Ratiba ya Ligi Kuu NBC Leo Juni 30, 2026: Yanga, Simba Kuamua Ubingwa Raundi ya Mwisho
Ratiba ya Ligi Kuu NBC leo Juni 30, 2026 inafunga pazia la msimu wa 2025-2026 kwa mechi zote nane kupigwa kwa wakati mmoja, huku macho ya mashabiki yakiwa kwenye mbio za ubingwa, vita ya kusalia ligi na mchuano wa mfungaji bora.
Raundi hii ya mwisho ina uzito mkubwa kwa sababu Yanga inaingia ikiwa kileleni kwa pointi 72 baada ya mechi 29, huku Simba ikifuatia kwa pointi 70. Ndani ya dakika 90 za mwisho, Yanga inaweza kutetea ubingwa, lakini Simba bado ina nafasi ya kusubiri makosa ya watani wake.
Ratiba ya Ligi Kuu NBC leo
| Mechi | Uwanja/Mji |
| JKT Tanzania vs Yanga | Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam |
| Simba vs KMC | Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam |
| Namungo vs Mtibwa Sugar | — |
| Mashujaa vs Tanzania Prisons | Kigoma |
| Mbeya City vs TRA United | — |
| Fountain Gate vs Singida Black Stars | — |
| Coastal Union vs Pamba Jiji | Uwanja wa Mkwakwani, Tanga |
| Azam FC vs Dodoma Jiji | Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam |

Mechi zote zinapigwa mda moja, hali inayozuia timu kusubiri matokeo ya wapinzani kabla ya kuingia uwanjani. Kila bao na kila pointi vinaweza kubadili hatima ya timu kwenye msimamo wa mwisho.
Yanga au Simba: hesabu za ubingwa
Yanga itacheza dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ikiwa na nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa wa tano mfululizo. Ikiwa itashinda, hakuna kitakachoizuia kumaliza msimu ikiwa bingwa.
Sare pia inaweza kuwa na manufaa kwa Yanga kutokana na tofauti ya pointi mbili iliyonayo dhidi ya Simba, lakini matokeo ya KMC Complex yatakuwa muhimu katika hesabu za mwisho.
Simba, kwa upande wake, haina nafasi ya kufanya makosa. Wekundu wa Msimbazi wanahitaji kushinda dhidi ya KMC, kisha kusubiri Yanga ishindwe kupata matokeo yanayotosha katika mchezo wake dhidi ya JKT Tanzania.
Beki wa Simba, Shomari Kapombe, amesema lengo lao ni kumaliza msimu kwa ushindi na kuwapa furaha mashabiki.
“Lengo letu ni kupata pointi tatu katika mchezo wa mwisho na kuwafurahisha mashabiki wetu ambao wamekuwa nasi tangu mwanzo wa msimu. Tunawaomba wajitokeze kwa wingi kwa sababu wao ni mchezaji wetu wa 12,” amesema Kapombe.
Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema mchezo dhidi ya KMC hautakuwa mwepesi licha ya wapinzani wao kuwa tayari wameshuka daraja.
“Kushuka daraja ni kwa timu, si kwa wachezaji. Kila mmoja atapambana kuonyesha uwezo wake, hivyo tunatarajia mchezo mgumu lakini sisi tunahitaji pointi tatu,” amesema Matola.
JKT yaweka msimamo, Yanga yasema iko tayari
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema maandalizi ya timu yake yanaendelea vizuri licha ya safari ndefu kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam. Amesema wachezaji wako katika hali nzuri kiafya isipokuwa Edson Katanga, atakayekosekana kwa adhabu ya kadi.
“Mchezo utakuwa mgumu kwa sababu kila timu ina malengo yake. Sisi tupo hapa kwa ajili ya kutimiza malengo ya JKT, si kuangalia timu nyingine zinafanya nini. Tutacheza kwa nidhamu ya kimkakati na kuhakikisha tunafanya kila tuwezalo kupata matokeo mazuri,” amesema Ally.
Kwa upande wa Yanga, Kaimu Kocha Mkuu Abdihamid Moallin amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo muhimu.
“JKT ni timu nzuri yenye kocha bora na iliyopangwa vizuri. Tunafahamu uwezo wao, hivyo tunapaswa kucheza kwa kiwango cha juu na kuwa makini hasa upande wa ulinzi. Lengo letu ni kushinda mchezo na kusherehekea ubingwa baada ya hapo,” amesema Moallin.
Mshambuliaji Emmanuel Mwanengo amesema mchezo huo ndio unaoamua hatima ya ubingwa wa Yanga.
“Hata ushindi wa bao moja unatosha kutupa ubingwa. Tunaamini mbele ya mashabiki wetu tutafanya vizuri na kumaliza kazi,” amesema.
Vita ya kusalia Ligi Kuu Bara
Wakati Yanga na Simba zikipambana juu ya msimamo, chini kuna presha ya kuepuka kushuka daraja na nafasi za mchujo.
KMC tayari imeshuka daraja, lakini nafasi nyingine ya kushuka moja kwa moja bado iko wazi. Mtibwa Sugar ipo kwenye wakati mgumu zaidi ikiwa na pointi 27 na italazimika kushinda dhidi ya Namungo ili kuendelea kuwa na matumaini.
