Simba VS Tanzania Prisons Leo 10/05/2026 Saa Ngapi?
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, leo watakuwa dimbani kusaka pointi tatu muhimu watakapokabiliana na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 01:00 usiku, huku Simba ikiwa mwenyeji dhidi ya Prisons inayopambana kujinasua kutoka kwenye presha ya kushuka daraja.

Simba inaingia kwenye mchezo huu ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 46. Timu hiyo inahitaji ushindi ili kuendelea kuipa presha Yanga, ambayo inaongoza msimamo na kutetea ubingwa wake.
Kwa upande wa Tanzania Prisons, hali si nzuri kwenye msimamo. Timu hiyo ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 14, na hata ikishinda dhidi ya Simba bado itaendelea kubaki kwenye nafasi hiyo kutokana na tofauti ya pointi kati yake na Mbeya City iliyo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 21.
Simba inatoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania. Baada ya mchezo huo, klabu hiyo imelazimika kuhamia Uwanja wa KMC Complex, ambao msimu huu umetumiwa pia na Yanga na KMC FC.
Historia ya timu hizi inaipa Simba rekodi bora zaidi. Katika michezo 19 ya ligi iliyopita baina yao, Simba imeshinda mara 12, Tanzania Prisons imeshinda mara nne, huku michezo mitatu ikiisha kwa sare.
Mwenendo wa karibuni pia unaonyesha Simba imekuwa na matokeo mazuri zaidi. Katika mechi tano za mwisho, Simba imeshinda tatu dhidi ya JKT Tanzania, Namungo na Fountain Gate, huku ikitoa sare dhidi ya Yanga na TRA United.
Tanzania Prisons imepoteza michezo minne kati ya mitano ya mwisho dhidi ya Mbeya City, TRA United, Yanga na Singida Black Stars. Pointi yake pekee katika kipindi hicho ilitokana na sare dhidi ya KMC.
Rekodi za Karibuni na Maandalizi ya Timu
Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema wanatarajia mchezo mgumu dhidi ya Tanzania Prisons licha ya nafasi ya wapinzani wao kwenye msimamo.
“Siku zote hakuna mechi rahisi kati yetu Simba na Prisons, mechi hii itakuwa ngumu, tumejipanga kukabiliana na ugumu huo, tumejiandaa vizuri kutafuta ushindi ili kuendelea kuutafuta ubingwa msimu huu,” alisema Matola.
Simba itawakosa wachezaji wawili katika mchezo huu. Nahodha Shomari Kapombe ataukosa mchezo kutokana na majeraha, huku Anicet Oura akiwa ameanza mazoezi lakini bado kukiwa na uwezekano mdogo wa kurejea uwanjani kwenye mechi hii.
Kwa upande wa Prisons, kocha Shadrack Nsajigwa amekiri kikosi chake hakipo kwenye nafasi nzuri, lakini amesema hawana nafasi ya kukata tamaa.
“Nikweli hatupo kwenye nafasi nzuri lakini hatuna nafasi ya kukata tamaa, lolote linaweza kutokea, haitakuwa mechi rahisi kwetu dhidi ya Simba lakini tumejiandaa kukabiliana nao, tunataka kutafuta pointi yoyote kesho (leo),” alisema Nsajigwa.
Umuhimu wa Mchezo kwa Pande Zote
Kwa Simba, mchezo huu ni sehemu ya hesabu za kuendelea kupambana kwenye mbio za ubingwa. Timu hiyo inahitaji kuendeleza ushindi ili kupunguza presha ya pengo la pointi dhidi ya Yanga.
Kwa Tanzania Prisons, mchezo huu una maana kubwa katika mapambano ya kujiondoa kwenye eneo hatari la msimamo. Timu hiyo haijashinda tangu Februari 14, 2026, ilipoifunga Namungo mabao 3-2 nyumbani.
Tangu Shadrack Nsajigwa apewe jukumu la kukinoa kikosi hicho, Tanzania Prisons bado haijapata ushindi. Hilo linaongeza uzito wa mchezo huu dhidi ya Simba, ambayo inaingia uwanjani ikiwa na rekodi nzuri zaidi na nafasi bora kwenye msimamo.
Simba na Tanzania Prisons zinaingia kwenye mchezo huu zikiwa na malengo tofauti lakini muhimu. Simba inahitaji ushindi ili kuendelea kuutafuta ubingwa, wakati Prisons inahitaji pointi ili kupunguza presha ya kushuka daraja.







Leave a Reply