CAF Yaondoa Marufuku Uwanja wa Benjamin Mkapa

CAF Yaondoa Marufuku Uwanja wa Benjamin Mkapa

CAF Yaondoa Marufuku Uwanja wa Benjamin Mkapa:

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeufungulia rasmi Uwanja wa Benjamin Mkapa kutumika kwa mechi za kimataifa za mashindano. Uamuzi huu unafanyika siku 15 baada ya CAF kuufungia uwanja huo kutokana na ubora duni wa eneo la kuchezea, uliobainika katika ukaguzi uliofanywa wiki mbili zilizopita.

Hatua hii ni habari njema kwa klabu ya Simba, ambayo sasa itautumia uwanja huo kwa mechi yake ya marudiano ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, itakayochezwa Aprili 9 mwaka huu. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limethibitisha kuwa CAF imeridhishwa na maboresho yaliyofanywa kwenye eneo la kuchezea la uwanja huo.

CAF Yathibitisha Maboresho

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya TFF iliyotolewa Ijumaa, Machi 28, 2025, CAF imeuruhusu Uwanja wa Benjamin Mkapa kutumika kwa mechi za hatua ya robo fainali na nusu fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) na Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC) kwa msimu wa 2024/2025.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uwanja huo umeruhusiwa baada ya ukaguzi uliofanywa hivi karibuni na wakaguzi wa CAF, ambao wamebaini maboresho makubwa yaliyofanywa. Hata hivyo, CAF inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya maboresho hayo ili kuhakikisha viwango vinavyotakiwa vinaendelea kudumishwa.

CAF Yaondoa Marufuku Uwanja wa Benjamin Mkapa

Kabla ya tangazo hili, meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kueleza kuwa CAF ilikuwa imeonesha matumaini ya kuruhusu uwanja huo kutumika. Alieleza kuwa ukaguzi ulikwisha fanyika na majibu rasmi yalikuwa yakisubiriwa, lakini mazungumzo yalionesha kuwa maboresho makubwa yalikuwa yamefanyika kulinganisha na ukaguzi wa awali.

Ahmed Ally pia alikumbusha kuwa msemaji mkuu wa Serikali alishathibitisha kuwa uwanja huo upo tayari kutumika. Kwa msingi huo, Simba ilianza maandalizi yake kwa kuamini kuwa mechi yao dhidi ya Al Masry itachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku wakiwa na uhakika wa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Uwanja wa Benjamin Mkapa na Historia ya Simba

Katika miaka ya hivi karibuni, Uwanja wa Benjamin Mkapa umekuwa uwanja wa nyumbani wenye mafanikio makubwa kwa Simba katika mashindano ya klabu Afrika. Takwimu zinaonesha kuwa katika mechi zake 10 zilizopita za mashindano tofauti ya klabu Afrika zilizochezwa katika uwanja huo, Simba imepata ushindi mara saba, kutoka sare mbili, na kupoteza mara moja. Katika kipindi hicho, timu hiyo imefunga mabao 20 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita pekee.

Uamuzi huu wa CAF una maana kubwa kwa Simba SC na mashabiki wake, kwani wanatarajia kutumia faida ya kucheza katika uwanja wao wa nyumbani kwa mechi muhimu dhidi ya Al Masry. Aidha, hatua hii inathibitisha juhudi za TFF na mamlaka za michezo nchini katika kuhakikisha viwanja vya Tanzania vinakidhi viwango vya kimataifa.

Kwa sasa, wadau wa soka wanatarajia kuona viwango bora vya uwanja huo vikiendelea kuboreshwa ili kuepuka changamoto kama zile zilizosababisha marufuku ya awali.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Sowah Aweka Bayana Nia Yake Yakubeba Kiatu Cha Dhahabu
  2. Majeraha ya Goti Yamkosesha Alphonso Davies Mechi za Mwisho za Msimu
  3. Yanga Yavamia Dili la Fei Simba
  4. Silaha 6 Muhimu za Simba SC Zatangulizwa Misri
  5. Vita ya Top 4 Ligi Kuu Tanzania Bara Yapamba Moto
  6. Morocco Yaishushia Tanzania Kichapo cha 2-0, Mechi ya Kufuzu Kombe la Dunia 2026
  7. Safari ya Serengeti Boys Kuelekea Kombe la Dunia Yaanzia Morocco
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo