Yanga Yaingia Mawindondi Kuisaka Saini ya Mohamed Omar Ali
Yanga SC imeanza mapema harakati za kuboresha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, safari hii ikielekeza macho yake katika soko la wachezaji wa Kenya kwa nia ya kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Mabingwa hao wa kihistoria nchini Tanzania wanatajwa kuwa katika mazungumzo ya kumsajili kiungo mshambuliaji kijana mwenye kipaji, Mohamed Omar Ali Bajaber, kutoka klabu ya Kenya Police FC, inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya.
Katika hatua inayodhihirisha dhamira ya klabu hiyo ya Wanajangwani kujijenga upya, Yanga pia inahusishwa na wachezaji wengine kama Jonathan Sowah wa Singida Black Stars na Jibril Sillah wa Azam FC.
Hata hivyo, jina la Mohamed Omar limeanza kuchukua nafasi kubwa katika mipango ya usajili ya Yanga, hasa kutokana na uwezo wake wa kucheza kama winga pande zote mbili na pia kama kiungo mshambuliaji.
Mohamed Omar, mwenye umri wa miaka 22, ni raia wa Kenya na pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Harambee Stars. Uwezo wake wa kucheza katika maeneo mbalimbali ya ushambuliaji umemfanya kuwa lulu inayowaniwa, si tu na Yanga, bali pia na klabu zingine katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Kenya, Yanga imeonyesha nia ya dhati ya kumnasa mchezaji huyo na huenda mazungumzo yakafikia hatua ya mwisho hivi karibuni, kwani inadaiwa kuwa Bajaber anaweza kusafiri kuja Tanzania muda wowote kwa ajili ya kukamilisha taratibu.
Uongozi wa Yanga pamoja na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Miloud Hamdi, linalenga kuongeza nguvu katika eneo la kiungo wa kushambulia kabla ya kuamua hatma ya Stephane Aziz Ki, ambaye anatabiriwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Katika mpango huo, Bajaber anaonekana kuwa chaguo sahihi la kujenga kikosi cha ushindani msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa zamani wa Kenya Police FC, Francis Baraza, ambaye kwa sasa anaifundisha Kakamega Home Boys, alithibitisha kuwepo kwa taarifa kwamba Yanga ipo katika mazungumzo ya kumsajili Bajaber.
“Ni taarifa ambazo zinazungumzwa sana huku kuwa kiungo huyo anafanya mazungumzo na moja ya timu Tanzania kwa ajili ya kujiunga nayo msimu ujao,” alisema Baraza.
Baraza aliongeza kuwa Bajaber ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, mwenye uwezo wa kucheza kama winga pande zote na kiungo wa kushambulia. Alisema aina ya uchezaji wake inaweza kuendana na kasi ya ligi ya Tanzania, hivyo ni chaguo sahihi kwa timu inayotafuta ushindi wa kitaifa na kimataifa.
Mbali na Bajaber, klabu hiyo pia ina mpango wa kusajili beki wa kati mmoja na kiungo mkabaji ambaye atasaidia kuziba pengo la Khalid Aucho, ambaye kwa sasa anakabiliwa na changamoto ya majeraha ya mara kwa mara, huku mkataba wake ukielekea ukingoni mwishoni mwa msimu huu.
Yanga inaonekana kuchukua tahadhari mapema kwa kuhakikisha kuwa mapungufu yote ya kikosi yanashughulikiwa kabla ya msimu mpya kuanza. Usajili wa mchezaji kama Bajaber unaweza kuwa chachu ya mafanikio mapya, hasa kwa kuzingatia umri wake mdogo na uwezo wa kucheza kwa kasi na ubunifu.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Fei Toto Aelezea Umuhimu wa Mechi Sita Zilizosalia Kwa Azam
- De Bruyne Atangaza Kuondoka Man city Mwishoni Mwa Msimu
- Ratiba Ya Robo Fainali Crdb Bank Federation Cup 2024/2025
- Simba Yaianza Robo Fainali Shirikisho CAF Kwa Kichapo Cha 2-0
- Matokeo ya Tabora united vs Yanga Leo 02/04/2025
- Kikosi cha Yanga VS Tabora united Leo 02/04/2025
- Viingilio Mechi ya Tabora united Vs Yanga SC Leo 02/04/2025
- Tabora United VS Yanga Leo 02/04/2025 Saa Ngapi?
- Real Madrid Yaweka Dau la Pauni Milioni 90 Kumnasa Bruno Fernandez
- Kagera Sugar Yagonga Mwamba Usajili wa George Mpole
Leave a Reply