Orodha ya Marefa Watakaochezesha Simba vs Yanga Leo 03/05/2026
Dar es Salaam. Waamuzi kutoka Morocco wamepangiwa kusimamia mechi ya dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga SC itakayochezwa leo Jumamosi, Mei 3, 2026, saa 12 jioni katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. Uamuzi huo umetangazwa na Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu, Karim Boimanda, ambaye ameeleza kuwa uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia kanuni za ligi na taratibu za kawaida zinazotumika katika mechi zenye umuhimu mkubwa.
Boimanda amesema kuwa matumizi ya waamuzi wa nje hayakutokana na ombi la klabu yoyote kati ya Simba au Yanga, bali ni sehemu ya mfumo unaoruhusiwa kikanuni pale kamati husika inapobaini kuwa kuna ulazima wa kufanya hivyo. Amesema kamati inaweza kutumia waamuzi wa ndani au wa nje kulingana na uamuzi wake na mahitaji ya mchezo husika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, marefa walioteuliwa kuendesha pambano hilo kubwa ni Hamza El Fareq ambaye atakuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Lahsen Agaou, Hamza Massiri na Mustapha Kechaf wote kutoka Morocco. Uteuzi huo umeifanya dabi ya Kariakoo kuvutia zaidi kutokana na ukubwa wa mchezo wenyewe na maslahi ya timu zote mbili katika mbio za ubingwa.
Simba Yajipanga Kutafuta Matokeo
Kocha wa Simba, Steve Barker, amesema mchezo wa leo ni mtihani mgumu kwa timu yake kutokana na uimara wa Yanga katika safu ya ulinzi. Ameeleza kuwa kushinda mechi hiyo kutategemea zaidi uwezo wa Simba kutumia nafasi zitakazopatikana.
Kwa mujibu wa kocha huyo, Simba inahitaji kufunga mabao ili kuweza kupata ushindi, akibainisha kuwa safu ya ulinzi ya Yanga si rahisi kuivunja. Hata hivyo, amesema kikosi chake kiko katika hali nzuri na kimejipanga kupata matokeo yatakayosaidia kupunguza tofauti ya pointi.
Kwa upande wake, beki wa Simba, Rushine De Reuck, amesema wachezaji wamejipanga kuhakikisha wanawapa mashabiki wao furaha kupitia matokeo mazuri katika mchezo huo mkubwa.
Yanga Yajibu kwa Ujasiri Kabla ya Mchezo
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kipigo walichopata katika fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Simba hakihusiani na mchezo wa ligi kuu. Amesisitiza kuwa kila mashindano yana uzito wake na kila mchezo huja na mazingira yake.
Yanga ilipoteza kwa mabao 1-0 katika fainali hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Hata hivyo, Pedro amesema timu yake imejipanga upya na inaamini inaweza kucheza vizuri leo.
Yanga itakosa huduma ya kiungo Mudathir Yahya, ambaye anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu. Licha ya pengo hilo, kocha huyo amesema kikosi kimezoea kucheza bila mchezaji huyo na kipo tayari kwa mtihani wa leo.
Mapendekezo ya Mhariti:








Leave a Reply