Yanga Yaanza Mchakato wa Kumsaka Mrithi wa Pedro

Yanga Yaanza Mchakato wa Kumsaka Mrithi wa Pedro

Yanga imeanza mchakato wa haraka wa kutafuta kocha mpya baada ya kuachana na Pedro Concalves, aliyeondolewa Mei 6, 2026, saa chache baada ya mchezo wa Ligi Bara dhidi ya KMC.

Pedro ameondoka akiwa ameiongoza Yanga kwenye mechi 35 za mashindano yote msimu huu tangu alipoanza kazi Oktoba 28, 2025, akichukua nafasi ya Romain Folz. Mechi yake ya mwisho ilikuwa dhidi ya KMC, ambapo Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0.

Mara baada ya kuondoka kwa kocha huyo raia wa Ureno, mabosi wa juu wa Yanga walianza kuzunguka kutafuta kocha mpya wa kuchukua nafasi yake. Jina la Khalil Ben Youssef, raia wa Tunisia, limeibuka mapema kwenye hesabu za klabu hiyo.

Ben Youssef si jina geni ndani ya Yanga. Aliwahi kufanya kazi klabuni hapo akiwa kocha msaidizi wa Nasreddine Nabi wakati Yanga ikiwa chini ya kocha huyo. Alikuwepo katika kipindi ambacho timu hiyo ilikuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia hatua ya robo fainali msimu ambao Yanga ilifika fainali mwaka 2023 dhidi ya USM Alger ya Algeria.

“Tumeshaanza mazungumzo, tumeanza na yule Khalil (Ben Youssef) nadhani unamkumbuka ni kocha mzuri sana, tunaona ni bora tutafute kocha wa kisasa kijana ambaye anajua mazingira ya soka la Tanzania,” amesema bosi huyo wa juu ndani ya Yanga.

Kwa sasa Ben Youssef yupo Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini akiwa kocha mkuu sambamba na Cedric Kaze wa Burundi. Wawili hao walichukua nafasi hiyo baada ya klabu hiyo kuachana na Nabi.

Yanga Yaanza Mchakato wa Kumsaka Mrithi wa Pedro

Mwenendo wa Ben Youssef Kaizer Chiefs

Ben Youssef, mwenye umri wa miaka 37, ameiongoza Kaizer Chiefs katika mechi 10 za Kombe la Shirikisho Afrika, akishinda tano, kupoteza tatu na kutoka sare mbili. Katika hatua ya makundi, timu hiyo ilimaliza na pointi 10 ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Al Masry na Zamalek.

Kwenye ligi, ameiongoza Kaizer Chiefs katika mechi 20, akishinda tisa, kupoteza nne na kutoka sare saba. Timu hiyo ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 48 baada ya kucheza mechi 27, nyuma ya Orlando Pirates yenye pointi 62 na Mamelodi Sundowns yenye pointi 65.

Kwa mujibu wa mchakato unaoendelea, dili la Ben Youssef linaweza pia kumrudisha Cedric Kaze Yanga endapo mazungumzo yataenda vizuri. Kaze akiirejea Yanga, itakuwa mara yake ya tatu kuhusishwa na klabu hiyo baada ya awali kuja akitokea Canada kabla ya baadaye kurejea tena kama msaidizi wa Nabi.

Kwa nini jina la Ben Youssef linaangaliwa Yanga

Moja ya mambo yanayompa Ben Youssef nafasi katika mazungumzo hayo ni uzoefu wake wa mazingira ya Yanga na soka la Tanzania. Pia, mfumo wake wa 4-2-3-1 unaelezwa kuwa si mgeni kwa wachezaji wa Yanga, kwa kuwa umewahi kutumiwa na makocha mbalimbali waliopita klabuni hapo, wakiwemo Nabi, Miguel Gamondi na Miloud Hamdi.

Hata hivyo, wakati Yanga ikiendelea na mchakato wa kuunda benchi jipya la ufundi, klabu hiyo imetangaza kuwa kikosi kitaendelea kuwa chini ya Abdihamid Moalin na Patrick Mabedi hadi mwisho wa msimu.

Kwa sasa macho ya mashabiki wa Yanga yapo kwenye uamuzi wa mwisho wa klabu kuhusu mrithi wa Pedro. Jina la Ben Youssef limeanza kutajwa mapema, lakini hatima ya mazungumzo hayo itategemea mwendelezo wa hatua zinazofanywa na uongozi wa klabu.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Mambo 6 Yaliyosababisha Pedro Kufungashiwa Vilago Yanga
  2. Harry Kane Aifikia Rekodi ya Cristiano Ronaldo Ligi ya Mabingwa Ulaya
  3. Rasmi: Simba SC Yahamishia Michezo ya Nyumbani Uwanja wa KMC
  4. Rasmi: Yanga SC Yatangaza Kumfuta Kazi Kocha Pedro Gonçalves
  5. Ratiba ya Ligi Kuu Ya NBC Leo 06/05/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo