwanza zilikutana Aprili 29, 2017 kwenye nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa. Simba ilishinda bao 1-0 kupitia Mohamed Ibrahim ‘MO’ dakika ya 48.

Julai 1, 2020, timu hizo zilikutana tena kwenye robo fainali katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Simba ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na John Bocco dakika ya 39 na Clatous Chota Chama dakika ya 56.

Mkutano wa tatu ulikuwa Juni 26, 2021 kwenye nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa Majimaji, Ruvuma. Simba ilishinda bao 1-0 kupitia Luis Miquissone dakika ya 89.

Azam ilipata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Simba kwenye michuano hii Mei 7, 2023, katika nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. Azam ilishinda mabao 2-1, yakifungwa na Lusajo Mwaikenda dakika ya 22 na Prince Dube dakika ya 75. Bao la Simba lilifungwa na Sadio Kanoute dakika ya 28.

Azam yatangulia Pemba, Simba yawasili kwa ndege

Azam ilikuwa ya kwanza kutua Pemba kwa ajili ya fainali hii, ikitumia usafiri wa boti. Hatua hiyo iliipa nafasi ya kuzoea mazingira ya kisiwani kabla ya mchezo.

Simba iliwasili Pemba siku moja kabla ya fainali kwa ndege ikitokea Dar es Salaam. Kabla ya safari, kikosi hicho kilifanya mazoezi ya mwisho, kisha kikaendelea kujifua Pemba kuanzia saa 12 jioni.

Waamuzi wa fainali

Fainali ya Simba dhidi ya Azam FC itachezeshwa na mwamuzi wa kati Sifu Amoni kutoka Mbeya.

Atasaidiwa na Hamdani Said kutoka Mtwara na Zawadi Yusuph kutoka Dar es Salaam, huku Ahmed Arajiga kutoka Manyara akiwa mwamuzi wa akiba.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Orodha ya Mabingwa Ligi kuu Tanzania Bara
  2. Mfungaji Bora Ligi Kuu ya NBC 2025/2026
  3. Yanga Yatwaa Ubingwa wa Tano Mfululizo NBC Premier League 2025/26
  4. Vinara wa Assist Ligi Kuu ya NBC 2025/2026
  5. Hawa Apa Wafungaji Bora Ligi Kuu ya NBC 2025/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo