Kilicho iponza Yanga Dhidi ya Azam Fc
Kwenye moja kati ya mechi zenye ushindani mkubwa huku timu zote zikishambuliana kwa awamu, mabingwa watetezi Yanga SC walishindwa kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2024/2025 baada ya kulazwa chuma moja bila kufurukuta na Azam FC. Timu hiyo kutoka Chamazi, maarufu kama Wanambarambamba, ilijipanga vema na kuweka juhudi kuhakikisha kuwa mchezo huo wa kukata na shoka unaenda vyema kwa upande wao.
Mkosi kwa Yanga sc ulianza mapema dakika ya 21 baada ya beki wa Yanga, Ibrahim Bacca, kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumuangusha mshambuliaji wa Azam FC, Nassoro Saadun, aliyekuwa anakwenda moja kwa moja langoni.
Mwamuzi Ahmed Arajiga, ambaye ni mshindi wa tuzo ya mwamuzi bora wa msimu uliopita, hakusita kutoa uamuzi huo mgumu, ambao uliwafanya Yanga kuanza mchezo kwa kucheza pungufu.
Wakati akitoka nje, Bacca aliwaomba radhi mashabiki wa yanga, ishara ya kukubali kosa lake na kujutia athari iliyosababishwa. Kuondoka kwake mapema uwanjani kulifanya Yanga SC kupoteza utulivu wa kiufundi na kutoa nafasi kwa Azam FC kuchukua udhibiti wa mchezo.
Bao la Djibril Sillah: Pigo Liliozamisha Yanga
Azam FC, ikitumia nafasi yao ya kucheza wakiwa kamili, walifungua ukurasa wa mabao kupitia shuti kali la Djibril Sillah dakika ya 33.
Sillah, ambaye amekuwa tishio kwa mabingwa hao mara kadhaa, alipokea pasi safi kutoka kwa kiungo Adolf Mutasingwa na kufanikiwa kuutuma mpira kimiani.
Hili lilikuwa bao la tatu kwa Sillah dhidi ya Yanga tangu asajiliwe Azam, na alionyesha kuwa ni mchezaji hatari kwa timu hiyo ya Jangwani. Mara ya mwisho kuwakabili, Sillah aliifunga Yanga mabao katika michezo miwili tofauti, ikiwemo bao moja kwenye ushindi wa 2-1 Machi 2024, na matokeo haya yanaonesha uwezo wake wa kuathiri rekodi nzuri za wapinzani.
Azam FC na Rekodi za Yanga: Wanarambaramba Waendeleza Ubabe
Kabla ya mchezo huo, Yanga walikuwa na rekodi ya kucheza zaidi ya michezo 50 nyumbani bila kupoteza tangu msimu uliopita na walikuwa hawajaruhusu bao lolote kwenye mechi nane za mwanzo wa msimu huu. Hata hivyo, Azam kwa mara nyingine walifanikiwa kuzuia rekodi hii, wakijidhihirisha kuwa ni miongoni mwa timu chache zinazoweza kuvunja ngome ya mabingwa hao watetezi.
Aidha, Azam wamekuwa na historia ya kuwa na ufanisi dhidi ya Yanga, ambapo Aprili 2021 waliizuia pia Yanga baada ya kucheza mechi 17 nyumbani bila kupoteza. Azam waliendeleza rekodi hii ya kuvunja rekodi za Yanga, na kwa mara nyingine wamethibitisha kuwa wao ni wapinzani wa kweli kwenye Ligi Kuu Tanzania.
Mabadiliko kwenye Msimamo wa Ligi na Matumaini ya Yanga
Matokeo ya mchezo huu yamewaweka Yanga kwenye presha ya kusalia na pointi 24, huku timu kama Singida BS zikiongeza ushindani kwenye msimamo wa ligi. Hali hii inaashiria kuwa Yanga itahitaji kujipanga upya ili kuendelea na mashindano kwa mafanikio.
Mapendekezo ya Mhariri:
Leave a Reply