Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Saa Ngapi? Muda wa Fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB

Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Saa Ngapi? Muda wa Fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB

Leo ndio ile siku ambayo mabingwa wa soka nchini Tanzania watashuhudia mtanange wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambao utawakutanisha Wekundu wa Msimbazi, Simba SC dhidi ya Wana Rambaramba, Azam FC katika mchezo wa kukatana shoka utakaopigwa katika dimba la Uwanja wa Gombani, Pemba.

Kwa mashabiki wanaouliza Simba vs Azam leo saa ngapi, jibu ni kwamba mchezo huu wa fainali utaanza kutimua vumbi majira ya saa 11:00 jioni leo, 04/07/2026, huku kila upande ukiingia uwanjani ukiwa na hesabu za kubeba kombe na kurudi nalo Dar es Salaam.

Simba vs Azam Leo 04/07/2026 Saa Ngapi? Muda wa Fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB

Fainali ya heshima kwa Simba na Azam

Simba na Azam zinakutana kwenye fainali hii baada ya kushuhudia Yanga ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ikiiacha Simba nafasi ya pili na Azam nafasi ya tatu.

Kwa mazingira hayo, Kombe la Shirikisho la CRDB limebaki kuwa taji muhimu kwa timu zote mbili msimu huu. Filimbi ya mwisho itakapopulizwa Pemba, upande mmoja utakuwa na furaha ya ubingwa, huku mwingine ukibaki na maumivu ya kupoteza fainali.

Hii pia ni mara ya kwanza kwa Simba na Azam kukutana katika hatua hii ya fainali ya michuano hiyo.

Simba ilivyofika fainali

Simba imetinga fainali baada ya kuiondoa Coastal Union kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa Juni 20, 2026 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Wekundu wa Msimbazi wanaliangalia taji hili kama nafasi ya kutuliza presha ya mashabiki wao baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC, ambao umeendelea kusalia kwa Yanga kwa msimu wa tano mfululizo.

Simba pia inaingia kwenye fainali ikiwa na rekodi nzuri kwenye mashindano haya tangu yaliporejea mwaka 2015. Imetwaa taji hilo mara tatu; msimu wa 2016-2017 ilipoifunga Mbao FC mabao 2-1, msimu wa 2019-2020 ilipoifunga Namungo kwa matokeo kama hayo, na msimu wa 2020-2021 ilipoifunga Yanga bao 1-0.

Azam ilivyokata tiketi ya fainali

Azam ilifika fainali baada ya kuivua ubingwa Yanga kwenye nusu fainali ya pili iliyopigwa Juni 21, 2026 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Matajiri hao wa Dar es Salaam waliibuka na ushindi wa mabao 3-2, matokeo yaliyowapa nafasi ya kwenda kukutana na Simba kwenye fainali ya leo.

Azam inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kiu ya kuongeza taji la pili la michuano hii katika historia ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004.

Rekodi za Simba na Azam kwenye fainali

Historia ya fainali za michuano hii inaibeba zaidi Simba, ambayo imeshinda taji mara tatu tangu kurejea kwa mashindano hayo mwaka 2015.

Kwa upande wa Azam, imeshinda taji hilo mara moja, ilipoifunga Lipuli bao 1-0 msimu wa 2018-2019.

Hata hivyo, Azam pia imepitia maumivu ya kupoteza fainali mara tatu dhidi ya Yanga. Ilipoteza kwa mabao 3-1 msimu wa 2015-2016, ikapoteza kwa bao 1-0 msimu wa 2022-2023, kisha ikalikosa taji msimu wa 2023-2024 kwa mikwaju ya penalti 6-5.

Barker aingia na hesabu za kufunga msimu vizuri

Kocha wa Simba, Steven Barker, alishatangaza vita kuelekea fainali hii, akisema wataingia uwanjani wakiwa na akili moja tu ya kuhakikisha wanalichukua taji.

Kama Simba itafanikiwa, hili litakuwa taji la pili kwao msimu huu baada ya awali kutwaa Kombe la Muungano kwa kuifunga Yanga bao 1-0.

Simba inaingia kwenye fainali ikiwa haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi wala mashindano haya chini ya Barker, ambaye amefanikiwa kurudisha kiwango bora cha Wekundu wa Msimbazi.

Nguvu nyingine ya Simba ipo kwenye ukuta wake, uliomaliza ligi ukiwa umeruhusu mabao 11 kwenye mechi 30. Safu yake ya ushambuliaji nayo ilifunga mabao 54.

Kwenye mchezo wa leo, Simba itawategemea wachezaji kama Elie Mpanzu, ambaye sasa anatumika kama mshambuliaji wa mwisho, pamoja na Clatous Chama, Libasse Gueye na Anicet Oura, ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye mechi za hivi karibuni.

Azam haijaja kinyonge Pemba

Azam nayo inaingia kwenye fainali ikiwa na kumbukumbu ya kutopoteza dhidi ya Simba kwenye msimu huu wa ligi. Matajiri hao wa Chamazi waliifunga Simba kwenye mchezo mmoja wa mzunguko wa kwanza wa ligi, kisha timu hizo zikatoka sare katika mchezo wa pili.

Chini ya kocha Florent Ibenge, Azam inaliona taji hili kama nafasi ya kuunogesha msimu wa 2025-2026.

Kabla ya fainali, Azam pia iliwapumzisha baadhi ya wachezaji wake muhimu katika mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji, ambao ilishinda mabao 2-0.

Miongoni mwa waliopumzishwa ni Feisal Salum ‘Fei Toto’, licha ya kuwa alikuwa anawania rekodi ya mfungaji bora, ambayo ilienda kwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, Mosi Nduwumwe.

Maandalizi ya mwisho Pemba

Azam ilikuwa ya kwanza kuwasili Pemba kwa ajili ya mchezo huu, ikitumia usafiri wa boti. Timu hiyo iliwahi kufika kisiwani humo kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa kabla ya fainali.

Simba ilitua Pemba siku moja kabla ya mechi kwa ndege, ikitokea moja kwa moja Dar es Salaam. Kabla ya safari hiyo, kikosi cha Simba kilifanya mazoezi ya mwisho, kisha jana kikajifua Pemba kuanzia saa 12 jioni.

Waamuzi wa fainali ya Simba vs Azam

Fainali hii itachezeshwa na mwamuzi wa kati Sifu Amoni kutoka Mbeya.

Atasaidiwa na Hamdani Said kutoka Mtwara na Zawadi Yusuph kutoka Dar es Salaam, huku Ahmed Arajiga kutoka Manyara akiwa mwamuzi wa akiba.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Orodha ya Mabingwa Ligi kuu Tanzania Bara
  2. Mfungaji Bora Ligi Kuu ya NBC 2025/2026
  3. Yanga Yatwaa Ubingwa wa Tano Mfululizo NBC Premier League 2025/26
  4. Vinara wa Assist Ligi Kuu ya NBC 2025/2026
  5. Hawa Apa Wafungaji Bora Ligi Kuu ya NBC 2025/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo