Amrouche Atangazwa Kocha Mpya wa Timu ya Taifa ya Rwanda
Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiwa halijatoa tamko rasmi kuhusu mustakabali wa kocha mkuu wa Taifa Stars, Adel Amrouche, kocha huyo ameibukia Rwanda baada ya kutangazwa rasmi kama kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo, maarufu kama ‘Amavubi’.
Shirikisho la Soka Rwanda (Ferwafa) limethibitisha uteuzi wa Amrouche, likimtangaza mchana huu kama kocha mkuu mpya wa Amavubi. Mbali na yeye, Ferwafa imewatangaza makocha wawili wazawa ambao wataunda benchi lake la ufundi. Erick Nshimiyimana atakuwa msaidizi wa kwanza, huku Dk. Carolin Braun akichukua nafasi ya msaidizi wa pili.
Katika mabadiliko mengine ndani ya Ferwafa, kocha Casa Mbungo ametangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya wanawake. Mbali na jukumu hilo, Mbungo pia atakuwa na wajibu wa kusimamia maendeleo ya soka chini ya kurugenzi ya ufundi.
Hatua ya Amrouche Kujiunga na Rwanda na Mgogoro Wake na CAF
Ujio wa Amrouche nchini Rwanda unakuja baada ya kushinda kesi dhidi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kesi iliyosababisha shirikisho hilo kulazimika kumlipa fidia. Hata hivyo, sintofahamu inazidi kutanda kuhusu jinsi Amrouche amefanikisha mkataba huu mpya wakati bado ana mkataba unaoendelea na TFF, ambao unatarajiwa kumalizika mwakani.
Kufikia sasa, viongozi wa TFF hawajatoa kauli rasmi kuhusu uhamisho huu wa ghafla wa kocha huyo.
Ikumbukwe kuwa Amrouche alikuwa akisumbuliwa na adhabu kutoka CAF baada ya kupigwa marufuku kwa mechi nane. Adhabu hiyo ilitokana na kauli tata aliyotoa dhidi ya Shirikisho la Soka la Morocco, akidai kuwa shirikisho hilo lina ushawishi mkubwa katika maamuzi ya CAF. Kauli hizo zilisababisha CAF kumtoza faini ya Dola 10,000, huku TFF nayo ikichukua hatua za kumsimamisha na kumkabidhi timu kwa makocha wazawa, Hemed Morocco na Juma Mgunda.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuona iwapo litatoa tamko rasmi juu ya uhamisho huu wa ghafla wa kocha wao kuelekea Rwanda.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Baraka Majogoro Karibu Kujiunga na Orlando Pirates
- Hat Trick Dhidi ya Coastal Yampa Mukwala Mzuka Kuelekea Dabi ya Kariakoo
- Matokeo ya Coastal Union vs Simba Leo 01/03/2025
- Kikosi cha Simba vs Coastal Union Leo 01/03/2025
- Coastal Union Vs Simba Leo 01/03/2025 Saa Ngapi?
- Mashujaa FC Yathibitisha Kumfuta Kazi Kocha Mohamed Abdallah ‘Baress’
- Arajiga Kuchezesha Mechi ya Kufuzu Kombe La Dunia 2026
- Twiga Stars Yavuka Raundi ya Pili WAFCON Baada ya Sare Dhidi ya Guinea
- Antony Afutiwa Kadi Nyekundu, Sasa Ruksa Kuivaa Madrid
Leave a Reply