JKU Yaiondoa Singida Black Stars Kombe la Muungano
Klabu ya JKU kutoka kisiwani Unguja imefuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Muungano baada ya kuibwaga Singida Black Stars ya Tanzania Bara kwa penalti 6-5. Mchezo huo wa robo fainali ulipigwa Aprili 24, 2025, kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba. Katika muda wa kawaida wa dakika 90, timu zote zilitoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mchezo huo uliokua na ushindani mkali, Singida Black Stars ilikuwa ya kwanza kuona lango kupitia mshambuliaji wao Victorien Adebayor aliyeipatia timu yake bao la mapema dakika ya 6. Bao hilo liliongeza shinikizo kwa wapinzani, na dakika ya 25, Iddi Khalid ‘Gego’ akaongeza bao la pili kwa upande wa Singida, na kuifanya JKU kuwa katika hali ya kufukuzia matokeo mapema kabisa.
Hata hivyo, JKU haikukata tamaa. Dakika ya 28, Tariq Mohamed alisawazisha kwa mkwaju wa penalti, kabla ya Fredy Seleman kuisawazishia kikamilifu JKU kwa bao la pili katika dakika ya 45+3, na kufanya timu kwenda mapumziko zikiwa sare ya 2-2.
Kipindi cha pili kilichezwa kwa tahadhari kubwa huku kila timu ikitafuta bao la ushindi, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda. Hali hiyo ilisababisha mshindi wa mchezo kuamuliwa kwa njia ya mikwaju ya penalti.
Katika mikwaju hiyo ya penalti, Singida Black Stars ilifunga penalti tano kupitia Damaro Mohamed Camara, Frank Assinki, Victorien Adebayor, Anthony Tra Bi Tra, na Edmund John. Hata hivyo, walikosa penalti tatu muhimu kupitia Edward Charles Manyama, Joe Ephraim Makoye na Elvis Rupia – makosa ambayo yaliigharimu timu hiyo nafasi ya kusonga mbele.
Kwa upande wa JKU, wachezaji wao walionesha utulivu mkubwa walipofunga penalti zao sita kupitia Habeeb Abiola, Mohamed Ali, Tarik Mohamed Mikonga, James Ambrose, Hassan Makame, na Mohamed Mtumwa. Ingawa Abubakar Nidhar na Koffy Hamza walikosa, mafanikio ya wachezaji wenzao yaliihakikishia JKU ushindi wa 6-5.
Kwa sasa, JKU inasubiri mshindi wa robo fainali ya pili itakayopigwa Aprili 25, 2025 kati ya KMKM na Azam FC, mchezo utakaofanyika saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa Gombani. Timu itakayoshinda itakutana na JKU katika nusu fainali ya Aprili 28, 2025.
Michuano ya Kombe la Muungano inaendelea kufanyika kwenye Uwanja huo huo wa Gombani, ikihusisha jumla ya timu nane — nne kutoka Tanzania Bara na nne kutoka Zanzibar — na inatarajiwa kufikia kilele chake Mei 1, 2025.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Wachezaji Saba Watimuliwa Zanzibar Kwa Tuhuma Za Kubeti
- Refa Mpya Apangwa Kuongoza Mechi ya Stellenbosch Dhidi ya Simba
- Ratiba ya Kombe la Muungano 2025
- Kikosi cha Simba Kitakachoivaa Stellenbosch Afrika Kusini April 27
- Timu Zinazoshiriki Kombe la Muungano 2025
- Yanga Yaishushia Fountain Gate Kichapo Cha 4-0 na Kuweka Rekodi
- Kikosi cha Yanga VS Fountain Gate Leo 21/04/2025
Leave a Reply