Ifahamu Timu ya Stellenbosch Wapinzani Wa Simba Nusu Fainali Kombe la Shirikisho CAF
Klabu ya Stellenbosch FC ni moja ya timu changa zaidi barani Afrika lakini yenye historia ya kipekee na mafanikio ya kuvutia ndani ya muda mfupi. Ilianzishwa mwaka 2016 huko Afrika Kusini baada ya kampuni ya Stellenbosch Academy of Sport (SAS) kuinunua klabu ya Vasco Da Gama iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza (National First Division). Hatua hiyo iliashiria mwanzo wa safari mpya kwa mji wa Stellenbosch, uliopo takriban kilomita 50 mashariki mwa Cape Town, kuwa na timu ya kwanza kabisa kushiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Kupanda Daraja na Mafanikio ya Awali
Msimu wa 2018/2019, Stellenbosch FC iliandika historia kwa kutwaa ubingwa wa National First Division kwa pointi 56 ndani ya mechi 30, hivyo kuipandisha rasmi DStv Premiership (Ligi Kuu ya Afrika Kusini). Tangu wakati huo, wameendelea kuwa miongoni mwa timu zinazotoa ushindani mkubwa dhidi ya vigogo wa soka la Afrika Kusini kama Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.
Katika msimu wao wa kwanza (2019/2020) kwenye DStv Premiership, waliweza kumaliza nafasi ya 10 kati ya timu 16, jambo lililowafanya wachukuliwe kwa uzito zaidi licha ya kuwa wageni kwenye ligi hiyo.
Stellenbosch 2024/2025: Kizazi Kipya Chenye Njaa ya Mafanikio
Kwa sasa, Stellenbosch FC inashika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa DStv Premiership wakiwa na pointi 35 huku wakibakiza michezo mitatu mkononi. Ni timu iliyojijenga juu ya msingi wa kuendeleza vipaji, zaidi ya asilimia 60 ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza wametoka kwenye akademia yao ya ndani. Miongoni mwa wachezaji wanaovutia zaidi msimu huu ni Devin Titus mwenye magoli 6 kwenye ligi na 2 CAF, pamoja na Ashley Cupido mwenye magoli 5 kwenye ligi.
Safari ya Stellenbosch Katika Kombe la Shirikisho CAF 2024/2025
Stellenbosch FC imeweka rekodi mpya kwa klabu hiyo kwa kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup). Safari yao ilianza kwenye hatua ya awali kabisa ambapo waliwagaragaza Nsingizini kutoka Eswatini:
Hatua ya Awali:
- Nsingizini 0-3 Stellenbosch (Ugenini)
- Stellenbosch 5-0 Nsingizini (Nyumbani)
Hatua ya Pili:
- Stellenbosch 2-0 Vita Club (Nyumbani)
- Vita Club 1-1 Stellenbosch (Ugenini)
Hatua ya Makundi – Kundi B:
- Stade Malien 2-0 Stellenbosch
- Stellenbosch 3-1 Berkane
- Lunda Sul 0-1 Stellenbosch
- Stellenbosch 2-0 Lunda Sul
- Stellenbosch 2-0 Stade Malien
- RS Berkane 5-0 Stellenbosch
Wakiwa na pointi 9 baada ya mechi 6, Stellenbosch walitinga robo fainali pamoja na RS Berkane kutoka kundi B.
Robo Fainali:
- Stellenbosch 0-0 Zamalek (Nyumbani)
- Zamalek 0-1 Stellenbosch (Ugenini)
Ushindi huo dhidi ya mabingwa watetezi wa CAF Confederation Cup, Zamalek SC ya Misri, uliwapa nafasi ya kuingia kwenye hatua ya nusu fainali ambapo sasa wanakutana na Simba SC ya Tanzania.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Simba na Stellenbosch Kukipiga Zenji Nusu Fainali Kombe la Shirikisho CAF
- Ratiba ya CRDB Federation Cup Fixtures 2024/2025
- Vilabu Bora Afrika 2024/2025 (CAF Club Ranking)
- Ratiba ya Nusu Fainali Klabu Bingwa Afrika CAF 2024/2025
- Al Ahly Yashindwa Kutamba Mbele ya Pyramids Pungufu
- Mpanzu na Kibu Wamtia Hofu Kocha wa Stellenbosch
- Ratiba ya Simba Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Afrika
- Kikosi cha Yanga vs Azam Leo 10/04/2025
Leave a Reply