Jinsi ya kuomba mkopo kwa wanafunzi wa diploma 2024/2025 | Mwongozo wa Kuomba Mkopo Diploma
Elimu ya diploma ina nafasi kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania na maendeleo ya jamii. Vijana wanaomaliza masomo ya diploma wanakuwa na ujuzi unaohitajika sana katika sekta mbalimbali, kuanzia afya, biashara, hadi teknolojia. Hata hivyo, gharama za masomo zinaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi wengi wenye ndoto za kutimiza malengo yao ya elimu.
Kupitia mikopo ya elimu ya juu, Serikali ya Tanzania inatoa fursa kwa vijana kupata elimu wanayostahili bila kujali hali zao za kiuchumi. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ndiyo taasisi kuu inayosimamia utoaji wa mikopo hii.
Mwaka wa masomo 2024/2025 unakaribia, na wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vya elimu ya juu wanashauriwa kuchunguza fursa za kupata mikopo ili kufadhili masomo yao. Makala haya yanatoa mwongozo wa kina kuhusu jinsi ya kuomba mkopo wa HESLB kwa wanafunzi wa diploma, kuanzia vigezo vya kuzingatiwa hadi hatua za mwisho za kuwasilisha maombi.
Tutaangazia kwa undani vigezo vya ustahiki, mchakato wa maombi, taratibu za ulipaji, na vidokezo muhimu vya kuongeza nafasi ya kupata mkopo. Tunatumaini kuwa makala haya yatakuwa mwongozo muhimu kwa wanafunzi wote wanaotafuta njia ya kutimiza ndoto zao za elimu.
Vigezo vya Kuomba Mkopo kwa Wanafunzi wa Diploma
Ili kutuma maombi ya mkopo wa HESLB kwa mwaka wa masomo 2024/2025, wanafunzi wa diploma wanatakiwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:
- Awe Mtanzania mwenye umri usiozidi miaka 35 wakati wa kuomba mkopo;
- Awe amedahiliwa katika taasisi ya elimu inayotoa elimu ya ngazi ya kati nchini;
- Awe amekamilisha na kuwasilisha maombi ya mkopo kupitia mfumo wa maombi ya mkopo (OLAMS);
- Asiwe na ajira au mkataba wa kazi serikalini au sekta binafsi unaompatia mshahara au kipato;
- Awe amehitimu elimu ya Kidato cha Nne (CSEE), Cheti (astashahada) au Kidato cha Sita (ACSEE) ndani ya miaka mitano; yaani kati ya mwaka 2020 hadi 2024.
- Kwa mwanafunzi anayeendelea na masomo ahakikishe matokeo yake yanayomwezesha kuendelea na masomo yametumwa Bodi, kupitia Afisa Mikopo/uongozi wa Chuo.
Mbali na vigezo vya msingi, wanafunzi wanaweza kupewa kipaumbele zaidi ikiwa wanakidhi mojawapo ya vigezo vifuatavyo:
- Yatima: Kuwa yatima (amefiwa na mzazi mmoja au wote wawili).
- Kipato cha Chini: Kutoka katika familia yenye kipato cha chini inayopokea ruzuku kutoka TASAF au taasisi nyingine zinazofanana.
- Ulemavu: Kuwa na ulemavu au kuwa na mzazi mwenye ulemavu.
Umuhimu wa Vigezo: Vigezo hivi vinahakikisha kuwa mikopo inatolewa kwa wanafunzi wenye uhitaji mkubwa zaidi na wale ambao wana uwezo wa kufaulu katika masomo yao. Ni muhimu kuzingatia kwamba kutimiza vigezo hivi hakuhakikishii kupata mkopo, kwani HESLB pia huzingatia bajeti yake na vipaumbele vya kitaifa katika utoaji wa mikopo.
Jinsi ya Kuomba Mkopo kwa Wanafunzi wa Diploma 2024/2025
Maombi yote ya mkopo wa HESLB kwa mwaka wa masomo 2024/2025 yatafanyika kupitia mfumo wa mtandao wa OLAMS. Ili kuhakikisha maombi yanashughulikiwa bila matatizo, fuata hatua hizi:
Fungua Akaunti
- Tembelea tovuti rasmi ya HESLB na ufungue akaunti kwenye mfumo wa OLAMS (https://olas.heslb.go.tz/olams/pre-applicant).
- Hakikisha unatumia namba sahihi ya mtihani wa kidato cha nne, ile ile iliyotumika kuomba udahili chuoni.
Jaza Fomu ya Maombi
- Jaza fomu ya maombi ya mkopo kwa usahihi na ukamilifu.
- Pakua fomu sahihi kulingana na umri (chini ya miaka 18 au miaka 18 na kuendelea).
- Ambatisha nyaraka zote zinazohitajika (angalia sehemu ya “Nyaraka Muhimu” kwa maelezo zaidi).
Saini na Thibitisha:
- Saini fomu ya maombi na mkataba wa mkopo.
- Hakikisha fomu imesainiwa pia na viongozi wa serikali ya mtaa, mdhamini, na kamishna wa viapo.
Lipa Ada ya Maombi
- Lipa ada ya maombi ya TZS 30,000 kupitia benki au mitandao ya simu.
- Hakikisha una namba ya kumbukumbu ya malipo iliyotolewa na mfumo.
Wasilisha Maombi
- Pakia fomu zilizosainiwa na nyaraka zingine kwenye mfumo wa OLAMS.
- Hakikisha umewasilisha maombi kabla ya tarehe ya mwisho (31 Agosti 2024 kwa muhula wa Oktoba).
Baada ya Kuwasilisha
- Subiri HESLB ichambue maombi.
- Matokeo ya maombi yatatangazwa kupitia akaunti ya SIPA.
- Ikiwa umefanikiwa, utapokea mkopo kulingana na vigezo na vipaumbele vya HESLB.
Nyaraka Za Kuambatisha Wakati Wa Maombi Ya Mkopo
Zifuatazo ni nyaraka muhimu za kuambatisha kwenye maombi ya mkopo: –
- Cheti cha kuzaliwa kutoka mamlaka husika, ZCSRA kwa waombaji kutoka Zanzibar au Namba ya Uhakiki (verification number) kutoka RITA kwa waombaji kutoka Tanzania Bara;
- Vyeti vya vifo vya wazazi kuthibitisha uyatima kutoka mamlaka husika, ZCSRA kwa waombaji waliozaliwa Zanzibar au Namba ya Uhakiki (verification number) kutoka RITA kwa waombaji waliozaliwa Tanzania Bara;
- Barua kutoka RITA au ZCSRA kuthibitisha taarifa za kuzaliwa kwa waombaji waliozaliwa nje ya nchi. Kwa mwombaji ambaye mzazi wake amefariki nje ya nchi anapaswa kuwasilisha barua kutoka RITA au ZCSRA kuthibitisha taarifa za kifo.
- Fomu ya Kuthibitisha Ulemavu wa mwombaji au mzazi wake iliyoidhinishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) au Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO);
- Namba ya kaya ya Mnufaika kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuthibitisha ufadhili wa kiuchumi alioupata mwombaji wakati wa elimu yake ya sekondari.
Vipengele Na Viwango Vya Mkopo
Bodi itapanga mkopo kwa viwango vya fedha kulingana na mahitaji na ukomo wa bajeti. Mkopo utagawanywa katika vipengele vifuatavyo: Chakula na Malazi, Ada ya Mafunzo, Gharama za Vitabu na Viandikwa, Mahitaji Maalumu ya Kitivo, Gharama za Utafiti na Mafunzo kwa Vitendo. Mkopo utatolewa kwa ajili ya kugharimia vipengele vyote au baadhi ya vipengele, kama itakavyochambuliwa na kuidhinishwa.
- Chakula na Malazi: Kiwango cha juu kisichozidi TZS. 7,500.00 kwa siku kitatolewa kulingana na idadi ya siku mwanafunzi atakazokuwa chuoni kama inavyoelekezwa kwenye kalenda ya chuo husika. Kiasi hiki kitalipwa moja kwa moja kwa mwanafunzi.
- Ada ya Mafunzo: Kiwango cha juu cha ada kisichozidi TZS. 1,200,000.00 kwa mwaka kulingana na gharama zinazolipwa katika chuo husika kwa mwaka na kitalipwa moja kwa moja kwa chuo husika kama itakavyoidhinishwa na Bodi.
- Gharama za Vitabu na Viandikwa: Kiwango cha juu kisichozidi TZS. 200,000.00 kwa mwaka kwa vitabu na viandikwa na kitalipwa moja kwa moja kwa wanafunzi.
- Mahitaji Maalumu ya Kitivo: Kiwango cha juu kisichozidi TZS. 300,000.00 kwa mwaka kitatolewa na gharama husika zitalipwa moja kwa moja chuoni.
- Mafunzo kwa Vitendo: Kiwango cha juu kisichozidi TZS. 7,500.00 kwa siku hadi siku 56 kwa mwaka, kwa ajili ya Mafunzo kwa Vitendo kitatolewa. Kiasi hicho kitalipwa moja kwa moja kwa mwanafunzi.
Mapendekezo Ya Mhariri:
- Vigezo vya Kupata Mkopo Ngazi ya Diploma 2024/2025
- Mwisho Wa Kutuma Maombi Ya Mkopo HESLB 2024/2025
- Sifa Za Kupata Mkopo wa Bodi Ya Mikopo Tanzania HESLB
- Mwisho Wa Kutuma Maombi ya Vyuo Vya Diploma NACTVET
- Fomu za Kujiunga Na Shule Kidato Cha Tano 2024/2025
- Tarehe Ya Kuripoti Shule Kidato Cha Tano 2024
Swali langu ni hivi huyu mwanfunzi alimaliza kusoma astashahada ya kilimo na mifugo 2017 na form four alimaliza 2015 .lakini wazazi wake walipata ajali wakapata ulemavu mmoja na mwengine alipoteza maisha .je!?mtu huyu anaweza kupata mkopo wa deploma?
Ina maana mikopo tunapokea hata tunaoingia diploma mwaka wa kwanza
Ndio
Kuna dirisha lingine litakalo funguliwa baada ya mwisho wa kutuma maombi August 31 au hakuna?