Fadlu Aanza Mikwara Kuelekea Dabi ya Kariakoo
Homa ya dabi ya Kariakoo imezidi kupanda, huku Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, akionyesha dhamira ya kuhakikisha Wekundu wa Msimbazi wanaibuka kidedea dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga. Katika mahojiano ya hivi karibuni, Fadlu ameweka wazi kuwa Simba ya sasa ni tofauti na ile iliyofungwa bao 1-0 na Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi Agosti.
Fadlu anaamini kuwa kikosi chake kimeimarika sana tangu mchezo huo, na wachezaji wake, hasa vijana, wamejifunza mengi kutoka katika dabi yao ya kwanza.
“Mchezo wa Ngao ya Jamii ulitusaidia sana,” alisema Fadlu. “Baadhi ya wachezaji wetu walikuwa ni mara ya kwanza kucheza dabi ya Tanzania, na sasa wameanza kuelewa nini maana ya michezo hiyo.”
Kocha huyo ameongeza kuwa wachezaji wake vijana sasa wana uzoefu zaidi na wataongeza umakini wakishirikiana na wachezaji wazoefu, hivyo Yanga watarajie kukutana na upinzani mkali zaidi.
Hata hivyo, Fadlu amesisitiza kuwa Simba hawaingii katika mchezo huu kwa lengo la kulipiza kisasi, bali wanataka kushinda ili kuvuna pointi tatu muhimu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Hatutaingia kwa kulipiza kisasi, ila kuendelea kupata uzoefu na kushinda kwa ajili ya kupata pointi tatu,” alisisitiza Fadlu.
Kocha huyo anakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu ambao wako katika majukumu ya timu za taifa. Hata hivyo, anaamini kuwa ataweza kuwajenga wachezaji waliobaki ili waweze kupambana vilivyo na Yanga.
“Kutokuwa na baadhi ya wachezaji waliokwenda kwenye vikosi vya timu ya taifa ni tatizo, lakini hata wapinzani wetu pia wanapitia changamoto hiyo,” alisema Fadlu.
Simba kwa sasa ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 13, nyuma ya vinara Singida Black Stars wenye pointi 16. Yanga ipo nafasi ya nne na pointi 12.
Dabi hii ya Kariakoo inatarajiwa kuwa yenye ushindani mkubwa na yenye kandanda safi, huku mashabiki wa pande zote mbili wakijiandaa kwa shangwe na nderemo. Je, Simba watafanikiwa kulipiza kisasi chao au Yanga wataendeleza ubabe wao?
Mapendekezo ya Mhariri:
- Max Nzengeli: “Hakuna Dabi Rahisi Duniani Kote”
- Ratiba ya NBC Championship Tanzania 2024/2025
- Morocco Ahimiza Ubora wa Umaliziaji wa Nafasi Kuelekea Mchezo wa Marudiano na DRC
- Simba Queen na JKT Queens Waanza na Moto Ligi Kuu wanawake
- Pamba Jiji FC Yafanya Vikao Vizito Baada ya Mwanzo Mbovu Ligi Kuu
- Coastal Union Yahamishia Mechi Zake Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha
Simba mjipange
kwa kosi hili
hamvuni point
hata moja
na hamuwez
kushinda labda
mshinde njaaa….!