NECTA Yatangaza Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita 2026, Ufaulu Wafikia 99.92%
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza rasmi Matokeo ya Kidato cha Sita 2026, huku watahiniwa wa shule wakirekodi kiwango cha ufaulu cha asilimia 99.92.
Matokeo ya Kidato cha Sita 2026/2027 yametangazwa Jumatatu, Julai 6, 2026, na Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Baraza hilo, watahiniwa 133,647 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita (ACSEE) 2026. Kati yao, 126,556 walikuwa watahiniwa wa shule na 7,091 walikuwa watahiniwa wa kujitegemea.
Kutangazwa kwa matokeo hayo kunafungua hatua nyingine kwa wahitimu wa A-Level wanaojiandaa kuendelea na elimu ya juu na kufanya maamuzi kuhusu programu za masomo watakazofuata.

Watahiniwa 125,056 wa shule wafaulu ACSEE 2026
NECTA imesema watahiniwa 125,320 wa shule walifanya mtihani, sawa na asilimia 99.02 ya waliojisajili.
Kati ya watahiniwa wenye matokeo, 125,056 walifaulu, sawa na asilimia 99.92. Watahiniwa 97 pekee, sawa na asilimia 0.08, hawakufaulu.
Kwa upande wa jinsia, watahiniwa wanawake 61,733 walifaulu kwa asilimia 99.94, huku wanaume 63,323 wakifaulu kwa asilimia 99.91.
Takwimu hizo zinaonyesha kiwango cha ufaulu kimeendelea kubaki juu miongoni mwa watahiniwa wa shule.
Zaidi ya nusu ya watahiniwa wapata Division I
Matokeo ya ACSEE 2026 pia yanaonyesha ongezeko la watahiniwa waliopata Daraja la Kwanza.
Jumla ya watahiniwa 67,696, sawa na asilimia 54.09, walipata Division I. Watahiniwa wengine 43,515, sawa na asilimia 34.77, walipata Division II.
Kwa ujumla, watahiniwa 124,603, sawa na asilimia 99.56, walipata madaraja ya kwanza hadi ya tatu.
Mwaka 2025, asilimia 48.57 ya watahiniwa walipata Division I. Kiwango hicho kimeongezeka hadi asilimia 54.09 mwaka 2026.
Ufaulu wa watahiniwa wa kujitegemea waongezeka
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, watu 6,476 walifanya ACSEE 2026, sawa na asilimia 91.33 ya waliojisajili.
Kati yao, watahiniwa 6,112 walifaulu, sawa na asilimia 94.5.
Kiwango cha ufaulu kwa watahiniwa wa kujitegemea kimeongezeka kwa pointi za asilimia 3.8 ikilinganishwa na mwaka 2025.
Wanafunzi sasa kujiandaa na elimu ya juu
Kwa wahitimu wengi, kupokea matokeo ya Kidato cha Sita ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu katika safari yao ya elimu.
ACSEE hutolewa kwa watahiniwa waliokamilisha elimu ya sekondari ya juu, maarufu kama A-Level. Matokeo yake ni miongoni mwa taarifa muhimu za kitaaluma zinazotumika katika michakato ya kuendelea na elimu ya juu.
Baada ya matokeo kutangazwa, wanafunzi wanaweza kuanza kufuatilia taarifa za udahili, kuangalia programu za masomo wanazokidhi sifa na kuandaa nyaraka zinazoweza kuhitajika wakati wa kutuma maombi.
Wahitimu wanashauriwa kuangalia kwa makini matokeo na sifa zao kabla ya kufanya maamuzi kuhusu kozi au taasisi wanazotaka kuomba.
Jinsi ya kuangalia Matokeo ya Kidato cha Sita 2026
Watahiniwa wanaweza kufuatilia matokeo ya ACSEE 2026 kupitia mfumo rasmi wa matokeo wa NECTA.
Mwanafunzi anatakiwa kufungua tovuti ya NECTA necta.go.tz, kwenda kwenye sehemu ya Results, kuchagua ACSEE na kufungua matokeo ya mwaka 2026.
Baada ya kufungua orodha ya matokeo, mtahiniwa anaweza kutafuta shule au kituo chake cha mtihani na kuhakiki namba yake ya mtihani.
Vilevile Ili Kukurahisishia kupata matokeo, hapa chini tumekuletea viungo vitakavyokupeleka moja kwa moja katika ukurasa wa shule yako na kuangalia matokeo yako kwa haraka. Tafuta jina la shule yako kwenye jedwahi hapa chini na kisha bofya jina kuona matokeo
NECTA pia inaelekeza watumiaji wanaotaka kupata matokeo kwa simu kupiga *152*00#, kuchagua namba 8 kwa ELIMU, kisha namba 2 kwa NECTA na kufuata maelekezo yanayotolewa.
Watahiniwa wanashauriwa kutumia mifumo rasmi ya NECTA wanapotafuta matokeo ili kuepuka taarifa zisizo sahihi au viungo visivyoaminika vinavyoweza kusambazwa mitandaoni.




```





Leave a Reply