Coastal Union Yahamishia Mechi Zake Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha
Klabu ya Coastal Union imetangaza rasmi kuuhamishia uwanja wake wa nyumbani kutoka jijini Dar es Salaam hadi Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Uamuzi huu unahitimisha tetesi zilizokuwa zikisambaa kwa muda mrefu kuhusu mpango wa viongozi wa timu hiyo kuihamisha Coastal Union kutoka Dar es Salaam ambapo ilikuwa ikitumia viwanja vya KMC Complex na Azam Complex kwa michezo yake ya nyumbani.
Awali, Coastal Union ililazimika kutumia viwanja hivyo kutokana na uwanja wake halisi wa Mkwakwani, uliopo Tanga, kufanyiwa ukarabati. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, uamuzi wa kuhamia Arusha umetokana na sababu kadhaa ikiwemo kuthamini mapendekezo ya wanachama na mashabiki, kuirudisha timu Kanda ya Kaskazini, na kuitikia ombi la mashabiki wa soka wa Arusha.
Mabadiliko Katika Benchi la Ufundi
Mbali na kuhamia Arusha, Coastal Union pia inatarajia kufanya mabadiliko katika benchi la ufundi. Abbas El Sabri, Ofisa Habari wa klabu hiyo, ametangaza kuwa timu hiyo itarudi uwanjani ikiwa na kocha mpya ambaye jina lake litatangazwa hivi karibuni.
“Tutatumia kipindi hiki cha kalenda ya FIFA kuendelea kukipa makali kikosi chetu kwani hatukuanza vizuri, lakini pia tutarudi upya tukiwa na nguvu, benchi letu likiwa limeimarishwa tukiwa na kocha mpya,” alisema Sabri.
Kwa mujibu wa Sabri, kocha huyo mpya ni mmoja wa makocha bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na alikuwa miongoni mwa waliohudhuria mchezo kati ya Coastal Union na Simba uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 Ijumaa iliyopita.
“Kwa sasa yupo Tanga tunamalizia mazungumzo kabla ya kumtangaza, tumeshampa malengo yetu na ameyakubali,” aliongeza Sabri.
Hadi kocha mpya atakapoteuliwa, Kwa sasa, nafasi ya Kocha Mkuu inashikiliwa na Joseph Lazaro, beki wa kushoto wa zamani wa timu hiyo, ambaye anatarajiwa kuongoza kikosi katika kipindi hiki kigumu. Timu hiyo inaendelea na mazoezi ili kujiandaa na changamoto za ligi huku wakitafuta njia za kuboresha matokeo yao.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Msimamo wa Ligi Kuu ya Zanzibar 2024/2025 PBZ premium League
- Mario Balotelli Aripotiwa Yupo Karibu Kurudi Italia
- Forest Kutoa Ofa ya Mkataba Mpya kwa Wood Kabla ya Uliopo Kumalizika
- Dortmund Yamsajili Yan Couto kwa €30 Milioni kutoka Manchester City
- Yanga Yajipa Nafasi ya Kutinga Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika
- Taifa Stars Yaangukia Pua Mbele ya DR Congo Kufuzu AFCON 2025
- Msimamo wa Kundi la Tanzania Kufuzu AFCON 2025
Leave a Reply