Yaliyojiri Mkutano wa Waziri Kabudi na TFF, TPLB, Yanga na Simba

Yaliyojiri Mkutano wa Waziri Kabudi na TFF

Yaliyojiri Mkutano wa Waziri Kabudi na TFF, TPLB, Yanga na Simba

Baada ya kuahirishwa kwa mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya Yanga SC na Simba SC, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alikutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), pamoja na viongozi wa vilabu hivyo viwili ili kutafuta suluhisho la mgogoro huo.

Mashabiki wa soka nchini wameendelea kujiuliza iwapo mchezo huo utaendelea au la, hasa baada ya Yanga kushikilia msimamo wao wa kutocheza mechi nyingine dhidi ya Simba na badala yake kudai pointi tatu. Kikao hicho cha dharura kilifanyika Alhamisi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kikihusisha mazungumzo kati ya pande husika ili kupata suluhisho la sakata hilo.

Yaliyojiri Mkutano wa Waziri Kabudi na TFF, TPLB, Yanga na Simba

Yanga Yasalia na Msimamo Wake

Baada ya kikao hicho, uongozi wa Yanga SC ulitoka huku Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, akizungumza kwa kifupi na waandishi wa habari. Alieleza kuwa walipata fursa ya kueleza hoja zao mbele ya Waziri Kabudi na timu yake.

Kwa mujibu wa Hersi, Yanga ilieleza msimamo wao rasmi kuhusu mchezo huo, huku wakisisitiza kuwa wanatetea maslahi ya klabu yao na wanachama wake. Aliwataka mashabiki wa Yanga kuwa watulivu huku wakisubiri mwafaka wa suala hilo.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kikao zilionyesha kuwa Yanga hawakubadili msimamo wao – wanasimamia msimamo wa kutocheza mechi nyingine na wanadai pointi tatu za mchezo huo wa ligi. Waziri Kabudi alifafanua kuwa kikao hicho hakikuwa cha kufanya maamuzi bali kusikiliza pande zote kabla ya kuangalia uwezekano wa suluhu.

Mashabiki wa Yanga Waonyesha Hisia Zao

Baada ya kikao hicho, mashabiki wa Yanga waliokuwa nje ya uwanja walionekana kusubiri kwa hamu taarifa kutoka kwa viongozi wao. Walipomuona Injinia Hersi akitoka, waliimba na kushangilia huku wakisisitiza msimamo wao wa “hatuchezi.”

Simba Yapinga Kujadiliwa kwa Mchezo wa Dabi

Kwa upande wa Simba SC, viongozi wao walikutana na Waziri Kabudi baadaye na walitoka kikaoni bila kujadili suala la mechi hiyo. Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, alieleza kuwa kikao chao kilijikita zaidi kwenye maendeleo ya soka nchini na siyo mchezo wa Kariakoo Dabi.  Mangungu alisema kuwa klabu yake inaheshimu maamuzi ya mamlaka za soka na kwamba mchezo huo utapangiwa tarehe nyingine kama ilivyoelekezwa.

TFF na TPLB Wabaki Kimya

Baada ya kikao hicho, viongozi wa TFF na TPLB walitoka bila kutoa tamko rasmi. Rais wa TFF, Wallace Karia, na viongozi wenzake walikwepa kuzungumzia kikao hicho huku wakielekeza waandishi wa habari kusubiri tamko rasmi kutoka serikalini.

Serikali Yasalia Kimya

Licha ya kuwaita wadau wa soka katika kikao hicho, Waziri Kabudi na viongozi wa wizara hawakutoa tamko rasmi kuhusu hatma ya mchezo huo. Naibu Waziri wa Michezo, Hamis Mwinjuma, na Katibu wa Wizara, Gerson Msigwa, pia walikataa kuzungumza, wakisisitiza kuwa taarifa rasmi itatolewa baadaye.

Kwa sasa, bado haijafahamika hatma ya mchezo wa Kariakoo Dabi na iwapo uamuzi wowote utachukuliwa. Mashabiki wa soka nchini wanasubiri kwa hamu kujua iwapo Yanga itaendelea kushikilia msimamo wake au kama suluhisho litapatikana kupitia mazungumzo yanayoendelea.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. CAF Yaondoa Marufuku Uwanja wa Benjamin Mkapa
  2. Sowah Aweka Bayana Nia Yake Yakubeba Kiatu Cha Dhahabu
  3. Majeraha ya Goti Yamkosesha Alphonso Davies Mechi za Mwisho za Msimu
  4. Yanga Yavamia Dili la Fei Simba
  5. Silaha 6 Muhimu za Simba SC Zatangulizwa Misri
  6. Vita ya Top 4 Ligi Kuu Tanzania Bara Yapamba Moto
  7. Morocco Yaishushia Tanzania Kichapo cha 2-0, Mechi ya Kufuzu Kombe la Dunia 2026
  8. Safari ya Serengeti Boys Kuelekea Kombe la Dunia Yaanzia Morocco
  9. Kocha Taoussi Akiri Azam FC Kupitia Kipindi Kigumu, Ataka Utulivu
  10. Matokeo ya Morocco vs Tanzania Taifa Stars Leo 25/03/2025
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo