Matokeo ya Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB

Matokeo ya Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB

Kikosi cha Mnyama Simba leo kitashuka dimbani katika mtanange wa kumsaka bingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB Federation Cup, maarufu kama Kombe la FA. Simba itachuana vikali dhidi ya Azam FC katika mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, leo Julai 4, 2026 kuanzia saa 11:00 jioni.

Ni fainali inayobeba heshima ya msimu kwa pande zote mbili. Simba na Azam zinaingia uwanjani zikitafuta taji lililosalia kwenye msimu ambao Yanga tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ikiwaacha wapinzani hao nafasi ya pili na tatu mtawalia.

Matokeo ya Simba vs Azam leo yatasubiriwa kwa shauku kubwa haswa na mashabiki wa mnyama, wakati Simba ikisaka kuendeleza rekodi yake bora katika fainali za michuano hii na Azam ikilenga kutwaa taji la pili la Kombe la Shirikisho katika historia yake.

Matokeo ya Simba vs Azam Leo 04/07/2026

Matokeo ya Simba vs Azam Leo 04/07/2026

Simba Sc1-0Azam Fc

Simba yaanza na Mpanzu, Chama na Oura

Simba imetangaza kikosi chake cha kwanza kwa ajili ya fainali dhidi ya Azam FC, huku Kassali akipewa jukumu la kulinda lango la Wekundu wa Msimbazi.

Duchu, Kibabage, Toure na De Reuck wamepewa nafasi ya kuanza, wakati Kagoma, Guede na Neo nao wakiwa kwenye kikosi cha kwanza.

Elie Mpanzu, Clatous Chama na Anicet Oura wanakamilisha kikosi cha wachezaji 11 waliochaguliwa kuanza pambano hili la fainali.

Kikosi cha Simba dhidi ya Azam FC: Kassali, Duchu, Kibabage, Toure, De Reuck, Kagoma, Guede, Neo, Mpanzu, Chama na Oura.

Kwenye benchi, Simba ina Abel, Alexander, Kapombe, Mligo, Vedastus, Semfuko, Morice, Kante, Mwalimu na Inno.

Kwa upande wa Azam FC, Manula ameanza langoni, huku Lusajo akiwa nahodha wa kikosi hicho. Wengine waliopangwa kuanza ni Msindo, Lawi, Fuentes, Himid, Sopu, Bin Zayd, Kitambala, Fei Toto na Nado.

Kikosi cha Azam FC: Manula, Lusajo, Msindo, Lawi, Fuentes, Himid, Sopu, Bin Zayd, Kitambala, Fei Toto na Nado.

Kwenye benchi la Azam FC wapo Foba, Twalib, Zouzou, Kibeku, Kanoute, Akaminko, Abah, Alobogast, Zidane na J J Ngita.

Simba na Azam zasaka heshima Pemba

Fainali hii imebeba uzito mkubwa kwa timu zote mbili baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Simba ilimaliza nafasi ya pili, huku Azam ikishika nafasi ya tatu. Taji la Kombe la Shirikisho CRDB sasa limebaki kuwa nafasi kwa mmoja wao kufunga msimu akiwa bingwa.

Kwa Simba, ushindi utasaidia kupunguza presha ya mashabiki baada ya Yanga kuendelea kutawala Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tano mfululizo.

Azam nayo inatafuta nafasi ya kuongeza taji jingine la Kombe la Shirikisho baada ya kutwaa michuano hiyo mara moja katika fainali zake nne zilizopita.

Simba ilivyoingia fainali

Simba imefika fainali baada ya kuifunga Coastal Union mabao 4-0 kwenye nusu fainali iliyopigwa Juni 20, 2026 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Wekundu wa Msimbazi walianza safari yao hatua ya 64 bora kwa kuifunga Greenland FC ya Kagera mabao 3-0.

Katika hatua ya 32 bora, Simba iliifunga B19 FC mabao 2-0, kisha ikaiondosha Dodoma Jiji kwa mabao 3-1 kwenye hatua ya 16 bora.

