HESLB na TRA Kushirikiana Katika Utoaji na Urejeshaji Mikopo
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameanzisha ushirikiano wa kipekee utakaosaidia kuboresha utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi.
Ushirikiano huu una lenga kubadilishana taarifa kati ya taasisi hizi mbili kwa lengo la kuimarisha mifumo ya huduma na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam, ikihudhuriwa na viongozi wakuu wa taasisi hizo. Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alieleza kuwa lengo la ushirikiano huo ni kuhakikisha taarifa za wanufaika wa mikopo zinapatikana kwa urahisi kupitia TRA, ili kuongeza kasi ya urejeshaji mikopo na kuboresha huduma za utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
“Kwa kushirikiana na TRA, tunaweza kupata taarifa muhimu zitakazotusaidia kuboresha huduma zetu, hasa katika utoaji wa mikopo na urejeshaji wake. Kupitia mabadilishano ya kanzidata, tutakuwa na uwezo wa kutambua changamoto zinazowakabili wanufaika na kuzitatua kwa haraka,” alisema Dkt. Kiwia.
Utekelezaji wa Maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan
Ushirikiano huu pia ni sehemu ya jitihada za kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye alihimiza taasisi za serikali kuhakikisha mifumo yao inasomana ifikapo Desemba 2024.
Dkt. Kiwia alisisitiza kuwa HESLB itahakikisha inakamilisha agizo hilo kabla ya muda uliowekwa ili kuhakikisha wanufaika wote wanarejesha mikopo kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
“Hili ni agizo muhimu kutoka kwa Mhe. Rais, na tunalichukulia kwa uzito mkubwa. Tumepanga kukamilisha mchakato huu kabla ya Desemba mwaka huu, ili kuhakikisha kuwa mifumo ya taasisi zote za serikali inashirikiana kwa ufanisi,” aliongeza Dkt. Kiwia.
Manufaa ya Ushirikiano kwa Wadau wa Mikopo
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Yusuph Mwenda, alieleza kuwa ushirikiano huu utawasaidia wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kupata fursa bora ya kurejesha mikopo yao kwa urahisi. Alitoa wito kwa wanufaika wa mikopo waliomaliza masomo yao kuhakikisha wanarejesha mikopo ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wengine wa kitanzania kuendelea kunufaika.
“Nawasihi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waanze kurejesha mikopo yao haraka. Wapo waliokopeshwa kabla yao na walifanikiwa kurejesha, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kwamba mikopo inarejeshwa kwa wakati,” alisema Kamishna Mwenda.
Jinsi Ushirikiano Utakavyofanya Kazi
Kupitia ushirikiano huu, TRA itatoa taarifa muhimu kuhusu mapato na hali ya kifedha ya wanufaika wa mikopo. Taarifa hizi zitasaidia HESLB kubaini wanufaika ambao wanapaswa kuanza kurejesha mikopo yao. Kwa kutumia kanzidata ya TRA, HESLB itakuwa na uwezo wa kufuatilia kwa karibu wanufaika wa mikopo wanaoendelea na ajira na kuhakikisha wanatekeleza jukumu lao la kurejesha mikopo.
Hii itapunguza mzigo wa kifedha kwa HESLB na kuhakikisha fedha za mikopo zinaongezeka na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi. Hatua hii ni muhimu katika kukuza usawa wa fursa za elimu kwa wote, huku ikiongeza uwajibikaji kwa wanufaika wa mikopo.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Muda wa Mwisho wa Maombi ya Mikopo wa HESLB 2024/2025 Waongezwa!
- Mwisho Wa Kutuma Maombi Ya Mkopo HESLB 2024/2025
- Jinsi Ya Kuomba Mkopo Wa Elimu Ya Juu HESLB 2024/2025
- Sifa Za Kupata Mkopo wa Bodi Ya Mikopo Tanzania HESLB
- Vyeti vya Kidato cha NNe (CSEE) 2023 Vipo Tayari – NECTA
- Majina ya Waliochaguliwa kujiunga na vyuo Vikuu 2024/2025
Leave a Reply