Azam Yashindwa Kutamba Ugenini, Singida yarejea kileleni

Azam Yashindwa Kutamba Ugenini, Singida BS Yarejea Kileleni

Timu ya Singida Black Stars imefanikiwa kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti, Singida. Hii ni sare ya kwanza kwa Singida msimu huu, lakini bado imewapa nafasi ya kukwea kileleni kwa alama 13, sawa na Fountain Gate.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani wa hali ya juu, huku timu zote zikionyesha nia ya kutaka kupata ushindi. Singida Black Stars walitangulia kupata bao la kuongoza dakika ya 15 kupitia kwa mshambuliaji wao mahiri kutoka Kenya, Elvis Rupia, baada ya kipa wa JKT, Yacoub Suleiman, kushindwa kuudhibiti mpira alioupangua. Bao hili liliwapa matumaini Singida kuwa wangeendelea na mfululizo wao wa ushindi baada ya kushinda michezo minne mfululizo kabla ya kukutana na JKT Tanzania.

JKT Tanzania, ambao hawakukata tamaa, waliongeza mashambulizi mara baada ya bao hilo la Singida, na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 45 baada ya Ismail Aziz Kader kuchezewa vibaya na beki wa Singida, Khalid Habib Idd, na mwamuzi kuamuru penalti. Hata hivyo, penalti hiyo iliyopigwa na Hassan Dilunga haikuzaa matunda kwani kipa wa Singida, Metacha Mnata, aliokoa mkwaju huo kwa ustadi mkubwa.

Mwishowe, dakika ya 67 ya kipindi cha pili, Wilson Nangu aliisawazishia JKT Tanzania bao kwa shuti kali ambalo lilimshinda Mnata, likiwa ni bao lake la kwanza msimu huu tangu ajiunge na JKT.

Nafasi ya Singida Black Stars Kurejea Kileleni

Licha ya sare hiyo, Singida Black Stars bado walifanikiwa kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 13. Kwa tofauti ya mabao tu ndiyo wanaongoza mbele ya Fountain Gate ambao pia wana pointi sawa. Ushindani huu wa karibu unaashiria kuwa mbio za ubingwa zitakuwa kali msimu huu.

Azam FC Yazidiwa Nguvu na Mashujaa FC

Azam Yashindwa Kutamba Ugenini, Singida yarejea kileleni

Katika mchezo mwingine muhimu wa Ligi Kuu, Azam FC ilibanwa mbavu na Mashujaa FC baada ya kutoka sare ya 1-1 katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma. Azam FC, iliyokuwa chini ya kocha mpya Mmorocco, Rachid Taoussi, haijawa na msimu mzuri, kwani hii ni sare yao ya tatu msimu huu baada ya michezo sita. Kikosi hicho kinachojaribu kurejea kwenye kiwango bora bado kinakosa matokeo thabiti, jambo ambalo linaweza kuwa changamoto kwao kwenye mbio za ubingwa.

Mapendekezo ya Mhariri:

Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo