Azam FC Yaibuka na Ushindi wa 2-1 dhidi ya Singida Black Stars

Azam FC Yaibuka na Ushindi wa 2 1 dhidi ya Singida Black Stars

Azam FC Yaibuka na Ushindi wa 2-1 dhidi ya Singida Black Stars

Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Ramadhan Nswanzurimo, ameanza kwa changamoto kubwa katika majukumu yake mapya baada ya kikosi chake kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Azam kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex. Matokeo haya yameweka shinikizo kubwa kwa kocha huyo mpya, ambaye aliteuliwa baada ya mabadiliko ya kiufundi ndani ya klabu.

Azam FC Yaibuka na Ushindi wa 2-1 dhidi ya Singida Black Stars

Ramadhan Nswanzurimo aliteuliwa rasmi Novemba 25, 2024, kuchukua nafasi ya Patrick Aussems aliyesimamishwa kazi pamoja na msaidizi wake Denis Kitambi kufuatia matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Nswanzurimo kuiongoza timu hiyo katika mchezo wa ushindani tangu uteuzi wake.

Mchezo huu ulikuwa na kasi kubwa, huku Azam FC ikionekana kuwa na mipango madhubuti ya ushambuliaji. Bao la kwanza kwa Azam lilifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 38 baada ya kumalizia pasi safi kutoka kwa kiungo mshambuliaji Idd Seleman ‘Nado’. Bao hilo lilikuwa la tatu kwa Feisal msimu huu katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dakika ya 56, mshambuliaji Mkolombia Jhonier Blanco aliongeza bao la pili kwa Azam FC, tena akipokea pasi ya Nado. Blanco, aliyesajiliwa kutoka Aguilas Doradas ya Colombia, alifikisha bao lake la pili msimu huu.

Singida Black Stars walipata bao lao pekee dakika ya 62 kupitia mshambuliaji Mkenya Elvis Rupia, aliyemalizia krosi ya kiungo Josaphat Arthur Bada. Bao hilo limemfanya Rupia kufikisha mabao matano msimu huu.

Kwa ushindi huu, Azam FC inaendelea kuwa na rekodi bora msimu huu. Kikosi hicho hakijapoteza mchezo wowote katika mechi saba zilizopita tangu kufungwa mabao 2-0 na Simba SC Septemba 26, 2024, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Tangu Kocha Rachid Taoussi ateuliwe kuiongoza Azam FC Septemba 7, 2024, timu hiyo imecheza mechi 11 za Ligi Kuu, kushinda minane, sare mbili, na kupoteza moja. Katika michezo 12 ya msimu huu, Azam FC imekusanya pointi 27, ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa imefunga mabao 16 na kuruhusu manne tu.

Kwa upande mwingine, Singida Black Stars wamecheza michezo 12 msimu huu, wakishinda saba, sare tatu, na kupoteza miwili. Wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 24, mabao 16 ya kufunga, na nyavu zao kutikiswa mara nane.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Kikosi cha Azam VS Singida Black Stars Leo 28/11/2024
  2. Matokeo ya Azam VS Singida Black Stars Leo 28/11/2024
  3. Ratiba ya Mechi Za Leo 28/11/2025
  4. Simba Yafungua Michuano ya Makundi ya CAF kwa Ushindi wa 1-0
  5. Msuva Asubiri Mkataba Mpya Mnono Al-Talaba SC
  6. Kocha Kagera amsifu Charles Boniface Mkwasa: ‘Kocha bora nchini’
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo