Kikosi cha Al Ahli Tripoli Chawasili na Bodyguards Kibao Airport

Kikosi cha Al Ahli Tripoli Chawasili na Bodyguards Kibao Airport

Klabu ya Al Ahli Tripoli, imewasili jijini Dar es Salaam mapema leo ikiwa imeambatana na idadi kubwa ya walinzi binafsi bodyguards, hatua iliyozua mjadala mzito miongoni mwa mashabiki wa soka Tanzania.

Kikosi hiki kimewasili kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Simba SC, utakaochezwa Jumapili, Septemba 22, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ukiwa ni wa hatua ya kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).

Kikosi cha Al Ahli Tripoli Chawasili na Bodyguards Kibao Airport

Kuwasili kwa kikosi hiki kumefuatana na hali ya tahadhari isiyo ya kawaida, kwani klabu hiyo imekodi walinzi binafsi kwa ajili ya kuwalinda wachezaji, benchi la ufundi, na viongozi wao mara tu walipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam. Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, walinzi hao wameajiriwa kutokana na hofu ya usalama inayotokana na matukio yaliyotokea kwenye mchezo wa awali kati ya Simba na Al Ahli Tripoli nchini Libya, ambao ulimalizika kwa sare ya 0-0.

Mmoja wa watu waliokuja kuwapokea uwanjani, ambaye alikataa kutaja jina lake, alisema kuwa klabu ya Al Ahli Tripoli imejipanga vizuri kiusalama ili kuepuka fujo au shambulio lolote wakati wa kujiandaa kwa mchezo huo muhimu. Alisema, “Jamaa wanaogopa kutokana na yaliyotokea kule kwao, hata hapa tulipo hatujaambiwa wanafikia hoteli gani, hadi wafike ndio tutajua.”

Matukio ya Fujo Nchini Libya

Taarifa za matukio ya fujo baada ya mchezo wa awali nchini Libya zilitawala vichwa vya habari. Katika mchezo huo, mashabiki wa Al Ahli Tripoli waliripotiwa kuwafanyia fujo wachezaji wa Simba SC mara baada ya mpira kumalizika.

Inasemekana mashabiki hao walijaribu kuwazonga wachezaji wa Simba wakati wakiwa njiani kuelekea vyumbani. Pia, kipa wa Simba, Aishi Manula, aliripotiwa kupigwa na mmoja wa maofisa wa usalama waliokuwa wakisimamia mchezo huo.

Mbali na tukio hilo la kumshambulia kipa Manula, iliripotiwa pia kwamba wachezaji wa Al Ahli Tripoli walihusika katika kumshambulia mmoja wa waamuzi wa mchezo huo, jambo lililoleta sintofahamu kubwa. Hii ndiyo sababu kuu iliyosababisha uongozi wa klabu hiyo kuamua kuchukua tahadhari kali za kiusalama wakati wa safari yao ya Dar es Salaam.

Matarajio ya Mchezo wa Marudiano

Mchezo wa marudiano kati ya Simba na Al Ahli Tripoli unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hasa baada ya matokeo ya sare ya 0-0 katika mchezo wa kwanza. Timu zote mbili zinahitaji ushindi ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, na presha kwa pande zote mbili inatarajiwa kuwa kubwa. Uwanja wa Benjamin Mkapa unatarajiwa kujaa mashabiki wengi wa Simba, ambao watakuwa wakiiunga mkono timu yao kuhakikisha inapata matokeo mazuri nyumbani.

Al Ahli Tripoli, kwa upande wao, wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri licha ya changamoto za kiusalama walizokumbana nazo. Kuwasili kwao wakiwa na walinzi binafsi ni ishara ya umakini mkubwa unaowekwa na klabu hiyo kuelekea mchezo huo muhimu.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Mtasingwa Afunguka Kwanini Aliitosa Yanga
  2. Ishu ya Joshua Mutale na Jezi ya Kombe la Shirikisho CAF
  3. Refa Asiye na Uzoefu Kuchezesha Mtanange wa Simba vs Al Ahli Tripoli
  4. Elie Mpanzu Kwenye Rada za Yanga na Simba
  5. Yanga Yafanya ‘Homework’ ya Kutosha, Gamondi Apania Tiketi ya Makundi
  6. Fadlu Davids Afurahishwa na Ngome ya Ulinzi Simba
  7. Zahera Aanza Tambo Baada ya Ushindi wa Kwanza wa Namungo Ligi Kuu
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo