Simba Yatoa Tamko Kuhusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Kuchezwa Pemba
Simba imetoa tamko kuhusu uamuzi wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Pemba kuchezwa kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba, huku mashabiki wa klabu hiyo wakionyesha kutoridhishwa na mazingira ya safari kuelekea huko.
Malalamiko hayo yamekuwa yakijitokeza mitandaoni, mashabiki wakieleza ugumu wa kufika Pemba kutokana na gharama za safari, malazi na mazingira ya mchezo huo unaotarajiwa kuzikutanisha Simba na Azam.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Juni 25 mwaka huu lilitangaza kuwa Uwanja wa Gombani ndio utakaotumika kwa fainali hiyo. Mchezo huo utapigwa Julai 4, 2026 kuanzia saa 11:00 jioni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori amesema klabu hiyo imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa mashabiki wake kuhusu uamuzi wa fainali kuchezwa Pemba.

Magori amesema Simba haipingi uamuzi wa TFF, kwa kuwa mamlaka ya kupanga mchezo huo upigwe wapi yapo kwa shirikisho hilo, lakini anaona mashabiki wengi wa timu hiyo watakutana na changamoto kubwa kufika uwanjani.
“Ni kweli tumeona mashabiki wengi wakilalamika, tumewaambia hatuna nafasi ya kubadili hilo kwa kuwa wenye mamlaka ya kuamua mchezo huo unachezwa wapi ni Shirikisho, tunatakiwa kuheshimu hilo,” amesema Magori.
Amesema malalamiko ya mashabiki yana msingi kwa sababu soka hupendeza zaidi pale mashabiki wanapojaza viwanja. Kwa mtazamo wake, gharama za kufika Pemba zinaweza kuwa kikwazo kwa wengi.
“Ukitazama malalamiko yao utaona yana msingi, soka linapendezeshwa na mashabiki wanavyojaa viwanjani, ukifikiria gharama za kufika Pemba utaona kwamba ni kweli kutakuwa na kazi kubwa watu wengi kufika huko,” amesema.
Magori pia ameeleza kuwa hata upande wa uongozi wa Simba, kuna changamoto za kupanga mazingira ya watu wote kukaa pamoja wakati wa safari hiyo, jambo lililosababisha baadhi yao kuanza kutawanywa.
“Uongozi tunasimamia kuipeleka timu lakini huku nako tunakutana na ugumu namna ya kuweka mazingira tulivu ya watu wote kukaa pamoja, tumeanza kuwatawanya baadhi,” amesema.
Kwa mashabiki, moja ya changamoto kubwa iliyotajwa ni malazi. Magori amesema safari ya Pemba si rahisi kuwa ya siku moja kwa mashabiki wengi wanaotoka maeneo mengine, hivyo gharama za sehemu za kulala zinaweza kuongeza mzigo.
“Mashabiki pia watapata shida hiyo ya kupata sehemu zenye unafuu kwenye malazi kwa kuwa haiwezi kuwa safari ya siku moja kufika Pemba na kurudi kwenye familia zao,” amesema.
Ameongeza kuwa wakati mwingine waandaaji wanapaswa kuangalia namna maamuzi kama hayo yanavyoathiri idadi ya mashabiki wanaoweza kuhudhuria mchezo.
“Nadhani wakati mwingine wenzetu wanatakiwa kuliangalia hili, tunaona kwamba utaweza kuwapa nafasi mashabiki wachache, unaweza kuangalia kama Unguja tu Kuna ugumu, je vipi Pemba,” amesema Magori.
Pamoja na changamoto hizo, Magori amewataka mashabiki wa Simba kujitahidi kwenda Pemba kuipa nguvu timu yao katika harakati za kutafuta taji lingine msimu huu.
Simba imefika fainali baada ya kuiondoa Coastal Union kwa jumla ya mabao 4-0 kwenye nusu fainali iliyochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Azam ilikata tiketi ya fainali baada ya kumtoa bingwa mtetezi Yanga kwa mabao 3-2 kwenye nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Hii itakuwa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la CRDB kuzikutanisha Simba na Azam, huku timu zote zikiwa na shauku ya kubeba ubingwa ambao kwa misimu minne mfululizo ulichukuliwa na Yanga.
Tangu msimu wa 2015-2016, mashindano hayo yaliporejea kwa jina la Azam Sports Federation Cup baada ya kusimama kwa takribani miaka 12 kuanzia 2003 hadi 2015, Azam tayari imecheza fainali nne.
Katika fainali hizo, Azam imeshinda moja msimu wa 2018-2019 baada ya kuichapa Lipuli bao 1-0.
Mapendekezo ya Mhariri:




```






Leave a Reply