Nafasi Mpya za Kujiunga JKT 2024 Zatangazwa
Dodoma, Tanzania – Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza nafasi mpya za kujiunga na mafunzo ya kujitolea kwa mwaka 2024. Nafasi hizi ni kwa vijana wote wa Tanzania Bara na Zanzibar na lengo ni kuwajengea uzalendo, umoja wa kitaifa, na kuwaandaa kwa stadi za maisha na kazi. Usajili utaanza rasmi tarehe 1 Oktoba 2024, ambapo vijana waliohitimu elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu, na wale wenye shahada ya uzamili wanakaribishwa kuomba. Hii ni fursa kubwa kwa vijana wa Kitanzania kujifunza na kuchangia katika ujenzi wa taifa.
Tangazo hili limetolewa na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Kanali Juma Mrai, kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kanali Mrai alieleza kuwa nafasi hizi za mafunzo ni kwa lengo la kuwajengea vijana uzalendo, ukakamavu, umoja wa kitaifa, na kuwapa ujuzi mbalimbali wa kazi na maisha kwa jumla.
Utaratibu wa Kutuma Maombi ya Kujiunga JKT Septemba 2024
Vijana wanaotaka kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mwaka 2024 wanapaswa kufuata utaratibu uliowekwa, ambapo maombi yao yatasimamiwa na ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya ambako waombaji wanaishi. Hii ina maana kuwa vijana wanatakiwa kuwasilisha maombi yao katika ofisi hizi, zikisaidiwa na wataalamu walioko katika mikoa na wilaya husika.
Mafunzo ya kujitolea ya JKT yana lengo la kutoa stadi muhimu kwa vijana ili waweze kujiajiri baada ya kumaliza mkataba wao na JKT. Ingawa JKT inatoa mafunzo haya kwa nia njema, Kanali Mrai alibainisha kuwa jeshi hilo halihusiki na utoaji wa ajira, wala halina wajibu wa kuwatafutia vijana kazi katika vyombo vya ulinzi na usalama au mashirika mengine.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, vijana watakaoteuliwa kwa ajili ya mafunzo haya watatakiwa kuripoti katika kambi za JKT kuanzia Novemba 1 hadi 3, 2024.
Sifa za Mwombaji na Maelekezo Muhimu
Ili kujiunga na mafunzo haya, vijana wanapaswa kuwa na sifa zinazotakiwa na JKT. Sifa hizi zimeainishwa kwa kina katika tovuti rasmi ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz. Aidha, tovuti hiyo pia inatoa maelekezo ya vifaa vinavyohitajika wakati wa kujiunga na mafunzo.
Ili kujiunga na mafunzo ya JKT, muombaji wa nafasi mpya za kujiunga JKT 2024 anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:
- Awe raia wa Tanzania.
- Awe na umri unaokubalika kulingana na kiwango cha elimu alichomaliza:
- Waliomaliza elimu ya msingi: Umri wa miaka 16-18.
- Waliomaliza elimu ya sekondari: Umri usiozidi miaka 20.
- Waliomaliza elimu ya kidato cha sita: Umri usiozidi miaka 22.
- Wenye stashahada: Umri usiozidi miaka 25.
- Wenye shahada: Umri usiozidi miaka 26.
- Wenye shahada ya uzamili: Umri usiozidi miaka 27.
- Awe na afya njema na akili timamu.
- Asiwe na alama yoyote ya mwilini (tattoo) na asiwe na rekodi ya uhalifu.
- Awe na cheti halisi cha kuzaliwa pamoja na Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA.
- Asiwe amewahi kutumikia idara yoyote ya ulinzi au kuajiriwa katika taasisi za Serikali au zisizo za Serikali.
Vilevile, mafunzo haya ni bure, na hakuna ada au gharama zinazohusishwa kwa vijana wanaokidhi vigezo vilivyowekwa. Kanali Mrai alisisitiza kuwa JKT halihusiki na matukio yoyote ya utapeli yanayohusiana na nafasi hizi, na wazazi pamoja na walezi wanapaswa kuwa makini na wale wanaotumia mwanya huu kuwalaghai fedha kwa ahadi za uwongo za kuwasaidia vijana kujiunga na mafunzo ya JKT.
Vifaa Muhimu vya Kubeba Kwa Watakaochaguliwa Kujiunga JKT
Vijana watakaoteuliwa kujiunga na mafunzo ya JKT wanapaswa kuwa na vifaa maalum vya matumizi katika kambi. Baadhi ya vifaa hivyo ni:
- Bukta yenye rangi ya bluu yenye mpira kiunoni.
- Raba za michezo zenye rangi ya kijani au bluu.
- Shuka mbili za rangi ya bluu bahari.
- Soksi ndefu za rangi nyeusi.
- Vazi la kuzuia baridi kwa waliopewa kambi za mikoa ya baridi.
- Fulana ya kijani kibichi isiyo na maandishi.
Kwa vijana wa kike, wanapaswa kuvaa bukta yenye mpira kiunoni na kwenye pindo za miguu.
Faida za Kujitolea Mafunzo ya JKT
Mafunzo haya ya JKT yanawalenga vijana kwa lengo la kuwajengea misingi thabiti ya uzalendo, nidhamu, na ukakamavu. Mbali na hayo, vijana pia watajifunza stadi za maisha na kazi ambazo zitawawezesha kujiajiri mara baada ya kumaliza mkataba wao wa JKT.
Ni muhimu kufahamu kuwa JKT haihusiki moja kwa moja na utoaji wa ajira, bali hutoa mafunzo ambayo yatamsaidia kijana kutumia ujuzi aliojifunza kujitegemea kimaisha.
Onyo Dhidi ya Utapeli
Jeshi la Kujenga Taifa limeonya dhidi ya utapeli unaohusisha kutoa fedha kwa ahadi ya kupata nafasi hizi. Nafasi za kujiunga na mafunzo ya JKT ni bure na hazitolewi kwa malipo. Jeshi la Kujenga Taifa halitahusika kwa namna yoyote ile ikiwa mzazi au mlezi atatapeliwa kwa kutoa fedha ili mwanawe apate nafasi ya kujiunga na mafunzo haya.
Kwa maelezo zaidi kuhusu sifa, maelekezo, na jinsi ya kujiandikisha, vijana wanashauriwa kutembelea tovuti rasmi ya JKT www.jkt.go.tz.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Majina ya Waliochaguliwa Kujiunga na Jeshi la Polisi 2024
- Orodha ya Vijana 3500 Waliochaguliwa Kujiunga Jeshi la Polisi Tanzania 2024 Yatangazwa
- Majina ya Walioitwa Kwenye Usaili jeshi la Polisi 2024
- Majina ya Walioitwa kwenye Usaili Ajira Portal 2024
- Taarifa Muhimu kwa Waombaji Kazi za Ualimu AJira Portal 14 September 2024
- Nafasi Mpya za Kazi Ajira Portal September 2024
Leave a Reply