Miguel Cardoso Akabidhiwa Mikoba ya Ukocha Mamelodi

Miguel Cardoso Akabidhiwa Mikoba ya Ukocha Mamelodi

Miguel Cardoso Akabidhiwa Mikoba ya Ukocha Mamelodi

Klabu ya Mamelodi Sundowns imemtangaza rasmi Miguel Cardoso kuwa kocha mkuu, akichukua nafasi ya Manqoba Mngqithi, ambaye aliachishwa kazi kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya klabu hiyo. Uteuzi huu unaleta matumaini mapya kwa mabingwa hao wa Afrika Kusini huku wakilenga kufanikisha malengo makubwa msimu huu na msimu ujao.

Cardoso, raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 52, ni kocha mwenye uzoefu mkubwa akiwa amewahi kuvinoa vilabu vikubwa barani Ulaya na Afrika. Akiwa na rekodi ya mafanikio katika klabu kama Rio Ave ya Ureno, Nantes ya Ufaransa, Celta Vigo ya Hispania, na AEK Athens ya Ugiriki, Cardoso anatua Sundowns akiwa na wasaidizi wake watatu, Fabio Fernandes, Pedro Azevedo, na João Araújo.

Hivi karibuni, Cardoso alikua kocha wa klabu ya Esperance ya Tunisia, ambapo aliipeleka katika fainali ya TotalEnergies CAF Champions League msimu wa 2023/24, lakini walipoteza kwa jumla ya mabao 1-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri. Baada ya matokeo hayo, aliachana na Esperance mnamo Oktoba 2024.

Miguel Cardoso Akabidhiwa Mikoba ya Ukocha Mamelodi

Malengo Makubwa ya Cardoso na Mamelodi Sundowns

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne, Cardoso alionyesha furaha yake na matumaini makubwa kuhusu jukumu lake jipya. “Ni heshima kubwa kuwa hapa. Klabu hii ina historia kubwa na utambulisho wa kipekee. Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha tunaleta furaha kwa mashabiki na kuiwakilisha klabu kwa njia bora zaidi,” alisema Cardoso.

Kocha huyo alisisitiza kuwa malengo yake ni kushinda mataji mengi na kuongeza urithi wa mafanikio ya klabu hiyo. “Nataka kukumbukwa kama mmoja wa makocha bora wa klabu hii, sawa na Pitso Mosimane, Rulani Mokwena, Steve Komphela, na Manqoba,” aliongeza.

Miguel Cardoso anakabiliwa na jukumu la kurekebisha mwenendo wa timu kwenye michuano ya TotalEnergies CAF Champions League, ambapo Sundowns wameanza hatua ya makundi kwa sare mbili dhidi ya Maniema Union (0-0, nyumbani) na AS FAR (1-1, ugenini). Mechi yao ijayo ni dhidi ya Raja Casablanca, ambayo itakuwa kipimo muhimu kwa mwelekeo wa timu.

Zaidi ya hilo, Cardoso atakuwa na jukumu kubwa la kuwaandaa Mamelodi Sundowns kwa michuano ya Kombe la Dunia la Klabu la FIFA 2025 litakalofanyika Marekani. Sundowns wamepangwa kundi moja na Borussia Dortmund ya Ujerumani, Fluminense ya Brazil, na Ulsan HD ya Korea Kusini. Michuano hiyo itakuwa fursa adhimu kwa Cardoso kuonyesha uwezo wake wa kiufundi na kuongeza heshima ya klabu katika ngazi ya kimataifa.

Mabadiliko katika Benchi la Ufundi

Kufuatia uteuzi wa Cardoso, benchi la ufundi la Sundowns limepata sura mpya huku makocha Steve Komphela na Kennedy Mweene wakibaki kuwa sehemu ya timu ya kiufundi. Ujio wa Fabio Fernandes, Pedro Azevedo, na João Araújo kama wasaidizi wa Cardoso unatarajiwa kuimarisha mbinu na mikakati ya timu kuelekea mafanikio makubwa.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Viingilio Mechi ya Simba VS CS Sfaxien 15/12/2024
  2. Timu Zinazoshiriki Mapinduzi cup 2025
  3. Ndoa Ya Coastal na Ley Matampi Yavunjika Rasmi
  4. Mapinduzi Cup 2025 Kuchezwa na Timu za Taifa Badala ya Vilabu
  5. Kocha Ramovic Aeleza Sababu za Yanga Kushindwa Mbele ya Waarabu
  6. Yanga Karibu Kumsajili Kelvin Nashon kutoka Singida
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo