Msigwa Afunguka Kuhusu Ukarabati wa Uwanja wa Mkapa
Baada ya kutokea kwa kasoro katika eneo la kuchezea (pitch) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amefafanua kuwa eneo hili halikuwa sehemu ya ukarabati unaoendelea kwa sasa. Msigwa alieleza kuwa uwanja huo ulifanyiwa ukarabati mwaka 2023 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili kuwa tayari kwa ajili ya michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), ambapo ukarabati huu ulipaswa kudumu kwa kipindi cha miaka miwili.
Hata hivyo, baada ya ukaguzi wa uwanja uliofanywa na CAF, uwanja huo ulifungiwa kwa muda kutokana na kasoro zilizobainika katika eneo la kuchezea, mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Azam, iliyochezwa Februari 24, 2025.
Tofauti na ilivyokuwa awali, uwanja ulifunguliwa tena ili kutoa nafasi kwa mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na Al Masry, iliyochezwa Aprili 9, 2025. Lakini, changamoto mpya zilijitokeza, ambapo eneo la kuchezea lilionekana kujaa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha siku ya mchezo huo, na hivyo kulazimu uwanja huo kufungwa tena.
Akizungumza katika warsha ya wadau wa Utamaduni na Sanaa tarehe 17 Aprili 2025, Msigwa alithibitisha kuwa changamoto inayoukumba uwanja huo ni kutokana na uwezo mdogo wa eneo la kuchezea kuondoa maji kwa haraka, na sio kwamba maji hayawezi kuondolewa kabisa. Ili kutatua changamoto hii, serikali imeleta wataalamu kutoka Uturuki, ambao wataungana na wataalamu wa ndani ili kufanya marekebisho muhimu kwa haraka na kuhakikisha uwanja unakuwa katika hali nzuri kwa ajili ya michuano ya kimataifa inayokuja.
Kwa upande mwingine, Msigwa alieleza kuwa CAF ilifanya ukarabati wa eneo la kuchezea kwa ajili ya michuano ya CHAN 2024, ambayo awali ilikuwa ifanyike Septemba 2024 lakini ikasogezwa mbele hadi Februari 2025, na sasa imesogezwa hadi Agosti 2025.
Hata hivyo, aliongeza kuwa baada ya michuano hiyo, serikali itafanya matengenezo makubwa zaidi ya uwanja, ikiwa ni pamoja na kuondoa sehemu ya juu ya eneo la kuchezea na kupanda nyasi mpya.
Pia, Msigwa alieleza kuwa ifikapo mwisho wa mwezi Aprili 2025, uwekaji wa viti utakamilika, ambapo makubaliano ya serikali na mkandarasi yanataka viti 62,000 kuwekwa kwenye uwanja. Kwa sasa, viti 40,000 tayari vimefika, na kazi inaendelea, ambapo tayari viti 20,000 vimewekwa, na ukarabati wa uwanja umefikia asilimia 80.
Viti vitakapokamilika, vitakuwa na rangi inayoshabihiana na bendera ya Taifa, na sehemu ya zege pia itapambwa kwa ‘material’ maalum, ili kuongeza uzuri na mvuto wa uwanja. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha uwanja wa Mkapa unakuwa na hadhi ya kimataifa, na unaendana na viwango vya CAF na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Hadi sasa, serikali inaendelea na juhudi za kuboresha uwanja wa Mkapa, na imedhamiria kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza katika uwanja huo zinatatuliwa kwa haraka, ili uweze kutumika katika michuano ya kimataifa ya hivi karibuni.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Polisi Tanzania Yajipanga Kulpa Kisasi Dhidi ya Mbeya City Babati
- Ifahamu Jayrutty Investment Company Limited, Mdhamini Mpya wa Simba
- Wafungaji Bora CRDB Bank Federation Cup 2024/2025
- Timu Zilizofuzu Nusu Fainali Klabu bingwa UEFA Champions 2024/2025
- Simba SC Yasaini Mkataba Mnono wa Vifaa vya Michezo
- Ratiba ya CRDB Federation Cup Fixtures 2024/2025
- Vilabu Bora Afrika 2024/2025 (CAF Club Ranking)
- Matokeo ya Yanga vs Stand United Leo 15/04/2025
Leave a Reply