Mashujaa v Simba Leo 14/05/2026 Saa Ngapi?

Mashujaa v Simba Leo 14/05/2026 Saa Ngapi?

Wekundu wa Msimbazi leo watakuwa ugenini kuchuana dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC wenye umuhimu mkubwa kwa Simba katika kujiweka sehemu nzuri zaidi kwenye mbio za ubingwa wa ligi, hasa baada ya Yanga SC inayoshika nafasi ya juu kuchapwa na Dodoma Jiji katika mchezo uliochezwa hapo jana.

Mchezo huo utapigwa leo Mei 14, 2026 katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, huku Simba ikihitaji matokeo ya ushindi ili kuendelea kuongeza presha kwenye mbio za ubingwa. Mashujaa, kwa upande wao, wataingia uwanjani wakitegemea rekodi yao nzuri ya kutopoteza nyumbani msimu huu.

Simba itakuwa ikitegemea mwendelezo wake mzuri wa matokeo baada ya kushinda mechi nne na kutoka sare moja katika michezo mitano iliyopita. Katika kipindi hicho, Wekundu hao wamefunga mabao 13 na kuruhusu matatu pekee.

Kwenye eneo la ushambuliaji, Seleman Mwalimu anatajwa kuwa moja ya silaha muhimu za Simba akiwa anaongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho akiwa nayo saba. Clatous Chama pia ataangaliwa kwa karibu baada ya kurejea kwenye kiwango bora na kufunga mabao matatu katika mechi tatu zilizopita.

Kwa upande wa Mashujaa, timu hiyo inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza nyumbani msimu huu. Mashujaa imeshinda michezo minne na kutoka sare saba katika uwanja wake wa nyumbani, jambo linaloufanya mchezo huu kuwa mtihani mkubwa kwa Simba.

Mashujaa v Simba Leo 14/05/2026 Saa Ngapi?

Mashujaa Wajipanga Kuzuia Kasi ya Simba

Mashujaa, chini ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, haijapoteza katika mechi zake tano zilizopita. Timu hiyo imeshinda mchezo mmoja dhidi ya TRA United kwa bao 1-0 na kutoka sare nne.

Simba pia ina kumbukumbu nzuri dhidi ya Mashujaa, baada ya kushinda michezo yote mitano ya ligi iliyowakutanisha timu hizo. Katika michezo hiyo, Simba imefunga mabao manane na kuruhusu bao moja.

Kocha wa Simba, Steve Barker, alisema anaamini mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na ubora wa Mashujaa inapocheza nyumbani.

“Nilikuwa naangalia mechi ya mwisho tulipocheza nao, ilikuwa ngumu, naamini pia haitakuwa rahisi safari hii kwani ni timu inayoonyesha upinzani mkubwa ikiwa nyumbani, lakini tunataka kuendelea kushinda, naamini wachezaji wangu watatekeleza vizuri mpango wa mechi hii,” alisema Barker.

Julio, kwa upande wake, alisema Mashujaa inaiheshimu Simba, lakini haitacheza kwa hofu.

“Tunaiheshimu Simba lakini kama ambavyo siku zote nimekuwa nikisema, sidhani kama tuna sababu ya kucheza kwa hofu dhidi yao, nimewaambia wachezaji hizi ndio mechi ambazo zitawatambulisha juu ya ubora wao, tutakwenda kuwapa shida kucheza kwa utulivu wao,” alisema Julio.

Umuhimu wa Mechi kwa Simba

Kwa Simba, mchezo huu una uzito mkubwa katika mbio za ubingwa. Ushindi ugenini dhidi ya Mashujaa unaweza kuipa timu hiyo nguvu zaidi katika kuendelea kufukuzia nafasi za juu, hasa katika kipindi ambacho kila pointi ina umuhimu mkubwa.

Hata hivyo, Simba italazimika kuwa makini dhidi ya Mashujaa ambayo imekuwa ngumu kufungika nyumbani. Rekodi hiyo ya wenyeji ndiyo jambo kubwa ambalo Wekundu wa Msimbazi wanapaswa kulivuka leo Kigoma.

Mashujaa v Simba ni moja ya michezo inayosubiriwa zaidi leo katika Ligi Kuu ya NBC, ikikutanisha Simba inayotafuta kuendeleza kasi ya ubingwa dhidi ya Mashujaa inayotaka kulinda rekodi yake ya nyumbani.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Dodoma Jiji Yaitungua Yanga 3-2 Singida na Kutibua Hesabu za Ubingwa
  2. Msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Baada ya Mechi za Leo Mei 13, 2026
  3. Msimamo wa EPL Leo 10/05/2026 Ligi Kuu ya Uingereza
  4. Washindi wa Tuzo Za BMT 2026
  5. Rekodi Nne za Azam FC Zavunjwa na TRA United Baada ya Kipigo cha 4-1
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo