Rasmi: Yanga Yamtambulisha Manqoba Mngqithi Kuwa Kocha Mkuu
Klabu ya Yanga imemtambulisha rasmi Manqoba Mngqithi kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, akichukua nafasi ya Pedro Goncalves aliyeondoka klabuni Mei 2026.
Uteuzi wa Manqoba Mngqithi Yanga unakuja wakati Mabingwa hao mara tano mfululizo wa NBC Premier League wakijiandaa kwa msimu wa 2026-2027, huku moja ya malengo makubwa ikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya CAF.
Mngqithi, raia wa Afrika Kusini, ametangazwa na Yanga Julai 10, 2026 na amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha timu hiyo.
Kocha huyo anatua Yanga akitokea Golden Arrows ya Afrika Kusini, timu aliyoiwezesha kumaliza nafasi ya sita katika Ligi Kuu ya nchini humo msimu wa 2025-2026 kwa kukusanya pointi 41.
Yanga bado haijaweka wazi lini Mngqithi atawasili nchini kuanza kazi ya kukiandaa kikosi kwa msimu ujao.

Manqoba Mngqithi Yanga achukua nafasi ya Pedro Goncalves
Mngqithi anachukua mikoba ya Pedro Goncalves ambaye Yanga iliachana naye Mei 6, 2026.
Baada ya kuondoka kwa Goncalves, Abdihamid Moallin alikabidhiwa timu kwa muda na kufanikiwa kuiongoza Yanga kutetea taji la Ligi Kuu ya NBC.
Awali Yanga ilihusishwa na Fadlu Davids, lakini pande hizo mbili zilishindwana mezani wakati wa makubaliano.
Hatua ya kumteua Mngqithi sasa inampa kocha huyo jukumu la kukiandaa kikosi cha Yanga kwa msimu mpya na kuendeleza malengo ya klabu ya kushindania mataji.
Manqoba Mngqithi ni nani?
Jina lake kamili ni Manqoba Brilliant Ferrimant Mngqithi, mmoja wa makocha wenye heshima kubwa katika soka la Afrika Kusini.
Mngqithi alizaliwa Aprili 25, 1971 katika eneo la Umzimkhulu, mkoani KwaZulu-Natal. Kabla ya kuingia kwenye ukocha, alikuwa mwalimu wa shule, lakini baadaye aliachana na taaluma hiyo na kujikita katika soka.
Ana Leseni ya UEFA A na zaidi ya miongo miwili ya uzoefu katika ukocha.
Safari yake ya ukocha ilipitia Maritzburg City, Moja United, Highlanders na timu ya Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal kabla ya kupewa nafasi ya kuinoa Golden Arrows mwaka 2007.
Mwaka 2009 aliiongoza Golden Arrows kutwaa ubingwa wa MTN8 baada ya kuifunga Ajax Cape Town mabao 6-0 katika fainali.
Baada ya hapo, Mngqithi alipita AmaZulu na Chippa United kabla ya kurejea Golden Arrows.
Uzoefu wa Manqoba Mngqithi akiwa Mamelodi Sundowns
Hatua nyingine kubwa katika maisha ya ukocha ya Mngqithi ilikua mwaka 2013 ambapo alipojiunga na Mamelodi Sundowns.
Akiwa Sundowns, alianza kama kocha msaidizi chini ya Pitso Mosimane na baadaye alifanya kazi pamoja na Rhulani Mokwena.
Mngqithi alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Sundowns katika kipindi ambacho timu hiyo ilitwaa mataji ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, CAF Champions League mwaka 2016 na CAF Super Cup mwaka 2017.
Mwaka 2020 alipandishwa kuwa kocha mkuu wa pamoja sambamba na Rhulani Mokwena. Wawili hao waliiongoza Sundowns kutwaa mataji mawili mfululizo ya ligi.
Baadaye Mngqithi aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo mwaka 2024, lakini akaondoka mwishoni mwa mwaka huo baada ya matokeo kutokidhi matarajio ya uongozi wa klabu.
Mngqithi ametwaa mataji 11
Katika maisha yake ya ukocha, Mngqithi ametwaa jumla ya mataji 11 makubwa.
Mataji hayo ni Ligi Kuu ya Afrika Kusini mara tano, CAF Champions League mara moja, CAF Super Cup mara moja, Nedbank Cup mara moja, Telkom Knockout mara moja na MTN8 mara mbili.
Kati ya mataji hayo 11, moja la MTN8 alilitwaa akiwa Golden Arrows, huku yaliyobaki yakihusisha kipindi chake akiwa Mamelodi Sundowns.
Rekodi hiyo ni miongoni mwa uzoefu anaokwenda nao Yanga baada ya klabu hiyo kumkabidhi jukumu la kuwa kocha mkuu.
Falsafa ya soka ya kocha mpya wa Yanga
Mngqithi anafahamika kwa falsafa ya soka inayosisitiza umiliki wa mpira, uchezaji wa pasi nyingi na mashambulizi ya haraka kupitia mfumo wa 4-3-3.
Pia anapenda kukuza vipaji vya vijana na kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika kiwango cha juu.
Machi 2025, Mngqithi alirejea kwa mara ya tatu Golden Arrows akiwa na jukumu la kuijenga upya timu hiyo.
Katika msimu wa 2025-2026, aliiongoza Golden Arrows kumaliza nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini kwa pointi 41. Aliondoka mwishoni mwa msimu baada ya mkataba wake kumalizika.
Kazi inayomkabili Manqoba Mngqithi Yanga
Mngqithi anaingia Yanga wakati timu hiyo ikiwa imetwaa ubingwa wa NBC Premier League mara tano mfululizo.
Mbali na kupambania mataji zaidi katika msimu wa 2026-2027, Yanga pia ina hitaji la kufanya vizuri katika mashindano ya CAF.
Msimu wa 2022-2023, Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa kanuni ya bao la ugenini.
Katika msimu ujao, Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Mngqithi akipewa jukumu la kukiandaa kikosi kwa malengo ya klabu ndani na nje ya Tanzania.
Mapendekezo ya Mhariri:




```






Leave a Reply