Kikosi cha Simba Queens vs Yanga Princess Leo 15/05/2026
Simba Queens na Yanga Princess zinakutana leo kwenye dabi ya Ligi ya Wanawake Tanzania katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kuanzia saa 11 jioni.
Mchezo huo unakuja baada ya mechi ya watani wa jadi kwa upande wa wanaume kati ya Simba na Yanga kumalizika kwa sare ya 2-2, huku sasa macho yakihamia kwa timu za wanawake katika pambano lenye uzito mkubwa kwenye mbio za ubingwa.
Simba Queens inaingia kwenye mchezo huu ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 43 baada ya kucheza mechi 15. Katika mechi hizo, imeshinda 14 na kutoka sare moja, ikiwa bado haijapoteza mchezo msimu huu.
Yanga Princess ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 39 baada ya idadi hiyo hiyo ya michezo. Tofauti ya pointi nne kati ya timu hizo mbili inaifanya dabi hii kuwa na umuhimu mkubwa kwa kila upande.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Yanga Princess ikiwa mwenyeji ilipoteza kwa mabao 2-0. Mabao ya Simba Queens yalifungwa na Jentrix Shikangwa na Aisha Mnunka.
Ushindi kwa Simba Queens leo utaifanya timu hiyo kufikisha pointi 46 na kuongeza pengo dhidi ya Yanga Princess hadi pointi saba. Kwa upande wa Yanga Princess, ushindi utawapeleka hadi pointi 42 na kupunguza tofauti hadi pointi moja.
Mbali na mbio za ubingwa, matokeo ya mchezo huu yanaweza kuathiri pia nafasi ya pili. JKT Queens ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 38, pointi moja nyuma ya Yanga Princess. Hivyo, Yanga Princess inaingia uwanjani ikifahamu kwamba kupoteza kunaweza kuifanya ishuke kwenye nafasi ya pili.
Rekodi za miaka ya karibuni zinaibeba Simba Queens. Tangu mwaka 2019, timu hizo zimekutana mara 18 kwenye mashindano mbalimbali, Simba Queens ikishinda mara 12, Yanga Princess mara tatu, huku mechi tatu zikimalizika kwa sare.
Katika ligi, zimekutana mara 14. Simba Queens imeshinda mara 10, sare mbili na kupoteza mara mbili. Yanga Princess imeshinda mara mbili, imetoka sare mbili na kupoteza mara mbili.

Kikosi cha Simba Queens Dhidi ya Yanga Princess Leo 15/05/2026
Kikosi cha Simba Queens kitakachoanza dhidi ya Yanga Princess leo kinatarajiwa kutangazwa na benchi la ufundi muda mchache kabla ya mchezo kuanza saa 11 jioni katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mashabiki wanatarajia kuona Kocha Mussa Hassan ‘Mgosi’ akipanga kikosi kitakachohakikisha Simba Queens inaanza mchezo kwa nguvu, ikitafuta bao la mapema na kudhibiti kasi ya Yanga Princess katika dakika za mwanzo.
Kikosi cha Simba Queens Kilichotangazwa vs Yanga Princess
- Ruth Aturo
- Zainah Nandede
- Asha Omary
- Ruth Ingosi
- Brice Zanga
- Elizabeth Joseph
- Aisha Juma
- Vivian Corazone ©
- Jentrix Shikangwa
- Fasila Adhiambo
- Elizabeth Wambui
Subs: Janeth S, Doto, Fatuma, Elizabeth, Zawadi, Emeliana, Ernestine, Janeth, Zawadi.
Mapambano ya Makocha na Wachezaji Muhimu
Pambano hili pia linabeba vita ya kiufundi kati ya makocha Edna Lema wa Yanga Princess na Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba Queens.
Edna Lema hataiongoza timu yake akiwa benchi kutokana na adhabu ya kadi nyekundu aliyopata katika mchezo uliopita. Hata hivyo, maandalizi yake, falsafa ya timu na maelekezo yake vinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mpango wa Yanga Princess.
Katika eneo la ushambuliaji, Yanga Princess inamtegemea Jeannine Mukandayisenga, ambaye anaongoza kwa mabao akiwa na 19. Kwa upande wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa ni miongoni mwa wachezaji wa kutegemewa akiwa na mabao 12.
Simba Queens imekuwa na safu imara ya ulinzi baada ya kuruhusu mabao mawili pekee katika mechi 15. Yanga Princess, kwa upande wake, imefunga mabao 44 na kuruhusu 13.
Kauli za Wachezaji Kabla ya Dabi
Mshambuliaji wa Simba Queens, Aisha Mnunka, amesema mchezo huo ni mkubwa na ushindi unaweza kuwapa nafasi nzuri katika mbio za ubingwa.
“Ni mechi kubwa kila mmoja amejiandaa kwa namna yake sisi tumejiandaa vizuri kwa ajili ya pointi tatu laakni siwezi kumzungumzia zaidi mpinzani yote kwa yote itaenda kujulikana nani mshindi na itaenda kutupa tasiwira nzuri,” alisema Mnunka.
Kiungo wa Yanga Princess, Agnes Pallangyo, amesema dabi haiamuliwi na mbinu pekee za makocha, bali pia kujitoa kwa wachezaji uwanjani.
“Naamini kila mchezaji ana morali na anatamani kushinda mechi kwa sababu ni mechi ya maamuzi, mbinu pekee hazitoshi kwa sababu muda mwingine inaweza kukubalia au kukataa ikikataa jitihada zetu zitaamua.”
Umuhimu wa Mchezo kwa Mbio za Ubingwa
Kwa Simba Queens, pointi tatu zitakuwa hatua muhimu ya kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuusogelea ubingwa. Timu hiyo pia itaendelea kulinda rekodi yake ya kutopoteza mchezo msimu huu.
Kwa Yanga Princess, ushindi utakuwa na maana kubwa katika kurejesha presha kwenye mbio za ubingwa na kuendelea kulinda nafasi yake dhidi ya JKT Queens iliyo karibu kwenye msimamo.
Dabi hii inabeba heshima, historia na ushindani wa moja kwa moja katika nafasi za juu za ligi. Matokeo yake yanaweza kuwa na athari kubwa kwa mwelekeo wa mbio za ubingwa msimu huu.
Mapendekezo ya Mhariri:







Leave a Reply