Dirisha la Maombi ya Vyuo 2026/2027 Lafunguliwa, TCU Yataja Tarehe ya Mwisho

Dirisha la Maombi ya Vyuo 2026/2027 Lafunguliwa, TCU Yataja Tarehe ya Mwisho Kutuma Maombi Vyuo Vikuu

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua rasmi Dirisha la Maombi ya Vyuo 2026/2027 kwa waombaji wa udahili wa shahada ya kwanza katika taasisi za elimu ya juu nchini.

Dirisha hilo limefunguliwa kuanzia Julai 10 hadi Agosti 10, 2026. Waombaji wanatakiwa kutumia muda huo kusoma miongozo ya udahili, kujiridhisha kuhusu sifa za programu wanazotaka na kutuma maombi kupitia mifumo ya vyuo walivyovichagua.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amesema dirisha hilo limefunguliwa siku chache baada ya kutolewa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2026. Asilimia 99.92 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Dirisha la Maombi ya Vyuo 2026/2027 Lafunguliwa, TCU Yataja Tarehe ya Mwisho

Dirisha la Maombi ya Vyuo 2026/2027 linawahusu Kinanani?

Kwa mujibu wa Profesa Kihampa, maombi ya udahili kwa mwaka wa masomo 2026/27 yanahusu makundi matatu ya waombaji:

  • Wenye sifa za kuhitimu kidato cha sita
  • Wenye sifa za stashahada au sifa zinazolingana nazo
  • Wenye Cheti cha Awali (Foundation Certificate) cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)

Kabla ya kutuma maombi, waombaji wanapaswa kuhakikisha kuwa wamekidhi vigezo vya kujiunga na programu wanazotaka kusoma.

Maelezo kuhusu vigezo hivyo yanapatikana katika kitabu cha mwongozo wa udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/27 kilichowekwa kwenye tovuti ya TCU, pamoja na tovuti za vyuo husika.

“Tunawasihi waombaji kusoma kwa makini mwongozo wa udahili pamoja na maelekezo maalumu yanayotolewa na kila chuo kabla ya kuanza kutuma maombi,” amesema Profesa Kihampa.

Maombi yanatumwa kupitia vyuo husika

TCU imeeleza kuwa waombaji hawatakiwi kuwasilisha maombi yao kupitia Tume. Badala yake, wanapaswa kutuma maombi moja kwa moja kupitia mifumo ya kielektroniki ya vyuo walivyovichagua.

Kila chuo kina maelekezo yake kuhusu namna ya kutuma maombi. Waombaji wametakiwa kufuatilia taarifa hizo kupitia tovuti za vyuo husika na kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa.

Kwa maswali yanayohusu programu za masomo, waombaji wanapaswa kuwasiliana moja kwa moja na chuo husika. Masuala ya jumla kuhusu udahili yanaweza kuelekezwa TCU.

Waombaji wenye vyeti vya nje ya nchi

Waombaji wa Kitanzania wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani ya nje ya nchi wanapaswa kwanza kuthibitisha ulinganifu wa vyeti vyao kabla ya kuomba udahili.

Vyeti vya elimu ya sekondari vinapaswa kuthibitishwa kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), huku vyeti vya stashahada vikithibitishwa kupitia Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet).

Uthibitisho huo unatakiwa kufanyika kabla ya mwombaji kuwasilisha maombi yake ya udahili.

Waombaji wasiokuwa Watanzania wenye vyeti vya nje ya nchi wanatakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja kupitia mifumo ya vyuo husika.

TCU yatoa tahadhari kuhusu utapeli

TCU imewataka waombaji kuendelea kupata taarifa kupitia tovuti yake rasmi, tovuti za vyuo vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza na taarifa zinazotolewa na Tume kupitia vyombo vya habari.

Profesa Kihampa pia amewataka wananchi kuwa makini na watu wanaojitambulisha kuwa mawakala au washauri wa kujiunga na vyuo vikuu.

Waombaji wanapaswa kutumia njia rasmi zilizowekwa na kufuata maelekezo ya vyuo husika ili kuepuka utapeli na usumbufu wakati wa kutuma maombi.

Tarehe ya mwisho ya Dirisha la Maombi ya Vyuo 2026/2027 ni Agosti 10, 2026.

Mapendekezezo ya Mhariri:

  1. Matokeo ya Kidato cha Sita 2026 NECTA Form Six Results
  2. Matokeo ya Kidato cha Sita 2026: Haya Hapa ACSEE Results
  3. Majina ya Wanafunzi na Shule Walizopangiwa Kidato cha Tano 2026
  4. Majina ya Waliochaguliwa Kidato cha Tano na Vyuo 2026 Yatangazwa na TAMISEMI
  5. Tarehe ya Kuripoti Shule Kidato Cha Tano 2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo