Moto Utawaka Msimu wa Ligi ya Championship 2024/2025

Moto Utawaka Msimu wa Ligi ya Championship 2024/2025

Msimu mpya wa Ligi ya Championship 2024/2025 unakaribia kuanza, na kama ilivyo ada, mashabiki wa soka nchini Tanzania wanatarajia burudani kubwa kutoka kwenye ligi hii inayozidi kuimarika. Ligi hiyo itashirikisha timu 16, zikiwa tayari kuanza rasmi mapambano ya kuwania kupanda Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2025/2026. Huu ni msimu unaosubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na timu nyingi zinazoshiriki, pamoja na ushindani mkali uliopo.

Ligi ya Championship imekuwa ikipanda kwa ubora kila msimu, ikitoa changamoto mpya kwa timu zinazotaka kufikia hatua ya kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Mbio za kupanda daraja haziwezi kutabirika kirahisi, tofauti na Ligi Kuu ambako mara nyingi ni rahisi kutabiri ni timu gani zitamaliza nafasi za juu.

Msimu wa 2023/2024 ulikuwa na mvutano mkubwa ambapo mpaka mechi ya mwisho ndipo zilipobainika timu zilizopanda daraja. Hali hii inatarajiwa kuendelea msimu huu mpya, huku timu zote zikijipanga vilivyo kuhakikisha zinasalia au zinapanda.

Moto Utawaka Msimu wa Ligi ya Championship 2024/2025

Timu Zinazotarajiwa Kuwasha Moto

Timu zilizoshuka daraja kutoka Ligi Kuu, kama Mtibwa Sugar na Geita Gold, zinajipanga upya kurejea kwenye ligi hiyo. Zote zimefanya usajili wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa, wakitarajia kutumia nafasi hii kurejea Ligi Kuu.

Mtibwa Sugar, moja ya timu kongwe nchini, ilijipatia umaarufu kupitia ushiriki wake wa muda mrefu Ligi Kuu, lakini sasa inahitaji kujipanga upya baada ya kushuka daraja. Aidha, Geita Gold imeimarisha kikosi chake, ikiwa na mastaa kama Fabrice Kayembe kutoka DR Congo na wengineo wenye nia ya kuirejesha timu kwenye ramani ya soka la juu nchini.

Ligi ya Championship haitakuwa rahisi kwa timu hizi kongwe, kwani timu nyingine 14 zimejipanga pia kuonesha uwezo wao. Mbali na usajili wa wachezaji wapya, timu hizi zimeimarisha mabenchi yao ya ufundi, hali inayoleta ushindani wa aina yake.

Kwa mfano, Mtibwa Sugar imeleta kocha mpya raia wa Marekani, Melis Medo, anayetarajiwa kupambana na makocha wenye uzoefu mkubwa wa ligi hiyo kama Amani Josiah na Mohammed Kijuso.

Wachezaji Nyota

Msimu huu wa 2024/2025 utashuhudia mastaa waliowahi kuwika kwenye Ligi Kuu wakiongoza vikosi vya timu za Championship. Kwa mfano, Mtibwa Sugar inawategemea wachezaji kama Anuary Jabir, Issa Rashid maarufu kama ‘Baba Ubaya’, pamoja na Amani Kyata. Hali kadhalika, Geita Gold imejipatia huduma ya wachezaji wenye uwezo kama Aaron Kalambo, Frank Magingi, na Abdulaziz Makame, ambao wanatarajiwa kuongeza nguvu katika harakati za kupanda daraja.

Kuwepo kwa wachezaji wenye uzoefu na vipaji vikubwa kunazidisha mvuto wa ligi hii, na mashabiki wanatarajia kuona burudani kubwa kutoka kwa mastaa hao wanaotafuta kurejesha makali yao kwenye soka la Tanzania.

Ushindani wa Kiwango cha Juu na Tahadhari

Msimu huu, ligi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa ambapo kila timu inahitaji kuonyesha ubora wake ili kuepuka kupoteza michezo muhimu. Hali hii inafanya kila mechi kuwa na mvuto wa aina yake, huku timu kama Geita Gold na Mtibwa Sugar zikihitajika kuchukua tahadhari kubwa ili kuepuka kuangukia pua kama ilivyotokea kwa timu kama Biashara United na Ruvu Shooting, ambazo zilishuka daraja na mpaka sasa hazijarudi tena Ligi Kuu.

Timu mpya kwenye ligi hii zinapaswa kuwa makini, kwani hakuna nafasi ya kuzubaa. Kila timu inacheza kwa tahadhari kubwa na kuleta mshangao baada ya dakika 90 za mchezo.

Vita ya Makocha

Mbali na wachezaji, ligi ya Championship pia itashuhudia vita ya makocha. Msimu huu utakuwa na makocha wakongwe kama Mohammed Kijuso na Ivo Mapunda, ambao watakuwa wakichuana na Melis Medo wa Mtibwa Sugar. Kila kocha anapambana kuonesha uwezo wake na kuhakikisha anaiwezesha timu yake kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Timu za Kuzifuatilia

Timu kama Biashara United, Mbeya Kwanza, na Songea United zinatarajiwa kuwa miongoni mwa zile zitakazofuatiliwa zaidi msimu huu. Timu hizi zimeonyesha ubora wao katika misimu iliyopita na zinajipanga kuhakikisha zinarejea Ligi Kuu Bara. Pia, timu kama TMA Stars na Polisi Tanzania zinaonekana kuwa na usajili mzuri, hali inayotarajiwa kuongeza ladha ya ushindani kwenye ligi.

Dabi za Kuvutia

Msimu wa 2024/2025 pia utashuhudia dabi kadhaa zinazotarajiwa kuongeza hamasa ya mashabiki. Dabi za Kanda ya Ziwa kati ya Geita Gold na Biashara United zinatarajiwa kuwa kali, huku pia zikiwa na msisimko wa kipekee. Vilevile, kuna dabi za jeshi kati ya TMA Stars, Polisi Tanzania, na Green Warriors, pamoja na dabi za Arusha kati ya TMA Stars na Mbuni FC.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Taifa Stars Yasafiri Kuelekea Yamoussoukro Kukabiliana na Guinea
  2. Yanga Kuvaana na CBE Sept 14, Gamondi Aanza Maandalizi Mapema
  3. Kocha Paul Nkata Ajipanga Upya Baada ya Mwanzo Mbaya Ligi Kuu
  4. Simba yaeka Marengo Ya CAF, Mo Dewji Arejea Kuongoza Mikakati
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo