Yanga na Simba Kunufaika Baada ya Vigogo Wanne Kukosa Klabu Bingwa Afrika
Yanga na Simba zimepata nafuu kuelekea ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya klabu nne zilizokuwa juu yao kwenye chati ya ubora wa klabu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kushindwa kujihakikishia nafasi ya kushiriki mashindano hayo.
Ingawa timu hizo mbili zimeshuka katika chati ya ubora wa klabu za CAF, hali hiyo imefungua nafasi ya kuwa miongoni mwa timu nane za juu zinazoweza kuwekwa katika vyungu viwili vya mwanzo wakati wa upangaji wa droo ya hatua ya makundi, iwapo zitafanikiwa kufuzu hatua hiyo.

Vigogo wanne waliokosa nafasi
Kwa mujibu wa chati ya ubora wa klabu ya CAF, timu zilizokuwa juu ya Simba na Yanga lakini hazitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ni Al Ahly, USM Alger, AS FAR na CR Belouizdad.
Kama klabu hizo zingefuzu mashindano hayo na kufika hatua ya makundi, Yanga na Simba zingekuwa na uwezekano wa kupangwa katika chungu cha tatu. Kutokuwepo kwao kunazisogeza wawakilishi hao wa Tanzania katika nafasi nane za juu kwa ajili ya upangaji wa droo ya hatua ya makundi.
Nafasi za Yanga na Simba kwenye viwango vya CAF
Kwa sasa Simba inashika nafasi ya 11 katika chati ya ubora wa klabu ya CAF ikiwa na pointi 38, huku Yanga ikiwa nafasi ya 12 na pointi 25.
Kutokuwepo kwa Al Ahly, USM Alger, AS FAR na CR Belouizdad katika mashindano hayo kunatoa nafasi kwa Simba na Yanga kuwa miongoni mwa timu zitakazowekwa katika vyungu viwili vya mwanzo iwapo zitafuzu hatua ya makundi.
Endapo hali hiyo itatokea, itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Yanga na Simba kuwekwa katika chungu cha pili kwenye upangaji wa droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Faida ya kupangwa kwenye vyungu vya juu
Kupangwa katika chungu cha kwanza au cha pili kuna faida kwa timu zinazofuzu hatua ya makundi.
Miongoni mwa faida hizo ni kuanza na kumalizia mechi za hatua ya makundi katika uwanja wa nyumbani. Pia, timu zinazokuwa katika vyungu hivyo huepuka kukutana na baadhi ya wapinzani wenye uzoefu zaidi katika hatua hiyo.
Chati ya ubora wa CAF
Kwa mujibu wa viwango vya sasa vya CAF, Mamelodi Sundowns ndiyo kinara ikiwa na pointi 73, ikifuatiwa na Al Ahly yenye pointi 66.
Esperance inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 58, RS Berkane ipo nafasi ya nne na pointi 57, huku USM Alger ikiwa ya tano na pointi 52.
Zamalek inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 49, Pyramids FC ipo nafasi ya saba na pointi 48, AS FAR inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 41, Al Hilal ipo nafasi ya tisa na pointi 39, wakati CR Belouizdad ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 38.
Simba inafuatia katika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 38, huku Yanga ikishika nafasi ya 12 na pointi 25.
Mapendekezo ya Mhariri:




```






Leave a Reply