Tarehe ya Kuripoti Shule Kidato Cha Tano 2026
Tarehe ya kuripoti shule Kidato cha Tano 2026 imetangazwa, ambapo wanafunzi waliopangwa kujiunga na kidato cha tano wanapaswa kuanza kuripoti shuleni kuanzia Julai 4, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Profesa Riziki Shemdoe, siku ya mwisho ya kuripoti ni Julai 31, 2026, huku muhula wa kwanza ukitarajiwa kuanza Julai 6, 2026.
Wanafunzi Waliochaguliwa Kidato cha Tano na Vyuo 2026
Jumla ya wanafunzi 246,197 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi mwaka 2026.
Kati yao, wasichana ni 114,102 na wavulana ni 132,095. Wanafunzi 631 kati ya waliochaguliwa ni wenye mahitaji maalumu.
Idadi hiyo imeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana, ambapo wanafunzi 214,141 walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi.
Mchanganuo wa Wanafunzi wa Kidato cha Tano
Profesa Shemdoe amesema wanafunzi 172,114, sawa na asilimia 69.9, wamechaguliwa kujiunga katika shule za kutwa na bweni.
“Watakaojiunga shule za bweni na kutwa kidato cha tano ni wasichana 85,987 na wavulana 86,127 wenye sifa wamepangiwa katika shule 856 zikiwemo bweni 825, kutwa 25 na kutwa na bweni sita,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi 163,499 wamepangwa katika shule za bweni. Kati yao, wasichana ni 81,746 na wavulana ni 81,753.
Wanafunzi wengine 7,067 wamepangwa katika shule za kutwa, wakiwemo wasichana 3,479 na wavulana 3,588.
Aidha, wanafunzi 1,548, wakiwemo wasichana 762 na wavulana 786, wamepangwa katika shule nane zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu.

Tarehe Muhimu za Kuripoti Kidato cha Tano 2026
| Tukio | Tarehe |
|---|---|
| Kuanza kuripoti shuleni | Julai 4, 2026 |
| Kuanza kwa muhula wa kwanza | Julai 6, 2026 |
| Mwisho wa kuripoti shuleni | Julai 31, 2026 |
Wanafunzi na wazazi wanashauriwa kuzingatia tarehe hizi ili maandalizi ya safari, mahitaji ya shule na taratibu nyingine muhimu yafanyike mapema.
Waliochaguliwa Vyuo vya Elimu ya Ufundi
Kwa upande wa vyuo vya elimu ya ufundi, wanafunzi 74,083, sawa na asilimia 30.1, wamechaguliwa kujiunga na vyuo hivyo. Kati yao, wasichana ni 28,115 na wavulana 45,968.
Profesa Shemdoe amesema wanafunzi 3,144 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vinne vya elimu ya ufundi.
Vyuo hivyo ni:
- Chuo cha Ufundi Arusha, ATC
- Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, DIT
- Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, MUST
- Chuo cha Maendeleo ya Maji, WMDI
Pia, wanafunzi 2,330 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya afya ngazi ya stashahada, huku wanafunzi 2,983 wakichaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu ngazi ya stashahada.
Katika kada nyingine, wanafunzi 65,626 wamechaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali.
Maelekezo kwa Wanafunzi Waliopangwa Vyuo vya Ufundi
Tofauti na wanafunzi wa kidato cha tano, waliopangwa katika vyuo vya elimu ya ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika vyuo walivyopangwa.
“Kwa wanafunzi waliopangwa kwenye vyuo vya elimu ya ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika vyuo walivyopangwa,” amesema Profesa Shemdoe.
Hivyo, wanafunzi waliopangwa katika vyuo wanapaswa kufuatilia maelekezo rasmi kutoka kwenye vyuo husika.
Hakutakuwa na Mabadiliko ya Shule
TAMISEMI imesema uchaguzi wa wanafunzi kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika shule.
Kutokana na hilo, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko ya shule kwa sababu ya ukosefu wa nafasi.
“Kwa wale wazazi mnaotamani watoto wenu wasome katika zile shule nane bora, hakutakuwa na nafasi ya uhamisho kwa sababu kumejaa,” amesema Profesa Shemdoe.
Kauli hiyo ina maana kuwa wanafunzi wanapaswa kujiandaa kuripoti katika shule walizopangiwa.
Wito kwa Wanafunzi, Wazazi na Viongozi
Profesa Shemdoe amewapongeza walimu, wazazi na walezi kwa juhudi zao katika malezi na ufundishaji zilizowezesha wanafunzi kufaulu vizuri.
Pia amewapongeza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi, akiwahimiza kuendelea kufanya bidii katika masomo ili waweze kufanikiwa kujiunga na elimu ya juu baada ya kuhitimu hatua hiyo.
Ametoa pia wito kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha azma ya kuwa na shule za sekondari za kidato cha tano katika kila tarafa inatekelezwa.
“Kutekelezwa kwa azma hii itawezesha wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kidato cha nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita,” amesema.
Mapendekezo ya Mhariri:




```






Leave a Reply