Tanzania Prisons yenye pointi 29 itakuwa na mchezo mgumu dhidi ya Mashujaa Kigoma. Matokeo mabaya yanaweza kuiweka kwenye hatari ya kushuka moja kwa moja au kuingia kwenye mchujo.
Mbeya City, nayo ikiwa na pointi 29, inahitaji kufanya vizuri dhidi ya TRA United ili kujiondoa kwenye hesabu mbaya za mwisho.
Tofauti ya pointi kati ya timu hizi ni ndogo, hivyo mabadiliko ya bao moja katika uwanja mmoja yanaweza kubadili msimamo kwa dakika chache.
Namungo na Fountain Gate bado hazijatulia
Namungo ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 31, lakini bado haijamaliza kazi. Ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar utaiondoa kwenye presha, huku sare ikiwa nafuu kwao.
Fountain Gate, yenye pointi 30 katika nafasi ya 12, pia inahitaji matokeo mazuri dhidi ya Singida Black Stars ili kuepuka kumaliza kwenye nafasi ya 13 au 14, ambazo zina maana ya kucheza mechi za mchujo.
Hizi si mechi za kukamilisha ratiba tu. Kwa timu zilizo karibu na eneo la chini, dakika 90 za mwisho zinaweza kuamua kubaki salama au kuingia kwenye safari ya kujinusuru.
Fei Toto, Okello na Mossi kwenye mbio za mfungaji bora
Mbali na mbio za ubingwa na kushuka daraja, vita ya mfungaji bora pia inaingia raundi ya mwisho ikiwa wazi.
Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, anaongoza kwa mabao 15. Nyuma yake wapo Allan Okello wa Yanga na Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars, kila mmoja akiwa na mabao 14.
Fei Toto atakuwa na nafasi ya kuongeza idadi ya mabao yake wakati Azam ikiikaribisha Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Okello atakuwa na kazi mbili; kuisaidia Yanga kumaliza kazi ya ubingwa na wakati huohuo kuwania tuzo ya mfungaji bora. Mossi, kwa upande wake, atakuwa na nafasi ya kuongeza idadi yake ya mabao Singida Black Stars itakapocheza dhidi ya Fountain Gate.
Mechi zisizo na presha ya kushuka
Coastal Union itaikaribisha Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, katika mchezo ambao hauna presha ya kushuka daraja kwa pande zote mbili.
Coastal Union ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 33, huku Pamba Jiji ikiwa nafasi ya saba na pointi 36. Coastal inahitaji ushindi ili kujaribu kupanda nafasi ya juu, wakati Pamba Jiji nayo inalenga kumaliza msimu kwenye nafasi nzuri zaidi.
Azam FC, iliyojihakikishia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 61, itaikaribisha Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya nane na pointi 35. Dodoma Jiji ipo salama dhidi ya kushuka daraja, lakini kupoteza kunaweza kuishusha nafasi endapo Coastal Union na Mashujaa zitashinda.
Wadau wa soka wazungumzia msimu
Nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, amesema msimu huu umekuwa na ushindani mkubwa na amepongeza Bodi ya Ligi Tanzania pamoja na TFF kwa kuifanya ligi kuwa na mvuto.
“Nawapongeza Bodi ya Ligi Tanzania na TFF zimefanya ligi iwe bora na yenye mvuto, ndiyo maana kila mtu anasubiri nani atakuwa bingwa pia timu zimezidiana pointi chache hata zile zilizopo chini kwenye msimamo wa ligi,” amesema Mgosi.
Beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua, amesema ligi imebakia na mvuto hadi mechi ya mwisho.
“Ligi imebakia na mvuto mkubwa hadi mechi ya mwisho ndipo itajulikana kati ya Yanga na Simba nani bingwa, pia itajulikana timu gani zinashuka au kucheza mtoano ukiondoa KMC ambayo ilishashuka,” amesema.
Staa wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma, amesema Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekuwa na mwendelezo mzuri wa kiwango.
“Kwa upande wangu mchezaji ninayemuona amekuwa na muendelezo wa kiwango ni kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ndiye kinara wa mabao 15, asisti nane, ila kwa ujumla ligi ni nzuri na bora,” amesema.
NBC kuandaa sherehe mbili za ubingwa
Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu, Benki ya NBC, wametangaza kuandaa sherehe mbili za ubingwa zenye viwango sawa ili bingwa atakayepatikana akabidhiwe kombe haraka.
Mkuu wa Idara ya Masoko wa NBC, David Raymond, amesema helikopta itatumika kusafirisha kombe kwenda kwenye uwanja ambao bingwa atapatikana.
“Kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi na TFF sisi kama wadhamini tukasema kwa ubora wa ligi yetu tuna wajibu wa kuhakikisha ya kwamba tunakwenda kuandaa sherehe mbili ambazo ziko na viwango sawa kabisa,” amesema Raymond.
Ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha mshindi anapata kombe siku hiyo hiyo, kulingana na ukubwa wa ligi na hadhi ya udhamini.
Mapendekezo ya Mhariri:




```






Leave a Reply