Ratiba ya Ligi Kuu Ya NBC Leo 14/05/2026
Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea leo, Mei 14, 2026, kwa michezo minne itakayopigwa kuanzia saa 8:00 mchana. Michezo hiyo inahusisha Mtibwa Sugar dhidi ya KMC FC, Tanzania Prisons dhidi ya Fountain Gate, Mashujaa FC dhidi ya Simba SC, pamoja na Azam FC dhidi ya Pamba Jiji.
Pambano kati ya Mashujaa na Simba ndilo linalotarajiwa kufuatiliwa zaidi, likipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma kuanzia saa 10:15 jioni. Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na mwenendo mzuri wa matokeo, wakati Mashujaa ikilinda rekodi yake ya kutopoteza nyumbani msimu huu.
Michezo ya mapema itaanza saa 8:00 mchana, ambapo Mtibwa Sugar itaikaribisha KMC FC kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Wakati huohuo, Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Baada ya michezo hiyo, Mashujaa itacheza na Simba saa 10:15 jioni, kabla ya Azam FC kuhitimisha ratiba ya siku kwa kuikaribisha Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kuanzia saa 12:30 jioni.
Ratiba ya Mechi za Ligi Kuu Ya NBC Leo 14/05/2026
| Muda | Mchezo | Uwanja/Mji |
|---|---|---|
| Saa 8:00 mchana | Mtibwa Sugar vs KMC FC | Uwanja wa Jamhuri, Morogoro |
| Saa 8:00 mchana | Tanzania Prisons vs Fountain Gate | Uwanja wa Sokoine, Mbeya |
| Saa 10:15 jioni | Mashujaa FC vs Simba SC | Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma |
| Saa 12:30 jioni | Azam FC vs Pamba Jiji | Azam Complex, Dar es Salaam |

Simba inakwenda Kigoma ikiwa imeshinda mechi nne kati ya tano zilizopita na kutoka sare moja dhidi ya Yanga. Katika michezo hiyo, Wekundu hao wamefunga mabao 13 na kuruhusu matatu.
Kwenye safu ya ushambuliaji, Simba itamtegemea Seleman Mwalimu, ambaye anaongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho akiwa nayo saba. Clatous Chama pia atakuwa miongoni mwa wachezaji wa kuangaliwa, baada ya kufunga mabao matatu katika mechi tatu zilizopita.
Simba pia ina rekodi nzuri dhidi ya Mashujaa kwenye ligi. Katika michezo mitano iliyopita iliyozikutanisha timu hizo, Simba imeshinda yote, ikifunga mabao manane na kuruhusu moja.
Hata hivyo, Mashujaa imekuwa imara nyumbani msimu huu. Timu hiyo inayonolewa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ haijapoteza mchezo wowote wa nyumbani, ikiwa imeshinda minne na kutoka sare saba.
Kocha wa Simba, Steve Barker, alisema mchezo huo unahitaji umakini kutokana na namna Mashujaa inavyocheza ikiwa nyumbani.
“Nilikuwa naangalia mechi ya mwisho tulipocheza nao, ilikuwa ngumu, naamini pia haitakuwa rahisi safari hii kwani ni timu inayoonyesha upinzani mkubwa ikiwa nyumbani, lakini tunataka kuendelea kushinda, naamini wachezaji wangu watatekeleza vizuri mpango wa mechi hii,” alisema Barker.
Kwa upande wa Mashujaa, Julio alisema timu yake inaiheshimu Simba, lakini itaingia uwanjani bila hofu.
“Tunaiheshimu Simba lakini kama ambavyo siku zote nimekuwa nikisema, sidhani kama tuna sababu ya kucheza kwa hofu dhidi yao, nimewaambia wachezaji hizi ndio mechi ambazo zitawatambulisha juu ya ubora wao, tutakwenda kuwapa shida kucheza kwa utulivu wao,” alisema Julio.
Mashujaa haijapoteza katika mechi tano zilizopita, ikiwa imeshinda moja na kutoka sare nne. Ushindi wake wa hivi karibuni ulikuwa dhidi ya TRA United kwa bao 1-0.
Tangu Julio achukue timu hiyo kutoka kwa Salum Mayanga, Mashujaa haijapoteza mchezo wowote. Katika michezo mitano ya mwisho, kikosi hicho kimefunga mabao mawili.
Mashujaa ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 26, baada ya kufunga mabao 11 na kuruhusu 19. Takwimu hizo ni kabla ya mechi za jana. Simba italazimika kuwa makini na Jafary Kibaya, aliyefunga mabao mawili, pamoja na Ismail Mgunda aliyefunga dhidi ya TRA United.
Mapendekezo ya Mhariri:






Leave a Reply