Mpanzu na Kibu Wamtia Hofu Kocha wa Stellenbosch
KOCHA wa Stellenbosch FC, Steve Barker, ameanza kuingiwa ubaridi mkubwa kabla ya pambano lao kali dhidi ya Simba SC katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, akiwataja Kibu na Elie Mpanzu kuwa ndio chanzo kikuu cha wasiwasi wake kuelekea mchezo huo mgumu.
Kwa mujibu wa takwimu za msimu huu, Simba SC imekuwa ikitumia vyema Uwanja wa Benjamin Mkapa kama ngome yao isiyotikisika, hasa katika michezo ya kimataifa. Hadi kufikia hatua hii ya mashindano, Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakifunga wastani wa mabao mawili au zaidi kila walipocheza nyumbani tangu hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hali hiyo imeifanya Stellenbosch kutambua wazi ukubwa wa kazi waliyo nayo mbele ya mashabiki wa Simba, ambao wamekuwa kama mchezaji wa 12 kila timu yao inaposhuka dimbani.
Akizungumza baada ya kuwatoa Zamalek ya Misri – mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika – Steve Barker alikiri kuwa na kazi nzito zaidi sasa, akieleza kuwa Simba ni timu yenye historia na uzoefu mkubwa barani Afrika. Aliongeza kuwa Kibu Denis na Elie Mpanzu ni wachezaji wanaomletea hofu kubwa kutokana na uwezo wao wa kipekee.
“Simba ni timu yenye uzoefu mkubwa wa michuano ya Afrika na wana wachezaji hatari ambao wakipata nafasi, wanakuadhibu. Mpanzu ni mshambuliaji wa kiwango cha juu, pamoja na Kibu. Ana kasi, anacheza kwa nguvu hilo tunalitambua,” alisema Barker kwa sauti iliyojaa tahadhari.
Kibu Denis Mkandaji
Mshambuliaji wa Simba SC, Kibu Denis, amekuwa miongoni mwa nyota wanaoangaza katika kikosi hicho msimu huu.
Hadi sasa, ana mabao matatu katika mashindano haya, mabao mawili tu nyuma ya kinara wa mabao – Ismail Belkacemi wa USM Alger ambaye tayari timu yake imetolewa mashindanoni. Hii inamuweka Kibu katika nafasi nzuri ya kushindania Kiatu cha Dhahabu, huku akiwa na mechi muhimu dhidi ya Stellenbosch kumwongezea nafasi zaidi.
Mbali na uwezo wake wa kufunga, kasi yake na nguvu za kimwili zimekuwa tatizo kwa mabeki wengi barani Afrika, jambo ambalo limemlazimu kocha wa Stellenbosch kumtambua mapema kama mchezaji wa kipekee wa kuangaliwa kwa karibu.
Elie Mpanzu: Silaha Nyingine Hatari ya Simba
Mbali na Kibu, Elie Mpanzu ameonekana kuwa chachu ya mafanikio ya Simba katika hatua hii ya mtoano. Uwezo wake wa kucheza kama mshambuliaji wa kisasa – akichanganya nguvu, akili na ustadi wa kumalizia – umeongeza hofu kwa Stellenbosch.
Mpanzu amepewa sifa kama mchezaji wa kiwango cha juu na mwenye uwezo wa kubadili matokeo muda wowote ule, hasa akiwa nyumbani mbele ya maelfu ya mashabiki wa Msimbazi.
Benjamin Mkapa: Machinjio kwa Wageni
Kocha Barker hakuficha hofu yake juu ya mazingira ya kucheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao ameutaja kuwa na presha kubwa kwa wachezaji wake kutokana na idadi na nguvu ya mashabiki wa Simba.
“Hatupaswi kuingia uwanjani kwa kujiamini kupita kiasi. Tunapaswa kuwa makini, kupunguza makosa na kuamini katika mipango yetu ya kiufundi. Tunajua Benjamini Mkapa ni moto lakini nusu fainali inahitaji roho ya chuma,” aliongeza kwa msisitizo.
Simba wanakuja katika mechi hii wakiwa na ari na morali ya juu baada ya kutinga nusu fainali kwa kuiondosha Al Masry ya Misri kwa mikwaju ya penalti 4-1, kufuatia kusawazisha mabao 2-0 waliyoruhusu kwenye mchezo wa kwanza. Huu ni ushahidi wa ukomavu wa kikosi cha Simba katika hatua za mtoano na uthibitisho kuwa timu hiyo imeiva kwa mafanikio makubwa barani Afrika.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Simba Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Afrika
- Kikosi cha Yanga vs Azam Leo 10/04/2025
- Azam vs Yanga Leo 10/04/2025 Saa Ngapi
- Mikwaju ya Penati Yaipeleka Simba Nusu Fainali Kombe la Shirikisho CAF
- Vituo Vya Kununua Tiketi za Mechi ya Simba VS Al Masry 09/04/2025
- Viingilio Mechi ya Simba VS Al Masry 09/04/2025
- Al Masry Yawasili Dar Kwa Ajili ya Simba – Robo Fainali Kombe la Shirikisho CAF
Leave a Reply