Al Ahly Yamtimua Kocha Marcel Koller Baada ya Kutolewa Klabu Bingwa Afrika
Klabu ya Al Ahly imemtimua rasmi kocha wake mkuu, Marcel Koller, siku moja tu baada ya timu hiyo kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa leo, Jumamosi Aprili 26, 2025, uongozi wa Al Ahly umetangaza kuwa umefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Koller kwa maridhiano. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya tathmini ya kina kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Sundowns katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali, uliochezwa Ijumaa Aprili 25.
Kwa kutumia sheria ya bao la ugenini, Mamelodi Sundowns waliibuka washindi baada ya mchezo wa kwanza nchini Afrika Kusini kumalizika kwa sare tasa. Hali hiyo ilifanya Al Ahly kupoteza nafasi ya kutetea taji lao la Afrika, na hivyo kuibua mabadiliko ya haraka ndani ya benchi la ufundi.
Katika sehemu ya taarifa yao, Al Ahly walisema:
“Baada ya tathmini ya kina kufuatia matokeo dhidi ya Mamelodi, bodi ya klabu imeamua kuachana rasmi na kocha Marcel Koller. Majadiliano ya kuvunja mkataba kwa makubaliano yanaendelea kwa njia inayoheshimu mchango wa kocha na hadhi ya klabu.”
Marcel Koller, raia wa Uswisi, alijiunga na Al Ahly mwaka 2022 na ndani ya muda wa chini ya miaka mitatu, aliisaidia klabu hiyo kutwaa mataji makubwa. Miongoni mwa mafanikio yake ni kushinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mataji mawili ya Ligi Kuu ya Misri, Kombe la Misri, pamoja na ubingwa wa Super Cup ya Afrika.
Uongozi wa Al Ahly umetangaza kwa heshima kubwa mafanikio ya Koller na timu yake ya benchi la ufundi, ukisema kuwa wanawashukuru wote kwa kujitolea kwao na mafanikio waliyoyapata pamoja na klabu hiyo kubwa ya Afrika.
Mapendekezo ya Mhariri:
Leave a Reply