Robo fainali, Simba iliichapa TRA United mabao 4-0 kabla ya kuirudia idadi hiyo ya mabao dhidi ya Coastal Union kwenye nusu fainali.

Azam ilivyoingia fainali

Azam FC imefika kwenye mchezo wa leo baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Yanga katika nusu fainali iliyopigwa Juni 21, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Matajiri hao wa Chamazi walianza hatua ya 64 bora kwa kuifunga Endument FC ya Kilimanjaro bao 1-0 na baadaye wakaiondosha Mbeya Kwanza kwa matokeo kama hayo.

Azam iliifunga Fountain Gate mabao 4-0 kwenye hatua ya 16 bora kabla ya kuichapa Mashujaa bao 1-0 katika robo fainali.

Ushindi dhidi ya Yanga uliipeleka Azam fainali na kumaliza rekodi ya mabingwa hao ya kucheza mechi 28 za Kombe la CRDB bila kupoteza.

Rekodi ya Simba kwenye fainali

Simba inaingia kwenye pambano la leo ikiwa na rekodi nzuri tangu michuano ya FA iliporejea msimu wa 2015-2016.

Wekundu wa Msimbazi wamecheza fainali tatu katika kipindi hicho na kushinda zote.

Simba iliifunga Mbao FC mabao 2-1 msimu wa 2016-2017, ikaichapa Namungo FC kwa matokeo kama hayo msimu wa 2019-2020 na baadaye kuifunga Yanga bao 1-0 kwenye fainali ya msimu wa 2020-2021.

Fainali dhidi ya Azam ni ya nne kwa Simba tangu michuano hiyo iliporejea.

Azam yasaka taji la pili

Kwa Azam FC, pambano la leo ni fainali ya tano tangu msimu wa 2015-2016.

Azam imetwaa taji mara moja katika fainali nne zilizopita. Ubingwa wake ulipatikana msimu wa 2018-2019 baada ya kuifunga Lipuli FC bao 1-0.

Katika fainali nyingine tatu, Azam ilipoteza dhidi ya Yanga.

Ilifungwa mabao 3-1 msimu wa 2015-2016, ikapoteza kwa bao 1-0 msimu wa 2022-2023 na baadaye kushindwa kwa mikwaju ya penalti 6-5 kwenye fainali ya msimu wa 2023-2024 baada ya dakika 120 kumalizika bila bao.

Rekodi za Simba vs Azam Kombe la FA

Simba na Azam zimekutana mara nne kwenye michuano ya Kombe la CRDB/FA kabla ya fainali ya leo.

Simba imeshinda mara tatu, wakati Azam ina ushindi mmoja.

Mwaka 2017, Simba iliifunga Azam bao 1-0 kwenye nusu fainali. Mwaka 2020, Wekundu wa Msimbazi walishinda tena mabao 2-0 katika robo fainali.

Simba iliendeleza rekodi hiyo mwaka 2021 kwa ushindi wa bao 1-0 kwenye nusu fainali.

Azam ilivunja mwendo huo mwaka 2023 ilipoifunga Simba mabao 2-1 kwenye nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Waamuzi wa Simba vs Azam leo

Sifu Amoni kutoka Mbeya ndiye mwamuzi wa kati wa fainali ya Simba dhidi ya Azam FC.

Atasaidiwa na Hamdani Said kutoka Mtwara na Zawadi Yusuph kutoka Dar es Salaam.

Ahmed Arajiga kutoka Manyara amepewa jukumu la kuwa mwamuzi wa akiba.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Kikosi cha Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Fainali Kombe la Shirikisho CRDB
  2. Rekodi Zinavyoibeba Simba Dhidi ya Azam FC Fainali ya Kombe la CRDB
  3. Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Saa Ngapi? Muda wa Fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB
  4. Orodha ya Mabingwa Ligi kuu Tanzania Bara
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo