Ufaransa Yashushiwa Kipigo cha Goli 3-1 na Itali
Paris (AFP) – Timu ya taifa ya Italia imepata ushindi wa kishindo baada ya kurudi mchezoni na kuichapa Ufaransa kwa mabao 3-1 kwenye mechi ya UEFA Nations League iliyochezwa Paris, Ijumaa.
Mchezo huo ulianza kwa Ufaransa kufunga bao la mapema kupitia Bradley Barcola ndani ya sekunde 13, lakini Italia ilijibu mapigo kwa mabao ya Federico Dimarco, Davide Frattesi, na Giacomo Raspadori.
Bradley Barcola aliweka rekodi ya kufunga bao la haraka zaidi kwa mchezaji wa Ufaransa, lakini licha ya mwanzo huo mzuri, Ufaransa ilishindwa kudhibiti mchezo, na hatimaye Italia ikaondoka na ushindi wa haki.
Ushindi huu ni faraja kubwa kwa kikosi cha kocha Luciano Spalletti, hasa baada ya Italia kushindwa vibaya katika Euro 2024, walipotolewa na Uswizi kwenye hatua ya 16 bora. Huu ni mwanzo mzuri kwa Italia katika mashindano ya UEFA Nations League, ambapo sasa wanashikilia nafasi ya juu katika kundi A2 wakiwa sawa na Ubelgiji, ambao pia waliifunga Israel 3-1 kwenye mechi nyingine ya kundi hilo.
Italia inatarajia kukutana na Israel katika mchezo wao ujao Jumatatu, huku mchezo huo ukichezwa Budapest kutokana na hali ya usalama ya Mashariki ya Kati.
Kwa upande mwingine, Ufaransa ikiongozwa na nahodha Kylian Mbappe, ilionekana kutatizika katika mchezo huu, huku Mbappe akishindwa kuonyesha makali yake. Kocha Didier Deschamps anatarajiwa kuboresha kikosi chake ili kukabiliana na Ubelgiji kwenye mchezo ujao jijini Lyon. Mchezo huo unatarajiwa kuwa marudio ya mechi ya hatua ya 16 bora ya Euro 2024, ambapo Ufaransa iliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ubelgiji.
Katika mchezo huu, Didier Deschamps alimpa nafasi ya kwanza ya kucheza katika kikosi cha wakubwa Michael Olise, winga wa Bayern Munich ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliong’ara katika kikosi cha Ufaransa kilichoshinda medali ya fedha kwenye Michezo ya Olimpiki mwezi uliopita. Barcola, ambaye ni mchezaji wa klabu ya Paris Saint-Germain, alipata nafasi ya kuanza pia, na hakupoteza muda kuacha alama yake.
Italia ilianza kwa mpira, lakini Barcola alifanya pressing ya hali ya juu na kufanikiwa kumwibia mpira Giovanni Di Lorenzo kabla ya kukimbia moja kwa moja na kufunga bao. Bao hilo lilifungwa ndani ya sekunde 13, likiwa ni goli la haraka zaidi kufungwa na mchezaji wa Ufaransa katika historia ya mechi za kimataifa, likipiku rekodi ya sekunde 38 iliyowekwa na Bernard Lacombe dhidi ya Italia katika Kombe la Dunia la mwaka 1978.
Hata hivyo, Italia haikukata tamaa. Walikaribia kusawazisha dakika ya sita, lakini kichwa cha Davide Frattesi kiligonga mwamba. Walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 30 kupitia goli safi lililofungwa na Federico Dimarco.
Dimarco alipokea mpira kutoka kwa Andrea Cambiaso, akaurudisha kwa Sandro Tonali ambaye alimrudishia mpira huo, na kwa ustadi wa hali ya juu, Dimarco alifunga kwa shuti la kwanza lililoingia juu kwenye kona ya mbali ya goli.
Italia iliongeza bao la pili dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza. Davide Frattesi alifanikiwa kuingilia kati pasi mbaya ya Youssouf Fofana na kuanzisha shambulizi kali. Frattesi alikimbia hadi kwenye eneo la hatari na kupokea pasi ya Mateo Retegui kabla ya kufunga bao la pili.
Ufaransa ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Michael Olise na kumuingiza Ousmane Dembele. Pia, Manu Kone aliingia dimbani kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa, lakini bado Ufaransa ilishindwa kudhibiti Italia, ambao walionekana kuwa bora zaidi.
Dakika ya 74, Italia ilifunga bao la tatu kupitia Giacomo Raspadori. Raspadori alipokea mpira kutoka kwa mchezaji mwenzake, Destiny Udogie, na kwa haraka alimzidi William Saliba na kufunga bao lililohitimisha ushindi wa Italia.
Ufaransa ilijaribu kurudi mchezoni, lakini walishindwa kupata mwanya wa kurudisha mabao, na hatimaye filimbi ya mwisho ilipigwa huku mashabiki wa nyumbani wakiwa na hisia mchanganyiko, wengine wakipiga filimbi na wengine wakiwa na utulivu wa kutoridhishwa.
Mapendekezo ya Mhariri:
Leave a Reply