Wachezaji Saba Watimuliwa Zanzibar Kwa Tuhuma Za Kubeti
Uongozi wa klabu ya Junguni United, inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), umechukua hatua kali dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya michezo kwa kuwaondoa rasmi wachezaji saba waliobainika kujihusisha na shughuli za kubashiri matokeo ya mechi (betting). Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia tuhuma nzito za ushiriki wao katika michezo ya kubeti mechi mbili dhidi ya Malindi FC na New City FC.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu wa klabu hiyo, Suleiman Mwidani, wachezaji hao wamekiuka kwa makusudi Katiba ya Junguni United pamoja na Kanuni za Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2024/2025, hasa kifungu namba mbili na tatu, sura ya 23.
Kanuni hizo zinakataza mchezaji yeyote kushiriki katika michezo ya kubahatisha yanayohusiana na matokeo ya mechi, kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya michezo na kanuni za ushindani wa haki.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya uchunguzi wa kina kufanywa na uongozi wa klabu na kujiridhisha juu ya ushiriki wa wachezaji hao katika vitendo hivyo, hatua ya kuwasimamisha mara moja ilichukuliwa. Wachezaji hao wamezuiwa kushiriki shughuli yoyote ya timu, ikiwemo mazoezi, mechi na vikao vya kiufundi.
Wachezaji waliotimuliwa ni:
- Salum Athumani ‘Chubi’
- Ramadhan Ally Omar ‘Matuidi’
- Abdallah Sebastian
- Danford Mosses Kaswa
- Bakari Athumani ‘Jomba Jomba’
- Rashid Abdalla Njete
- Idd Said Karongo
Aidha, uongozi wa Junguni United umeiomba rasmi Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kuwachukulia hatua kali zaidi wachezaji hao, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukomesha tabia ya kubeti miongoni mwa wachezaji. Uongozi huo umetilia mkazo kuwa vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo ya soka visiwani Zanzibar na vinapaswa kudhibitiwa kwa njia ya kisheria.
Uongozi wa Junguni United umetumia tukio hili kutoa onyo kwa wachezaji wengine wote kuwa kujihusisha na michezo ya kubashiri matokeo ni kosa kubwa la kinidhamu. Sheria za mchezo wa soka kimataifa pia zinakataza tabia hiyo, na mara nyingi husababisha adhabu kali zikiwemo kufungiwa kucheza soka kwa muda mrefu au maisha.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Refa Mpya Apangwa Kuongoza Mechi ya Stellenbosch Dhidi ya Simba
- Ratiba ya Kombe la Muungano 2025
- Kikosi cha Simba Kitakachoivaa Stellenbosch Afrika Kusini April 27
- Timu Zinazoshiriki Kombe la Muungano 2025
- Yanga Yaishushia Fountain Gate Kichapo Cha 4-0 na Kuweka Rekodi
- Kikosi cha Yanga VS Fountain Gate Leo 21/04/2025
Leave a Reply