Simba Yachezea Chuma 2-1 Dhidi ya CS Constantine
Kipigo cha Wekundu wa Msimbazi leo kimekuwa ni muendelezo mbaya kwa timu za Tanzania, baada ya juzi usiku, Yanga nao kufumuliwa mabao 2-1 na MC Alger ya Algeria. Hali hii imeongeza shinikizo kwa vilabu vya Tanzania katika michuano ya kimataifa ya Afrika.
Katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui, mji wa Constantine nchini Algeria, Simba SC ilishindwa kufurukuta mbele ya CS Constantine na kulazimika kukubali kichapo cha mabao 2-1.
Mechi hiyo ilikuwa ya raundi ya pili ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, na licha ya juhudi kubwa kutoka kwa kikosi cha Simba, mabao mawili ya haraka ndani ya dakika tano za kipindi cha pili yaliwanyong’onyesha kabisa.
Mchezo ulianza huku mvua kubwa ikinyesha, lakini haikuzuia timu zote mbili kuonesha kiwango bora cha soka. Dakika za mwanzo zilitawaliwa na mashambulizi ya kushtukiza kabla ya Simba kutawala mchezo na kutengeneza nafasi za kutosha kufunga.
Dakika ya 24, juhudi za Simba zilizaa matunda kupitia kwa nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, aliyefunga bao tamu kwa ustadi mkubwa. Tshabalala alipokea krosi safi na kupiga mpira uliomshinda kipa wa Constantine, Kheireddine Boussouf, na kuupachika wavuni. Bao hili liliongeza kasi ya mchezo, huku Simba wakitawala kipindi cha kwanza na kuingia mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja.
Kipindi cha Pili: Wenyeji Wacharuka
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kutoka kwa wenyeji, ambao walifanikiwa kusawazisha na kuongeza bao la pili ndani ya dakika tano. Beki wa Simba, Abdulrazack Hamza, alijifunga dakika ya 48 katika harakati za kuokoa mpira, hali iliyopelekea Constantine kusawazisha.
Dakika mbili baadaye, Brahim Dib aliiandikia CS Constantine bao la pili kwa shuti kali, na kuiacha Simba ikihangaika kurudi kwenye mchezo. Matatizo yaliendelea pale Hamza alipojeruhiwa dakika ya 55, na nafasi yake kuchukuliwa na Debora Mavambo.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids, alifanya mabadiliko makubwa akiwatoa Leonel Ateba na Tshabalala, na nafasi zao kuchukuliwa na Valentin Nouma na Steven Mukwala. Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuzaa matunda, huku Simba wakishindwa kupata bao la kusawazisha.
Msimamo wa Kundi A
Matokeo haya yamewaacha Simba katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi A, wakiwa na pointi tatu tu. CS Constantine inaongoza kundi hilo kwa pointi sita, baada ya kushinda michezo miwili mfululizo, ikiwemo dhidi ya Watunisia wa CS Sfaxien.
Simba sasa inarejea nyumbani kwa maandalizi ya mechi yao ya raundi ya tatu dhidi ya CS Sfaxien, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili ijayo.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Msimamo Kundi la Simba Kombe la Shirikisho CAF 2024/2025
- Matokeo ya CS Constantine vs Simba Leo 08/12/2024
- Kikosi cha Simba Vs CS Constantine Leo 08/12/2024
- Ratiba ya Mechi za Leo 08 December 2024
- Dodoma Jiji Yatolewa Kombe la Shirikisho na Leo Tena kwa Penalti
- CS Constantine vs Simba Leo 08/12/2024 Saa Ngapi?
- Msimamo wa Kundi la Yanga Klabu Bingwa Afrika CAF 2024/2025
- Yanga Yapasuka Tena Klabu Bingwa, Yachapwa 2-0 na MC Alger
Leave a Reply