Simba SC vs Pamba Jiji Leo June 14 2026 Saa Ngapi?
Wekundu wa Msimbazi leo watakua katika kibarua cha kuzisaka pointi tatu dhidi ya Pamba Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam. Mechi hiyo itaanza saa 10:00 jioni na kurushwa mubashara kupitia AzamSports1HD.

Simba inaingia kwenye mchezo huu ikisaka pointi tatu muhimu katika mbio za kuufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Wekundu hao wako nyuma ya Yanga kwa pointi mbili, huku Yanga ikiwa kileleni na pointi 60 baada ya mechi 25 kabla ya mchezo wake wa jana dhidi ya Mashujaa.
Ushindi kwa Simba utaongeza presha kwenye mbio za ubingwa, wakati Pamba Jiji nayo inahitaji matokeo mazuri ili kuendelea kukaa katika sehemu salama ya msimamo na kubaki Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Mara ya mwisho Simba na Pamba Jiji kukutana
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Kirumba, Pamba Jiji ililazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba. Simba walitangulia kupata bao kupitia Anicet Oura, kabla ya James Mwashinga kusawazisha kwa upande wa Pamba.
Matokeo hayo yanaipa mechi ya leo uzito zaidi, hasa kwa Simba ambao wanajua Pamba si timu ya kubeza. Simba pia inakumbuka ilivyopata ushindi wa tabu dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa KMC Complex, bao pekee likifungwa na Ellie Mpanzu baada ya penalti iliyokoswa na Clotous Chama.
Simba haijaangusha alama katika mechi sita zilizopita
Simba imekuwa kwenye mwendo mzuri katika Ligi Kuu Bara. Timu hiyo haijaangusha alama yoyote katika mechi zake sita zilizopita, na tangu ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga, imeshinda mechi zote za ligi hadi sasa.
Kiwango hicho kinaifanya Simba kuendelea kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo, huku mchezo wa leo dhidi ya Pamba Jiji ukiwa sehemu muhimu ya kuendeleza presha kwenye kilele cha ligi.
Chama arejea kikosini
Habari njema kwa Simba ni kupona kwa kiungo wake Clotous Chama, ambaye alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji. Chama amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Simba, akiwa amefunga mabao nane na kutoa asisti sita.
Urejeo wake unaweza kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji, huku Simba pia ikiwa na Anicet Oura na Lebasse Gueye, ambao ni wachezaji hatari katika kikosi cha Wekundu hao.
Barker: Tunafahamu haitakuwa mechi rahisi
Kocha wa Simba, Steven Barker, amesema mapumziko mafupi ya kalenda ya FIFA yamewasaidia wachezaji wake kupata muda wa kurejesha nguvu baada ya kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi.
“Tulipata muda mzuri wa kupumzika, wachezaji wetu hapo kabla walikuwa na uchovu mkubwa wa kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi. Sasa wako sawa tumefanya mazoezi ya kutosha, tunafahamu haitakuwa mechi rahisi. Hii ndio moja ya timu ambayo ilitupa mechi ngumu tulipokutana nayo kwao, hivyo tutakuwa makini tuweze kushinda,” alisema Barker.
Rekodi za Pamba Jiji kabla ya kuikabili Simba
Pamba Jiji tayari imeshatua Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa saa 10:00 jioni. Timu hiyo imefanya mazoezi mara tatu tangu ilipowasili jijini, huku wachezaji wake wote wakiwa tayari kwa mchezo.
Katika mechi tano za mwisho, Pamba imeshinda moja tu, dhidi ya KMC kwa bao 1-0. Pia imepoteza michezo mitatu dhidi ya Tanzania Prisons nyumbani, Azam ugenini na Singida Black Stars, kabla ya kutoa sare moja dhidi ya Dodoma Jiji.
Pamba Jiji, inayofundishwa na kocha Mkenya Francis Baraza, inashika nafasi ya saba kwenye msimamo. Timu hiyo itamtegemea mshambuliaji wake Mathew Tegisi, ambaye ana mabao saba.
Soma Pia




```







Leave a Reply