Hiki Hapa Kikosi cha Azam Dhidi ya Simba Leo 04/07/2026
Kikosi cha Azam dhidi ya Simba leo kimeshatangazwa tayari kuelekea mtanange wa fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB Federation Cup, maarufu kama Kombe la FA. Matajiri hao wa Chamazi watamenyana na Wekundu wa Msimbazi kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, leo Julai 4, 2026 kuanzia saa 11:00 jioni.
Azam inaingia kwenye mchezo huu ikisaka kutwaa taji la pili la michuano hiyo katika historia yake, huku ikikutana na Simba ambayo haijapoteza fainali yoyote ya Kombe la Shirikisho tangu michuano hiyo iliporejea msimu wa 2015-2016.
Kikosi cha Azam dhidi ya Simba leo
Azam FC imeanza na Aishi Manula katika kikosi chake cha kwanza, huku Lusajo akipewa jukumu la unahodha katika pambano hilo la fainali.
Msindo, Lawi, Fuentes na Himid pia wamepewa nafasi ya kuanza, wakati Sopu, Bin Zayd, Kitambala, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Nado wakikamilisha orodha ya wachezaji 11 wa Azam.
Kikosi cha Azam FC dhidi ya Simba: Manula, Lusajo, Msindo, Lawi, Fuentes, Himid, Sopu, Bin Zayd, Kitambala, Fei Toto na Nado.
Kwenye benchi la Azam wapo Foba, Twalib, Zouzou, Kibeku, Kanoute, Akaminko, Abah, Alobogast, Zidane na J.J Ngita.
Fei Toto aanza dhidi ya Simba
Feisal Salum ‘Fei Toto’ amepewa nafasi ya kuanza katika kikosi cha Azam baada ya kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu waliopumzishwa kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji.
Azam ilishinda mchezo huo mabao 2-0, huku benchi la ufundi likiwa limewapumzisha baadhi ya wachezaji wake muhimu kuelekea fainali ya leo.
Sopu na Bin Zayd nao wamejumuishwa kwenye kikosi cha kwanza, huku Azam ikisaka kuendeleza rekodi yake nzuri dhidi ya Simba katika mechi za ligi za msimu wa 2025-2026.
Azam yaingia fainali baada ya kuitoa Yanga
Azam imefika fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB baada ya kuifunga Yanga mabao 3-2 katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Juni 21, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Ushindi huo uliwavua Yanga ubingwa wa michuano hiyo na kumaliza rekodi yao ya mechi 28 za Kombe la CRDB bila kupoteza.
Matajiri hao wa Chamazi walianza kampeni zao hatua ya 64 bora kwa kuifunga Endument FC ya Kilimanjaro bao 1-0, kabla ya kuiondosha Mbeya Kwanza kwa matokeo kama hayo katika hatua ya 32 bora.
Azam iliifunga Fountain Gate mabao 4-0 kwenye hatua ya 16 bora, kisha ikaiondosha Mashujaa kwa bao 1-0 katika robo fainali kabla ya kuifunga Yanga kwenye nusu fainali.
Azam yasaka taji la pili la Kombe la Shirikisho
Fainali ya leo ni ya tano kwa Azam FC tangu msimu wa 2015-2016. Katika fainali nne zilizopita, timu hiyo imetwaa taji mara moja.
Azam ilibeba Kombe la Shirikisho msimu wa 2018-2019 baada ya kuifunga Lipuli FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi. Bao la ushindi lilifungwa na Obrey Chirwa dakika ya 64.
Katika fainali nyingine tatu, Azam ilipoteza dhidi ya Yanga. Ilifungwa mabao 3-1 msimu wa 2015-2016, ikapoteza kwa bao 1-0 msimu wa 2022-2023 na baadaye kushindwa kwa mikwaju ya penalti 6-5 msimu wa 2023-2024 baada ya dakika 120 kumalizika bila bao.
Sasa kikosi cha Florent Ibenge kina nafasi nyingine ya kupigania taji hilo, safari hii kikikutana na Simba katika fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho inayozikutanisha timu hizo mbili.
Azam na Simba zataka kufunga msimu kwa taji
Azam na Simba zinaingia kwenye fainali hii baada ya Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Simba ilimaliza nafasi ya pili, huku Azam ikishika nafasi ya tatu.
Kwa Azam, ushindi dhidi ya Simba utaifanya timu hiyo kutwaa Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili na kuhitimisha msimu wa 2025-2026 kwa taji.
Simba nayo inaingia kwenye pambano hilo ikiwa na rekodi ya kutwaa taji katika fainali zote tatu ilizocheza tangu michuano hiyo iliporejea msimu wa 2015-2016.
Filimbi ya mwisho kwenye Uwanja wa Gombani ndiyo itakayoamua kama Azam itaongeza taji la pili la Kombe la Shirikisho kwenye historia yake au Simba itaendeleza rekodi yake bora katika fainali za michuano hiyo.
Mapendekezo ya Mhariri:




```





Leave a Reply