Wydad Bado Katika Harakati za Kumsajili Mzize

Wydad Bado Katika Harakati za Kumsajili Mzize

Klabu ya soka ya Wydad Casablanca ya Morocco inaendelea na jitihada zake za kumsajili mshambuliaji mahiri wa Yanga SC, Clement Mzize, ambaye aling’ara kwenye Kombe la FA msimu uliopita kwa kuwa mfungaji bora.

Mzize, mwenye umri wa miaka 20, amekuwa topiki kubwa kwenye soko la usajili hivi karibuni baada ya vilabu vikubwa kuwinda huduma yake, hii ni kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao alouonesha, jambo ambalo limevutia vilabu vikubwa barani Afrika.

Mzize ni zao la timu za vijana za Yanga, na mchango wake mkubwa kwa timu ya wakubwa umepelekea klabu kadhaa barani Afrika kumfukuzia kwa nia ya kumsajili. Miongoni mwa vilabu vinavyomwinda ni Wydad Casablanca na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Ushindani huu wa vilabu vikubwa ni ishara ya umahiri wa kijana huyo kwenye dimba la soka, huku Wydad wakiwa mstari wa mbele katika kutaka kupata huduma zake.

Wydad Yawasilisha Ofa ya Tatu kwa Yanga

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, Wydad Athletic imetuma ofa ya tatu kwa ajili ya kumsajili Clement Mzize, huku ikiwa imeongeza dau la usajili kufikia kiasi cha takribani Tsh Bilioni 1.4. Ofa hiyo, kulingana na makubaliano ya ziada, inaweza kufikia Tsh Bilioni 2.1, ikiwa Yanga watakubali masharti yaliyowekwa.

Wydad Bado Katika Harakati za Kumsajili Mzize

Taarifa kutoka vyombo vya habari vya Morocco zinaeleza kuwa uongozi wa Wydad unaamini kuwa ofa hiyo ni ya kuvutia, na wanatarajia kwamba Yanga itaafiki kumruhusu Mzize ajiunge nao. Aidha, Wydad imejipanga kuvutia Yanga zaidi kwa kutoa ofa ya kuandaa kambi ya maandalizi ya msimu mpya nchini Morocco, ambapo klabu hiyo itagharamia kila kitu kwa upande wa Yanga.

Hata hivyo, Yanga imeweka wazi kuwa haitamuuza mshambuliaji huyo chini ya dau la Tsh Bilioni 2.7. Msimamo huu wa Yanga unaonyesha umuhimu wa Mzize kwa timu hiyo, huku ikionekana kuwa uongozi unataka kuhakikisha kwamba wanapata thamani halisi ya mchezaji wao iwapo wataamua kumuachia.

Kocha wa Wydad, Rulani Mokoena, ambaye aliwahi kuinoa timu ya Mamelodi Sundowns, anaamini kwamba Mzize ataongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Mokoena amekuwa akifuatilia maendeleo ya mshambuliaji huyo kwa muda, na ana matumaini kuwa dili hili litakamilika hivi karibuni.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Kikosi cha Chelsea UEFA Conference League 2024/2025
  2. Bellingham Afuata Nyayo za Ronaldo, Aingia YouTube Rasmi
  3. Manchester United Yatangaza Kikosi cha Wachezaji 25 kwa Ajili ya Europa 2024-25
  4. Ufaransa Yashushiwa Kipigo cha Goli 3-1 na Itali
  5. Ronaldo Afunga Bao Lake 900, Aandikisha Historia Mpya
  6. “Kazini Kwangu Kuzito” – Sure Boy Aelezea Vita ya Kupambania Nafasi Yanga
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo